https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Saturday, July 06, 2013

Dayna Nyange: Anayeamini ataendelea kung'aa katika soko la muziki wa kizazi kipya



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SOKO la muziki wa kizazi kipya nchini linazidi kushika kasi, huku wasanii wengi wakizidi kujitokeza kwa ajili ya kufanya sanaa hiyo kwa lengo la kujikimu kimaisha.
Mr Blue akiwa kwenye picha na mwanadada Dayna Nyange
Kila mtu anayejiingiza kwenye sanaa hiyo anajitahidi kufanya kazi nzuri, ili kumuweka juu japo kuwa sanaa hiyo ya muziki wa kizazi kipya, maarufu kama Bongo Fleva, inaelemea kwa wanaume.



Dayna Nyange akiuza sura kama unavyomuona hapa.
Mabinti wamekuwa wakikumbwa na changamoto nyingi, japo wapo wachache wanaoendelea kufanya vizuri na kushindana na wanaume wanaotesa katika muziki huo.



Wasanii wa kike wanaojitahidi kulinda majina yao ni Lady Jay De, Mwasiti, Recho, Linah, Maunda Zoro na mwanadada Mwanaisha Said, maarufu kama Dayna Nyange.
Dayna Nyange anatambulika kama Mkali wao, anasaka mafanikio katika muziki kwa uchungu baada ya kuvumilia msoto mwingi, uliopo katika tasnia hiyo ya muziki wa kizazi kipya.

Kwa miaka kadhaa sasa, Dayna amekuwa akiingia kwenye tuzo za Kili, japo anashindwa kufanya vizuri kutokana na changamoto mbalimbali katika soko lao.

Mwanadada huyo alipozungumza jijini Dar es Salaam, anasema kuwa sanaa ni kazi anayoipenda kwa dhati, hivyo anaendelea kufanya bidii kujiweka kileleni.

Anasema japo kuwa anakabiliwa na changamoto kadhaa, ila haoni sababu ya kumfanya achoke kufanya kazi nzuri, kwa ajili ya kuburudisha mashabiki wake katika tasnia hiyo.

“Bado nipo imara kuhakikisha nafanya kazi nzuri, kwa ajili ya kuonyesha makali yangu katika tasnia ya muziki huu, ambao kwa kiasi kikubwa ndio ajira yangu.

“Tangu niachie wimbo wangu ‘Leo’, maendeleo ni mazuri kwasababu wadau wameupokea vizuri hivyo kupata moyo kuwa nitafika mbali zaidi katika tasnia ya muziki wa Bongo Fleva,” alisema.

Dayna anasema kuwa wimbo huo ameimba na msanii Mr Blue, mwimbaji aliyewahi kufanya vyema katika muziki huo, huku wimbo wake wa ‘Mapozi’ ukiendelea kukumbukwa na wengi.

Anasema wimbo huo umeimbwa kwa hisia kubwa, huku ukipokelewa kwa shangwe na mashabiki wake kwasababu ya kumuunga mkono.

Dayna Nyange anasema anachofanya kwa sasa ni kuweka mipango, na uthubutu wa kufanya kazi za maana katika hali ya kuonyesha makali yake katika soko la muziki wa kizazi kipya.

Dayna anasema kwamba albamu yake ipo katika hatua za mwisho, ikiwa na nyimbo mbalimbali, ukiwamo ule wa ‘Mafungu ya Nyanya’, ‘Fimbo ya Mapenzi’, ‘Nivute Kwako’ pamoja na Leo.
  
Wimbo wake wa Nivute Kwako, ameimba sambamba na Barnabas, nyota wa Tanzania House of Talents (THT) na kuuweka juu zaidi akiamini Barnaba ni mkali.

Dayna anasema kuwika kisanaa ni kutokana na kipaji chake imara, na mwenye malengo makubwa ya kuhakikisha kuwa anafanya vizuri.

“Kila mtu alikuwa akiniambia kwamba mwonekano wangu ni wa kisanii, hivyo niingie humo kwa ajili ya maisha yangu, jambo ambalo limeanza kutimia.

“Mwanzo nilisita kidogo, ila baada ya kufikiria kwa muda nikaona naweza hivyo nikafanya maamuzi sahihi, na kuanza kufanya sanaa kwa malengo,” alisema.
  
Mafanikio yake yamesabishwa na watu wengi, akiwamo Marlaw, aliyeimba naye katika wimbo wa Mafungu ya Nyanya, wakati huo ni msanii mchanga.

Yeye na mkali huyo wa Bembeleza walikutana mkoani Morogoro, hatimae kurekodi wimbo huo katika Studio za MJ Records.

Anamshukuru msanii huyo kwa kukubali kuimba naye, katika wimbo uliofanya vizuri katika ulimwengu wa muziki wa Bongo hapa nchini.

Maisha yake katika sanaa yamekuwa ya kawaida, sio ya mizunguko kama wanavyofanya wengineo.

“Uwezo wangu ni mkubwa katika sanaa, ndio maana kwa miaka michache nimeweza kufanya vizuri.

“Najua uwezo wangu huo ndio ulioniweka juu katika Bongo Fleva, kitu kinachonifariji ipo siku mambo yangu yatakuwa mazuri,” alisema.

Anasema lengo lake ni kuwa msanii wa Kimataifa, kwa juhudi zake na kuhakikisha mambo yake yanakuwa mazuri, akitegemea pia ushirikiano kutoka kwa wadau wa muziki pamoja na mashabiki wake.

Atahakikisha anatunga nyimbo nzuri, akifanya sanaa ya kweli, ili uwezo wake uwe juu katika sanaa ya Bongo Fleva.

Msanii huyo anayevutiwa na mwanadada Stara Thomas, anasema kwa sasa anaangalia mbele ili afike malengo yake, na kuwa msanii mwenye mafanikio katika tasnia hiyo.

Dayna ni miongoni mwa wasanii nyota kwa sasa, huku anapokuwa jukwaani mashabiki hupata burudani kubwa kwa umahiri wake wa kuimba na kumilili jukwaa.

Anachofanya ni kuweka mkazo katika utendaji wake wa kazi, ingawa anaamini kuwa ushindani umeshika hatamu na kila mtu anataka kuwa na mafanikio kimuziki.

Makali ya Dayna mbali na kuimba, pia anajulikana kwa jinsi anavyojipanga katika ufanyaji wa shoo zake nyingi, jambo ambalo limewafanya mashabiki wapende na kuthamini kazi zake.


No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...