Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KATIKA mfululizo wa makala zangu, niliwahi kuelezea kasumba
wanazokutana nazo wasemaji wa klabu za Tanzania, hasa za Simba na Yanga.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
Msemaji wa Simba alikuwa ni Ezekiel Kamwaga na yule wa Yanga
akiwa ni Louis Sendeu, ambao wote wameondoka kwenye timu hizo, tena kwa
matatizo makubwa.
Bila kuficha, Sendeu alinipigia simu akinilaumu sana, akisema
maneno niliyosema katika makala yangu, japo yalikuwa ni ukweli, ila yataeleweka
yametoka kwenye vinywa vyao, hivyo kupigia kelele kitumbua chake kuingizwa
mchanga.
Sikumshangaa Sendeu, maana lazima atetee kibarua chake.
Wakati Sendeu anailalamikia makala yangu, Kamwaga aliyeacha kazi Simba, kwa madai kuwa mkataba wake
umekwisha, yeye aliisoma ile makala na kunipigia simu pia, tukajadili hili na
lile, ukizingatia kuwa ilikuwa ni kuwatetea wao.
Ninachokumbuka ni kuwa Simba, ikiwa chini ya Ismail Aden
Rage, aliilalamikia ile makala yangu, akimlaumu pia Kamwaga kuwa huenda maaandishi
yangu yalitoka kwake.
Maudhui ya makala yangu, yalitokana na namna wasemaji
wanavyokuwa vitumishi na wasioheshimiwa. Wanaopewa kazi nyingi bila mapumziko.
Hata hivyo haitoshi, mshahara wao ni wa kubabaisha.
Kama Sendeu aliniona mimi mjinga, basi leo akiisoma makala
hii atakumbuka kitu, maana aliachwa kama mwana mkiwa.
Nasema hivi baada ya kuona kuwa kinachoendelea ndani ya Simba
kwa sasa, hasa kutangaza kuwa kiwango cha Juma Kaseja, kipa wao kimeshuka ni
jambo la kawaida mno.
Kwa viongozi wa Simba, chini ya Rage na jopo lake kauli kama
hizo ni rahisi kutolewa na kumuacha kwa mizengwe pia. Mtambuka msemaji wa
zamani wa Simba, Criford Ndimbo alivyozalilishwa kwa maneno ya kejeli.
Mtambuka wanachama wa Simba kutokea tawi la Mpira Pesa
walivyotukanwa. Kwa wale wasiokuwa na kumbukumbu, Rage aliwaambia Mpira Pesa
kuwa kikao chao ni cha harusi na maneno mengine ya dharau.
Hii ni kawaida, ndio maana siwezi Kuvumilia. Kumuacha
mchezaji katika timu yoyote ni jambo la kawaida mno. Wengi walisajiliwa kwa
gharama kubwa na baadaye kutemwa na kuangalia maisha mengine.
Wapo pia ambao baada ya kugundua mwelekeo mbaya, waligeuka na
kuangalia maisha mengine, ukizingatia kuwa hawawezi kucheza Simba au Yanga hadi
mwisho wa maisha yao.
Wale walioachwa na umri hupumzika kwa ridhaa yao au kulazimishwa
kuachwa katika vikosi vyao, ila si kwa dharau. Yoyote anayemuita Kaseja leo
kuwa kiwango chake kimeshuka hakika anashangaza umati.
Kaseja bado yupo kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa
Stars, chini ya kocha wake Kim Poulsen na kusimama langoni kila mechi. Mchezaji
aliyeshuka kiwango hawezi kung’ang’aniwa kwenye timu ya Taifa.
Kaseja hana kiwango wakati katika msimu mzima wa ligi yeye
amesimama langoni kwa mechi nyingi zaidi? Hii inashangaza Dunia. Bila kuacha
unazi juu ya kipa huyu, ila ni dhahiri viongozi wa Simba wameamua kumdhalilisha
kwa faida zao.
Kuna jambo moja tu Simba wanaweza kufanya na kikawaongezea
pia mapato ya kusajili wachezaji wengine, kwa kuandaa hata bonanza la mashabiki
wa Simba, wenye mapenzi na Kaseja kwa ajili ya kumuaga na wakavuna shilingi.
Kila mtu atapenda kumuaga Kaseja kama kweli anaachwa na timu
yake, maana amecheza Simba kwa mapenzi makubwa na kuisaidia kwa kila aina. Ni
mwendawazimu tu anayeweza kumdhalilisha Kaseja Tanzania.
Tanzania nzima sasa imegawanyika juu ya Kaseja. Kila mtu
anasema lake, anaelemea zaidi kumtetea maana kinachofanywa na Simba
kinachekesha. Pamoja na yote hayo, ukweli unabaki pale pale kuwa Kwa Simba hii haiwezi
kumheshimu Kaseja.
Tangu lini asiyekuwa na nidhamu akamheshimu mtu mwingine?
Wafanye wanavyotaka, ila ubabaishaji huu haujaanza leo japo ndani ya uongozi wa
Rage, Mbunge wa Taboro Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
umeongezeka mara dufu, hivyo wadau wa soka, wapenzi na wanachama wa Simba
wanapaswa kumuangalia mara mbilimbili.
Mungu ibariki Tanzania.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment