SIWEZI KUVUMILIA
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara.
Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
WAPO watu ambao wamekaa, malalamiko yao wameanza kuyapeleka
kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, eti
amekurupuka katika kuchukua uamuzi wa kuifuta Katiba ya mwaka 2012 ya
Shirikisho la Soka nchini (TFF).
Rais wa TFF, Leodgar Tenga, kushoto akisisitiza jambo.
Mukangara aliwalazimisha TFF kutumia Katiba ya mwaka 2006
ndio halali, ukiacha hi iamb ayo wanaitumia sasa kupitishwa bila kufuata
taratibu, hivyo kuingiza mgogoro mzito, jambo ambalo suluhu yake ni kuifuta
katiba hiyo.
Mengi yanasemwa, tena kila mtu anaegemea upande wake. Kwa
mfano, mtu ambaye anaona kuwa TFF wanajiendesha tofuati, huyo ni mwepesi
kuwalaumu wao na kuwasifia viongozi wa serikali, huku wanaovutiwa na utendaji
wa TFF nao kuwaponda serikali.
Katika suala hilo, ni rahisi kusikia, Serikali haiwezi
kuingilia mambo ya soka. Jamani, kama serikali hairuhusiwi kuingilia mambo ya
soka, kwanini Bungeni mawaziri wa michezo mara kwa mara wanalaumiwa kwa matokeo
mabaya Tanzania?
Pamoja na hayo yote, hakika siwezi kuvumilia kuona wapo watu
wanaoanza kuitolea macho serikali, hasa kwa uamuzi wao wa kuifuta Katiba ya
TFF. Kiukweli, hata kama ningekuwa mimi, uamuzi huo ningeuchukua kwa kuepusha
migogoro.
Najua kuwa kuipinga Katiba ya mwaka 2012 na kuitaka ile ya
mwaka 2006 ina tabu, hasa kwa kuona wanachama wake, vyama vya soka vya mikoa na
klabu zimefanya uchaguzi, lakini hali hii ya kukanyaga Katiba zetu ikindelea
hakuna maendeleo.
Siku zote mkubwa akivukwa na nguo huchutama. Kuilaumu
serikali sio kitendo cha kiungwana, hasa tukitambua kuwa Tanzania inajiendesha
kwa kufuata sheria. Hata Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Leodgar
Tenga, anajua serikali ndio kila kitu.
Hivyo ili isiingilie katika mambo yetu, lazima tuwe wakweli,
tujiendeshe vizuri bila kuweka mizengwe ya hapa pale, ukizingatia kuwa huo ndio
utawala bora. Watu wengine wanashindwa kuelewa kuwa serikali imetengua Katiba
kwakuwa imepatikana vibaya.
Utaratibu si mzuri, ukiwamo ule wa kutuma waraka, hali ya
kuwa uwezekano wa kufanya kikao cha pamoja, kuipitisha au kuipinga ulikuwapo.
Kama TFF inasema haijakuwa na fedha za kuitisha Mkutano huo, hizi ni sababu
zisizokuwa na ukweli.
Ingawa kadhia hii imeibuka katika Uchaguzi wa TFF kwa kuona
wagombea wengine wanapingwa huku wachache wao wakipitishwa kienyeji, hakika
lawama, malumbano lazima yawe makubwa. Suluhisho pekee, ni kufanya kikao cha
pamoja, kati ya serikali, TFF na wadau wengine kwa ajili ya kuona jinsi hilo
linaweza kuepukwa.
Ndio FIFA wanaweza kuifungia TFF, hivyo kuharibu mfumo mzima
wa soka letu, lakini kama hatuna mipango, sisi ni wababaishaji, hakuna njia ya
mkato.
Waziri Mukangara, aliishauri TFF itume barua FIFA kuwa wasije Tanzania,
kama ilivyotangazwa kuwa watu hao wapo kwenye mipango ya kuja kuangalia mgogoro
wa kanuni na malalamiko kwenye uchaguzi wao.
Hii ni aibu kubwa kwa Taifa tena ikichangiwa na uwepo wa
Katiba isiyokuwa na ubora, ikipitishwa kienyeji, ikichangiwa na mipango ya
kujiendesha kwa mizengwe, hivyo hatuwezi kwenda kwa mtindo huo, bado tukasema
tunahitaji maendeleo.
Najua wapo wachezaji wenye lengo la kutaka kucheza nje ya
nchi, lakini ili twende huko, pia lazima tutambuwe makosa yetu na
kuyarekebisha. Lazima kila mtu ajuwe kuwa katika mchakato mzima wa Uchaguzi au
kupitisha Katiba hiyo ya mwaka 2012 kulikuwa na kasoro nyingi.
Ili Tanzania irudi kwenye heshima yake, kujua kuwa Taifa
linajiendesha kwa utaratibu mzuri na sheria zake, hivyo hili suala la kuigiza
TFF ni jambo zuri. Leo tukiona serikali imekurupuka, kesho haya yataendelea,
hivyo kuleta mkanganyiko wa hapa na pale.
Siku zote supu inanywewa ikiwa ya moto. Na dawa ni kujua
tatizo kwa ajili ya kurekebiha makosa yetu, kama kweli lengo ni kutaka
kutangaza soka letu, kwa mipango ya kweli na sio ubabaishaji kama huu
unaofanywa na TFF.
Hili lazima lisemwe, maana hakika nimeshindwa kuvumilia,
hasa kwa kuangalia mchakato mzima ulivyotokea mwanzo hadi mwisho. Kwanza
kitendo cha Kanuni kuchanganyana, matamko ya Rais wa TFF na Kamati zake ni
zengwe la aina yake.
Leo Tenga anasema kuwa Kamati ya Rufaa inaweza kupitia upya
vipengele vyake, wakati kesho yake mwenyekiti wa kamati hiyo anatangaza kuwa
hakuna kitu kama hicho. Hili ni tatizo la TFF na Kamati zake au serikali?
Siku zote watu wameshindwa kujua kwamba daima lisilotafunika
huwa halimezeki. TFF wameshindwa kutafuna Katiba yao, Uchaguzi wao, hivyo
kulazimisha kulimeza, yani kulimaliza
kienyeji, ni jambo la ajab u mno.
Haiwezekani, maana hata kama leo lingeisha, lakini mgogoro
mkubwa ungeendelea kuwapo, hivyo watu kufanya kazi kwa visasi, hasa kwa kuona
kuwa hakuna hujudi wala mipango kwa ajili ya soka letu, huku chanzo kikiwa
uongozi wa mizengwe.
Hili lazima lisemwe, hata kama litakuwa chungu, maana katika
kuliangalia hilo, nimegundua kuwa bado hatuwezi kupata maendeleo ya mpira wa
miguu, wakati viongozi wenyewe wameamua kufanya kazi kwa kushughulikiana,
ubabaishaji wa aina yake.
Sipingi kwa maombi ya Tenga juu ya kufanya kikao cha pamoja
na Waziri Mukangara, lakini ifikie wakati tuone hatuwezi kufanya ‘madudu’ bado
tukaona serikali haiwezi kuingilia katika michezo, hivyo tusifanye vitu
kienyeji.
Huo ndio ukweli wa mambo, kama kweli tunahitaji kuwa na
mipango ya kujiletea mafanikio katika sekta ya michezo, ukiwamo mpira wa miguu,
ambao kwa siku za karibuni umekumbwa na matatizo ya aina yake, hivyo lazimaa
mizengwe hiyo itoweke.
Hata kama kikao hicho kitafanyika, lakini majibu yake lazima
yawe ni tunu, ili siku nyingine asitokee mwingine na kukanyaga Katiba bila
mpango. Kuhusu Uchaguzi, bado tunaweza kufanya uchaguzi bila kusubiri busara za
watu kutoka FIFA.
Wao ndio nani? Ina maana Tenga, akiwa na wataalamu wengi
katika Shirikisho hilo, ameshindwa kabisa kubaini mapungufu yaliyojitokeza,
yakiwamo yale ya kuwaondosha baadhi yao kwa sababu zisizoeleweka na kuwapitisha
hata wale wanaojulikana kuwa hawakuwa na vigezo, hasa kile cha uzoefu ambacho
ndio kikubwa katika Uchaguzi huo.
Kila mtu anajua hilo, hivyo kamwe huwezi kuipenda pepo
huwezi kuogopa kufa. Maendeleo ya mpira wa miguu yatapatikana kwa kuongoza bila
kufuata nani hatakiwi ndani ya chombo husika, kama vile TFF na vyama vingine
vya mikoa.
Huo ndio ukweli wa mambo, maana hakika siwezi kuvumilia,
ingawa naomba kikao cha pamoja kati ya Waziri Mukangara, Naibu wake, Amos
Makalla, TFF na wadau wengine wenye mawazo mazuri kwa ajili ya Tanzania yenye
tija na michezo.
0712 053949
0753 806087
2 comments:
WEWE UNASEMA MAREKEBISHO YA KATIBA KWA NJIA YA WARAKA HAYAKUWA SAHIHI,LAKINI WAJUMBE WENGI WA MKUTANO MKUU WA TFF WALIONA NI SAHIHI NA KUPIGA KURA KWA NJIA HIYO,ISIPOKUWA WALE WA MKOA WA KAGERA NA WENGINE WACHACHE.SASA WEWE NA WAJUMBE WA MKUTANO MKUU WA TFF TUMSIKILIZE NANI JAMANI?
ASANTE msomaji na mfuatiliaji wa karibu wa Handeni Kwetu Blog juu ya maoni ua mtazamo wako. Ukweli ni kwamba, katika kupitisha hayo marekebisho ya Katiba kwa kupitia wakaraka kulikuwa na mushkeli. Taratibu nyingi hazikufuatwa. Hata hivyo, kwakuwa hayo yamebainika katika Uchaguzi wa TFF, ndio maana wadau wakuu wakiwamo Serikali ikaona Uchaguzi huo usitishwe kwasababu Katiba inayotumika si halali. Kikubwa ni kufuata sheria na taratibu zilizowekwa. Ni kweli,serikali haipaswi kuingilia mambo ya soka, lakini kwa bahati mbaya serikali inatambua na ndio maana tukaweka waziri au watendaji wengi wanaohusu mambo ya michezo. Leo tukisema tuchekee kufinyanga Katiba, kuna siku yataamuliwa maamuzi mengi mabaya na tutaingia kwenye mgogoro mkubwa zaidi ya huu. Nashukuru, naamini serikali na TFF watafikia muafaka kwa kuangalia lipi bora, kusuka au kunyoa? Mungu ibariki Tanzania. Endelea kuipitia blog hii ya www.handenikwetu.blogspot.com upate kupitia habari na makala za aina mbalimbali.
Post a Comment