Na Kambi
Mbwana, Dar es Salaam
WADAU wa michezo,
hususan viongozi wao kwa ujumla wanaangamia kwa kukosa maarifa. Hali hii
inasababisha juhudi zinazofanywa kuwa za zimamoto huku nchi nyingine
zikisoganga mbele.
Ivory Coast ni Taifa linalofanya vema katika soka wakati Watanzania tunaendelea na porojo zetu.
Nchi kama
vile Uganda, leo imeweza kujiweka katika nafasi nzuri mno katika soka, wakati
majirani zao Tanzania hawana jipya. Leo hii Taifa Stars, kuwafunga Uganda ndani
au nje ya nchi ni kazi kubwa.
Naweza
kulaumu kwa namna moja ama nyingine, ila kwa kiasi Fulani viongozi wetu wa
soka, hususan wanaoongoza klabu zetu Tanzania kutokuwa na jipya katika mipango
yao.
Leo hii
usajili wa klabu ya Simba, unafanywa na Katibu au Mwenyekiti wa Usajili, ambaye
hajui chochote kinachohusu mambo ya ufundi. Hata kama akijua, sidhani kama
makocha wanashirikishwa.
Hali hii
ni mbaya mno. Na hakika siwezi kuvumilia, maana kinachofanywa sasa ni porojo
zisizokuwa na mashiko. Ndio maana nasema tupige domo letu kadri tuwezavyo,
tukichoka tucheze soka.
Nasema
hivi huku nikiumizwa mno kinachofanywa viongozi hawa wa soka, maana hata
usajili wao ni porojo tu. Hata kama mchezaji husika akiwa na hana uwezo
uwanjani, ila kwa timu za Simba na Yanga atakuzwa.
Atakuzwa
kwa magazeti. Ataandikiwa vichwa vya habari vinavyozalisha sifa zisizokuwa na
tija. Hii si njia nzuri kwa ajili ya kukuza na kuendeleza soka letu hapa
nchini.
Tufanye
kazi kwa kuangalia namna gani Tanzania inaweza kusonga mbele na sio kuweka
mzaha. Timu kama Simba iliyoanzishwa mwaka 1936, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya
Yanga kuasisiwa, imekosa jipya.
Leo hii
wanaiangalia timu ya Azam kwa mzaha. Wengine wanafika mbali kwa kusema Azam
haiwezi kufanana na Simba kwasababu inamilikiwa na mfanyabiashara mmoja wakati
wao ni timu ya wanachama.
Huu ni
uongo uliotukuka. Hata kama ni kweli, lakini bado klabu hizi zinaongozwa na
binadamu. Simba ipo chini ya Ismail Aden Rage, wakati Yanga ipo chini ya
mfanyabiashara Yusuph Manji.
Hawa nao
wanaweza kuziletea mafanikio klabu zao. Watimize wajibu wao. Lakini kuendelea
kukalia mtaji mkubwa wa wanachama waliozagaa kila mahali ni udhaifu mkubwa mno.
Angalia,
leo hii Simba na Yanga wameona uzandiki na uongo ndio mtaji wa kuonekana wao ni
zaidi. Hata usajili wao unagubikwa na utata. Anahitaji kigogo mmoja kufanya
usajili.
Huyo ana
uwezo wa kubadilisha matokeo au kuwataka wachezaji wagomee kama kuna jambo
hajafurahia. Hili mara nyingi linasemwa. Utasikia Fulani ametumwa ahujumu.
Hii
inaweza kuwa kweli au uongo. Kama amesajiliwa na kigogo mmoja na anamtegemea
kuhusu mshahara wake, kukataa jambo lolote analoweza kuambiwa ni ngumu.
Haya
yanatokea na yataendelea kutokea siku zote. Lakini kama timu hizi zitaacha
porojo na kuamua kufanya kazi kwa kutetea maslahi ya soka letu Tanzania, hakika
nchi itapiga hatua.
Huu ndio
ukweli wa mambo. Lakini tukisema tuendelee kupiga porojo zisizokuwa na faida
yoyote tuendelee kusubiri hasara. Ndio maana nasema tuendelee kupiga domo,
tukichoka tucheze soka.
Ndugu
zetu Wakenya ambao miaka kadhaa tulikuwa tunawafunza soka, leo hii nao
wamezinduka. Soka lao linafanya vema mno. Wanafanya juhudi kubwa kuliendeleza.
Ndio
maana hata wachezaji wao wanaonekana katika Mataifa makubwa, akiwamo Victor
Wanyama aliyesajiliwa katika klabu ya Southampton ya Uingereza, akitokea
Celtic.
Katika
vitu vingi tunavyoshiriki na Wakenya wanatuacha mbali. Hata huu mchezo wa
riadha ndio kabisa. Hii ni kwasababu sisi tunajua porojo na wenzetu wanajua
kucheza pamoja na kuweka mipango.
Hakika
siwezi kuvumilia, maana hatuna jipya tunalofanya kila siku zaidi ya hadithi ya
sungura na fisi. Nalisema hili bila kuangalia matokeo ya Mkutano Mkuu wa Simba
uliotarajiwa kufanyika Jumamosi iliyopita jijini Dar es Salaam.
Tusipokuwa
makini, kila mwaka tutapiga soga na kulidumaza soka letu na michezo kwa ujumla
maana hakuna jipya. Hali hii ni mbaya mno na lazima tujuwe ugonjwa wetu kabla
ya kutafuta dawa ya kututibu.
+255 712 053949
No comments:
Post a Comment