Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
MABINGWA wa Tanzania
Bara, Yanga, leo inaingia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kuvaana na timu ya mkoa
huo, Rhino Rangers, katika mchezo wa kirafiki, wenye lengo la kuwapatia
burudani ya soka mashabiki wao.
Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto.
Mchezo huo unafanyika
siku chache baada ya kutembelea mikoa ya Mwanza na Shinyanga, ambapo pia
waliweza kucheza mechi kadhaa za kirafiki kwa ajili ya kujiandaa na ligi ya
Tanzania Bara inayotarakiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 24 mwaka huu.
Akizungumza jana kwa
njia ya simu, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema kuwa mchezo huo
utakuwa mwangaza kwa upande wa benchi la ufundi linaloendelea kuinoa timu yao.
Alisema mechi yao ya
kirafiki inafanyika huku ikiwa na lengo kubwa la kuwapelekea burudani ya mpira
wadau na mashabiki wa soka mkoani Tabora sambamba na ubingwa wao wa Bara.
“Tuliamua kufanya
ziara katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora kwa ajili ya kujiandaa na
ligi ya Tanzania Bara ambapo sisi ndio bingwa mtetezi baada ya kumpoka mtani
wetu wa jadi, Simba.
“Mechi ya kesho
(leo), itakuwa ya mwisho maana tutarudi jijini Dar es Salaam kuendelea na
ratiba nyingine kwa ajili ya kuiweka timu yetu katika mfumo wa ushindani kabla
ya kuanza kwa ligi,” alisema.
Yanga inatumia ziara
hiyo mikoani kama kushukuru kwa kuungwa mkono, sanjari na kuwaonyesha ubingwa
waliotwaa katika msimu wa 2012/2013, ambapo sasa maandalizi yamepamba moto
kuanza tena kwa ligi hiyo Agosti 24 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment