Makamu Wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. Mohammed Gharib Bilal pichani, ameiwakilisha Tanzania katika Mkutano wa Umoja wa Afrika unaojadili namna ya
kumaliza Baa la Njaa katika nchi za Afrika. Mkutano huo wa siku moja umefanyika
jijini Addis Ababa, Ethiopia Jumatatu Julai Mosi, 2013 ambapo nchi washiriki
wamekumbusha kuhusu Azimio la Maputo walilolitoa miaka 10 iliyopita yaani mwaka
2003, azimio lililolenga kukabiliana na Njaa na Utapiamlo.
Azimio hilo lililenga kuzitaka nchi za Afrika
kukabiliana na Baa la Njaa sambamba na kuhakikisha kuwa wananchi wa Bara hili,
si tu kwamba wanapata uhakika wa chakula, bali kula chakula bora chenye
virutubisho vinavyohitajika katika kulinda afya za binadamu na hivyo kuwa na
uwezo wa kukabiliana na magonjwa. Pia azimio hilo lilizitaka nchi wanachama wa
Umoja wa Afrika kuhakikisha zinatanua bajeti zake za Kilimo ili zifikia
asilimia 10 ya Bajeti Kuu na pia kukifanya Kilimo kuchangia kwa asimilia 6
katika ukuaji wa uchumi wa nchi za Afrika.
Katika mkutano huo, Mheshimiwa Makamu wa Rais
alieleza kuwa Tanzania inashirikiana bega kwa bega na nchi za Afrika katika
kuhakikisha kuwa Bara hili linakabiliana vilivyo na baa la njaa na hivyo
kutokomeza Baa hilo kama nchi hizo zilivyokubaliana katika mkutano uliofanyika
Maputo mwaka 2003 uliopendekeza pia kuwa nchi za Afrika ziwe zimefanikiwa
kukabiliana na Baa la Njaa na Utapiamlo ifikapo mwaka 2025.
Katika maelezo yake, Mheshimiwa Makamu wa Rais
alifafanua kuwa Tanzania imepiga hatua katika kilimo kupitia mpango wa Kilimo
Kwanza na pia mpango wa kukuza uzalishaji kwa kutumia kanda maalum maarufu kama
SAGGOT (unaojumuisha mikoa iliyo na uwezo wa kuzalisha chakula kwa wingi)
umeanza kukubalika na kuwa mpango wa nchi nyingi za Afrika. Hata hivyo
Mheshimiwa Makamu wa Rais alifafanua pia kuwa, ukuzaji wa Kilimo unapaswa
kuambatana na sekta nyingine kama Nishati, Miundombinu, Viwanda na Biashara.
Umuhimu wa kukuza sekta hizo unatokana na ukweli
kuwa, zinachangia kukuza kilimo, kukifanya kuwa na tija na pia kutoa unafuu wa
uzalishaji kwa wakulima. Tena kwa kukuza sekta hizo, Afrika inaweza kupiga
hatua kubwa kwani tatizo la uzalishaji halitokani na upungufu wa uzalishaji tu,
bali hata pale panapokuwa na uzalishaji mkubwa, kuna maeneo ambayo mazao
yameshindwa kulifikia soko ama kufikishwa kwa watu wenye mahitaji.
Awali akichagia katika mkutano huo, Rais Mstaafu
wa Brazil Lula da Silva alisema njaa ni jambo la kijamii, linalochangiwa kwa
kiasi kikubwa na binadamu wenyewe hasa pale mtaji na kipato kinapobakia kuwa
katika mikono ya wachache wakati wengi wakiambulia patupu.
Rais Lula pia alimnukuu Hayati Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kusema; “kama mnataka maendeleo lazima
mshirikishe wananchi wote.” Kwa kutumia nukuu hii, Rais Lula anasisitiza kuwa,
Afrika inapaswa kuwa na mipango inayoshirikisha wananchi ili iwasaidie kukua
kiuchumi na kukabiliana na matatizo yanayowakabili katika maisha yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika
Dkt. Nkosazana Zuma alisema barani Afrika kuna changamoto kubwa inayowakabili
akina mama na moja ni kubwa ni kukosa fursa ya kumiliki ardhi hali inayofanya
uzalishaji kuwa duni. “Jambo hili linaweza kubadilishwa na sisi, tunaweza
kubadili tamaduni zetu kwa kuwa tunatambua mchango mkubwa wa akina mama katika
Kilimo. Hata hivyo, kama hatutafanya mabadiliko akina mama watabakia nyuma na
bara la Afrika litazidi kukabiliana na Baa la Njaa,” alisema.
Naye Rais Mstaafu wa Nigeria Olesegun Obasanjo
aliueleza mkutano huo kuwa, zipo tamaduni barani Afrika ambazo zinawabagua
wanawake japokuwa ndio wazalishaji zaidi. Pia akaongeza kuwa, wanawake
wasitumike katika shughuli za kisiasa tu bali wawezeshwe ili kufanikisha azma
ya Afrika kukabiliana na njaa.
Makamu wa Rais katika mkutano huo ameambatana na
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Injinia Christopher Chiza pamoja na Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mahadhi Juma Maalim. Katika
Mkutano huo pia viongozi mbalimbali wamehudhuria akiwemo Rais Mstaafu wa Brazil
Lula da Silva, Rais Mstaafu wa Nigeria Olesegun Obasanjo, Rais Mstaafu wa Ghana
John Kuofor.
Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni Mkurugenzi wa
Shirika la Chakula Duniani, Jose Graziano da Silva, Mwenyekiti wa Kamisheni ya
Afrika Dkt. Nkosazana Zuma, Rais wa Sudan, Benin na wawakilishi wa nchi
mbalimbali ambazo ni wajumbe wa Umoja wa Afrika.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Ethiopia Julai 02,
2013.
No comments:
Post a Comment