Na Kambi Mbwana, Handeni
KUAMINI ni tendo la hiyari. Ila ni wazi kuwa mwendo huu wa
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), juu ya siasa za Tanzania inajiweka
kubaya.
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe
Hili ukilisema wapo watakaobisha. Watavaa vibwaya
kuporomosha matusi kadri ya uwezo wao. Hao ni wale wasiopenda kuambiwa ukweli.
Wakiambiwa wanachukia.
Hata hivyo, ukweli siku zite unauma lakini unasaidia
kumuweka mtu huru na lazima tujuwe kuwa kuamini ni tendo la hiyari. Leo hii
ambapo baadhi yao wanaamini Chadema ndio kila kitu, ukiwaambia juu ya njia
mbaya wanayopita ni ngumu kukuelewa.
Ni wazi Chadema kwa sasa ndio Chama Cha upinzani katika
siasa za Tanzania Bara. Nasema Tanzania Bara kwakuwa chama hicho kinachoongozwa
na mwenyekiti wake Freeman Mbowe, upande wa pili wa Muungano, yani Zanzibar
hawana chao.
Kule hakuna anayeiamini Chadema. Ingawa Wazanzibar wengi
hawaiamini Chadema kwa sababu za kidini, ila hata mwenendo wao wenyewe,
kuangalia sana Kanda ya Kaskazini kunasababisha kuibua maswali kama wengine
wanawajitaji.
Katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Chambani, uliofanyika
mjini Zanzibar ambapo Chama Cha Wananchi CUF kiliibuka mshindi kwa mgombea wao
kinyang’anyiro hicho cha Ubunge, Chadema waliambulia kura 11 tu.
Katika hali ya kushangaza zaidi, chama kipya ambacho hakina
hata mwaka mmoja, yani ADC, chenyewe kilipata kura 112, ikiwa ni ishara kuwa
katika visiwa hivyo Chadema hawana chao.
Katika mchanganuo wa kura hizo katika jimbo la Chambani,
Chama Cha Mapinduzi CCM wenyewe walipata kura 202, wakati CUF wao 2708 na
kunyakua jimbo hilo.
Sio Zanzibar tu, ila katika sehemu nyingi za Tanzania Bara,
pia Chadema haijulikani na haina heshima. Hii ni kwasababu sera na mpangilio
wao haueleweki.
Wanachoweza wao ni kubuni matamko yasiyokuwa na mashiko kwa
Watanzania wote, ukiacha wale waliokuwa katika Mkoa wa Kilimanjaro, Arusha,
Mbeya Mjini na baadhi ya maeneo wanapokubalika.
Wajuzi wa mambo ya siasa wanajua kuwa ili chama kifanikiwe
kushika dola, walau kinastahili kuungwa mkono na watu wengi. Chama
kinachojulikana Tanga tu na kuheshimiwa, kamwe haiwezi kuwa njia ya kuwapatia
Dola.
Wakati haya yanaendelea kutokea, Chadema wanajikuta wakiubua
maswali yasiyokuwa na majibu. Viongozi wao wa chama na serikali mtazamo wao
unasua utata.
Kwa mfano, mara baada ya kutokea mlipuko wa bomu
uliosababisha vifo vya watu watatu katika Mkutano wa Kampeni za udiwani
uliofanyika jijini Arusha, Mbowe kama Mwenyekiti alitangaza kuwazuia wabunge
wake kuingia bungeni.
Lengo la Mbowe lilikuwa ni kuwataka wabunge hao washiriki
mazishi ya wafuasi wao waliokufa kwa mlipuko wa bomu. Mazishi ambayao Chadema
walijua kuwa walitakiwa wasiandamane au kuaga kwa makundi kwasababu za
kiusalama.
Kwakuwa wanajua mtaji wao ni propaganda chafu dhidi ya
wananchi na serikali yao iliyopo madarakani, Chadema waligoma. Wakaamua kufanya
wanavyotaka wao.
Hii ilisababisha kuzua mgogoro baina yao ni Jeshi la Polisi.
Jeshi ambalo kila siku ya Mungu Chadema wamekuwa wakitoa lawama, wakiwadhihaki
na kuwatusi pia.
Mara kadhaa tunasikia Jeshi la Polisi likitwa PoliCCM.
Maneno mengi dhidi ya walinzi hawa wa raia na mali zao yanatoka katika vinywa
vya watu wanaojipambanua kuwa wanahitaji kuwaongoza Watanzania.
Huu sio mpango mzuri. Ili Watanzania waendelee kuwa na
heshima na vyama vya siasa, ni wazi Chadema kama Chama Kikuu cha upinzani
Tanzania Bara, lazima kijisahihishe.
Kabla ya kuzungumza jambo, lazima wakae na kufanyika
tathimini. Huu ndio ukweli wa mambo.
Kinyume cha hapo Chadema wataendelea kuwagawa wananchi, huku
wale wanaowaunga mkono pia wakitafakari uwapo wao. Kwa mfano, Chadema kwa
kupitia kikao cha Kamati Kuu kimetangaza kuwafundisha vijana wao namna ya
kujilinda.
Hii ndio kusema kuwa Chadema wameona jeshi halali la
Tanzania limeshindwa kuwalinda. Ingawa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania imekataza vikundi vya namna hiyo, kikiwamo hiki cha Red Brigade
kilichotangazwa na Chadema.
Wataalamu wa mambo wanahisi kuunda vikundi vya aina hii ni
kuzalisha chuki na machafuko. Kwa Chadema ambao wamekuwa wakilalamikia jeshi la
Polisi kesho vijana wao hawatafanya fujo?
Leo hii wakiwa wakomavu na mafunzo hayo hawatawarushia
mabomu askari wetu? Haya ni maswali yanayotakiwa yajibiwe na kila Mtanzania juu
ya siasa za Tanzania, hususan Chadema.
Chama ambacho dhamira yao inaweza kuyeyuka kama watashindwa
kujiweka sawa. Mwendo wao si mzuri. Kauli zao nyingi inaonyesha inatoka bila
kufanyiwa uchunguzi.
Kwa mfano, Chadema wao waliweza kususia vikao halali vya
Bunge kwa kisingizio cha mazishi ya wafuasi wao. Mbaya zaidi, waligomea katika
Bunge la Bajeti.
Bunge ambalo tangu lilipomalizika, tayari kumekuwa na
matokeo magumu ya kupandishwa kwa kodi katika baadhi ya huduma, zikiwapo za
simu za mikononi.
Leo hii Mtanzania ambaye hata kula yake haijulikani, bado
atapaswa kulipia kiasi cha Shilingi 1,000 kwa namba yake (simcard). Hii ni kodi
tofauti na gharama nyingine za muda wa maongezi ambazo zimepanda mara dufu.
Ingawa wabunge wa CCM wapo wengi bungeni, wakifikia 245 tofauti
na wale wa upinzani hususan Chadema, ila kuwapo kwao kungesaidia kuibua hoja
katika mrejesho wa hutuba ya Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa na wataalamu
wake.
Kitendo cha uwapo wao, huenda kingezindua zile hoja zenye
mashiko na Watanzania wote. Lakini waligoma kuingia kwasababu ya Arusha,
wabunge wao wote wakiwapo huko, bila kujua kuwa Tanzania ina mikoa mingine
inayohitaji uwapo wa wapinzani.
Bado kuna mikoa kama vile Mwanza, Geita, Morogoro, Tanga,
Ruvuma, Pwani na mingineyo, hivyo si vizuri pia kwa chama hiki kuangalia zaidi
Kanda ya Kaskazini.
Aidha tunahitaji hoja zaidi badala ya kupayuka maana huko
kunaoanyesha mapungufu ya hadharani kabisa. Kwa mfano, katika makala yangu ya
Mbunge wa Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chadema, Joseph Mbilinyi Sugu, nilipinga
kumuita Mpumbavu Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Wapo waliokosoa na waliosifia pia. Katika makala ile,
nilijaribu kusisitiza wanasiasa wetu, viongozi wetu kupenda kuweka hoja badala
ya mihemko isiyokuwa na tija.
Huu ndio ukweli. Hivyo hata hili suala la Red Brigade la
Chadema linaweza kuwa baya zaidi kama litatumiwa tofauti. Chadema lazima wajuwe
wana kila sababu ya kuilinda amani ya nchi yetu.
Sioo Chadema tu, ila vyama vyote vya siasa vinastahili
kupigania amani maana ndio msingi wa maendeleo. Leo hii kama kila mtu ataweza
kuunda vikosi anavyojua mwenyewe tutasababisha mwingiliano na machafuko
yasiyokuwa na mpango.
Shughuli za ulinzi wa Taifa letu tushiriki kwa pamoja, ila
zaidi jeshi la Polisi lina imudu zaidi kazi hiyo. Muhimu ni kuwapa moyo na
kuwapa ushirikiano pia.
Hakuna haja ya mwanasiasa kutoa maneno ya kejeli kwasababu
Dola ipo chini ya CCM. Tusipokuwa makini na kufanya siasa za kuvumiliana, hata
kesho Chadema wakiingia Ikulu au ama CUF basi machafuko, lawama za mtindo huo
zitashika kasi.
Angalia nchini Misri. Mwaka jana wananchi waliweza
kuandamana kushinikiza rais wao Hosni Mubarak ajiuzulu. Walifanikiwa. Mubarak
alitoka na uchaguzi huru wa kwanza kufanyika.
Lakini wakati watu wakiwa hawajui kinachotokea, wananchi hao
hao tena wanaingia barabarani kumtaka rais wao Mohamed Morsi ang’oke kwa madai
kuwa ameshindwa kuliongoza Taifa hilo.
Pia wakafanikiwa, hasa baada ya jeshi kumsaliti na
kumuengua. Hii ni ishara kuwa hata Tanzania hayo yanaweza kutokea. Kama
wananchi watafundishwa kufanya vurugu, maandamano, matusi na kejeli dhidi ya
serikali au jeshi, basi hata kama Chadema wakiingia Ikulu, mtindo huo
utaendelea kushika kasi.
Ni vyema tukajifunza katika hili. Tanzania tunakabiriwa na
changamoto nyingi has azan ugumu wa maisha. Ni vyema basi tukatumia muda mwingi
kuwaza namna ya kujiletea maendeleo na sio kupanga namna ya kulisumbua Taifa
kwa namna yoyote ile.
Ni wakati wa wanasiasa wetu kutumia busara na siasa za
uvumilivu ili iwe nafasi ya kujiletea maendeleo. Vyama vya upinzani kama kweli
vinahitaji kuwakomboa Watanzania kama wenyewe wanavyosema, wasimamie kwanza
katika suala zima la amani yetu inayoelekea ukingoni, ukizingatia kuwa kaatika
siku za hivi karibuni, kumekuwa kukitokea matukio ya kuogofya, hasa ya utekwaji
na uteswaji.
+255 712 053949
No comments:
Post a Comment