https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, July 08, 2013

SIWEZI KUVUMILIA: Mkutano Mkuu wa Simba usiendeleze porojo



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UONGOZI wa klabu ya Simba, umetangaza siku ya Mkutano Mkuu kwa ajili ya kukutana na wanachama wote halali na kujadili mustakabali wao na kwa maendeleo yao pia.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
Mkutano huo umepangwa kufanyika Julai 20, kama ulivyotangazwa na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itangale, Mzee Kinesi, huku ukitarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, jijini Dar es Salaam.

Uamuzi huo umefikiwa na Kamati ya Utendaji iliyoketi katika siku za hivi karibuni, ambapo pia sio mgeni maana upo kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Klabu hiyo ya Simba.

Sio vibaya, huku nikiutakia kila la kheri mkutano huo kwa ajili ya kuwakutanisha wana Simba na kuangalia walipotoka na wanapokwenda sasa, ukizingatia kuwa timu imebaki jina tu.

Simba haina chochote cha kujivunia. Japo ukilisema hili, wapo wanaokuja juu wakisema klabu yao hiyo yenye hadhi inazalilishwa bila sababu za msingi, licha ya ukongwe wake.

Kwa klabu kama Simba, iliyoasisiwa mwaka 1936, ukiwa ni mwaka mmoja tu tangu mahasimu wao Yanga ilipoanzishwa, hainiingii akilini kama haina chochote cha haja.

Kila mwaka imekuwa ikifanyia kazi majungu na vurugu zinazozuka kila siku chache, huku mfumo huo ukizidi kuwa mchungu kwa maendeleo yaa klabu hiyo.

Wapo wanaojivunia kuwa na jingo lao lililokuwa katikati ya jiji, ingawa hao hao wanashindwa kuelewa kwanini jingo hilo halitumiki kwa manufaa na kubaki kama pambo tu.

Ndugu yangui Ismail Aden Rage wakati anaingia madarakani kama mwenyekiti wa Simba, alitangaza sera yake kuwa timu hiyo itakuwa na mafanikio katika kipindi kifupi tu.

Alitoa siku 90 kuwa kila mwanachama wa Simba na shabiki kwa ujumla atajivunia mafanikio. Siku zinazidi kusonga mbele na hakuna chochote cha maana zaidi ya mazungumzo ya kisiasa.

Mafanikio makubwa yaliyopatikana ni kulipiga rangi jingo lao la Msimba,. Tena katika baadhi ya maeneo. Kila mtu anaweza kufanya hivyo. Nikisema haya, wachache hawatanielewa.

Hao hao watasema nimetumwa na Yanga ili niwakosoe, wakati hatua hiyo inakuja kwa ajili ya kuwekana sawa. Hakika siwezi kuvumilia. Hiyo ni kwasabahu sioni cha kujivunia.

Najionea porojo zinazozuka kila siku ya Mungu, kama seheemu ya kuwatuliza wana Simba. Baada ya wanachama wapatao 700 kutoka tawi la Mpira Pesa wakiungana na wenzao kuhitaji mkutano wa dharura, Rage alitoa maneno ya kejeli kwa kusema kuwa kikao chao kilikuwa cha mipango ya harusi.

Hili liliwauma sana na hatimae kulimaliza kiutu uzima kwa kutembelewa
na wanachama wengine na wafadhili wao, akiwamo Rahma Al Kharous, ama Malkia wa Nyuki kama wanavyomuita.

Lakini tulishuhudia matatizo zaidi na zaidi. Ubingwa ulitoka katika mikono yao sambamba na kupigwa bao 3-1 na mtani wake wa jadi, Yanga na kuwapa sononeko la aina yake.

Kufungwa na Yanga si jambo la ajabu maana ni matokeo ya kawaida katika mpira wa miguu, ila ahadi, mazungumzo yataendelea kushika kasi kila wakati?

Yani baadaa ya kurushiana maneno, uongozi unakaa na wanachama wao kwa ajili ya kupeana moyo tu. Hii si njia nzuri kwa mafanikio ya klabu hiz kongwe.

Watu wanahitaji maendeleo. Timu ziwe na miradi ya kimaendeleo sambamba na kujenga viwanja vyao. Hatua hii imefikiwa na Azam tu, timu isiyokuwa na muda mrefu tangu kuanzishwa kwake.

Leo hii uwanja wao wa Chamazi unatumika katika mechi mbalimbali za ligi ya Tanzania Bara. Hongera viongozi wa Azam japo baadhi yao wanatakaa tusiiwekee mfano timu hii kwasababu inamilikiwa na tu mmoja na Simba na Yanga zinamilikiwa na wanachama.

Kauli hizi hazina mashiko na ni sumu kwa Yanga na Simba. Hii ni kwasababu timu kama Simba ina utajiri mkubwa wa wanachama wenye nazo na wasio nazo.

Na ndio maana mechi zao zinakuwa na msisimko wa aina yake, hivyo ifikie wakati hata hii mikutano ya Simba, ukiwapo huo wa Julai 20 uwe na manufaa kwa kuangalia mustakabali wao, mikakati yao na mipango ya kmaendeleo na sio kukaa kujadili porojo tu.
Tukutane wiki ijayo.
0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...