https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, July 15, 2013

DRFA yaipongeza Friends Rangers

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
CHAMA ya Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kimeipongeza timu ya Friends Rangers kwa kufuzu kucheza Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao baada ya jana Jumapili kuifunga Polisi Jamii ya mkoani Mara mabao 3-1.

Msemaji wa DRFA, Mohamed Mharizo
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Julai 6 kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma, Polisi waliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Katika mechi ya marudiano iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam na kuchezeshwa na mwamuzi Hans Mabena kutoka Tanga, Rangers walipata mabao yao kupitia kwa Robert Katabi katika dakika ya 53, Bakari Bakari dakika ya 67 na Mick Castro dakika ya 87.

Bao la Polisi lilifungwa na Faustine Faru katika dakika ya 68 na hivyo kuipa tiketi ya Friends Rangers kufuzu kucheza Daraja la Kwanza kwa jumla ya mabao 3-2.

Ofisa Habari wa DRFA, Mohamed Mharizo, amesema ni faraja kwao kuona Friends Rangers imetinga Ligi Daraja la Kwanza na kuuwakilisha vyema Mkoa wa Dar es Salaam.

“Kwa niaba ya DRFA nachukua fursa hii kuwapongeza wachezaji, viongozi na mashabiki wa Friends Rangers kwa uvumilivu na subra waliyokuwa nayo katika kipindi chote cha ushiriki wa Ligi ya Mabingwa wa Mkoa, bado tupo pamoja nao katika kufanikisha timu hiyo inafanya vizuri zaidi na hatimaye kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara,” alisema Mharizo.

Friends Rangers inaungana na Kimondo FC ya Mbeya na Stand United ya Shinyanga kucheza Ligi Daraja la Kwanza.

Wawakilishi wengine kutoka Mkoa wa Dar es Salaam katika Ligi ya Mabingwa wa Mikoa walikuwa Red Coast na Abajalo ambazo ziliaga michuano katika hatua za awali.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...