Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KAMATI ya Sheria na Hadhi za
Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesema uwakilishi wa
ujumbe kwenye Mkutano Mkuu unaanzia kwenye chama cha mpira wa miguu cha mkoa,
kufuatiwa na chama shiriki na baadaye klabu ya Ligi Kuu.
Mwongozo huo juu ya uwakilishi wa
wajumbe kwenye Mkutano Mkuu umetolewa kutokana na maombi ya Sekretarieti ya TFF
kwa kamati hiyo iliyokutana jana (Septemba 16 mwaka huu) baada ya kubaini
baadhi ya wajumbe wanashikilia nafasi mbili kwenye vyama tofauti.
Kwa mujibu wa Ibara ya 5 ya Katiba,
kuna makundi ya aina tatu ya wanachama wanaounda TFF. Makundi hayo ni vyama vya
mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu.
Sekretarieti ya TFF imebaini kuwa
kuna baadhi ya viongozi wa kuchaguliwa wa mikoa ambao pia ni viongozi wa vyama
shiriki na klabu za Ligi Kuu, hivyo wana nafasi zaidi ya moja ya kuingia kwenye
Mkutano Mkuu.
Hivyo, kutokana na mwongozo huo
ushiriki wa wajumbe kwenye Mkutano Mkuu wa TFF utaanzia chama cha mkoa,
kufuatiwa na chama shiriki na baadaye klabu za Ligi Kuu.
Pia nafasi ambazo zinaweza
kuwakilishwa kwenye Mkutano Mkuu kama mhusika hayupo ni za Mwenyekiti
atakayewakilishwa na Makamu Mwenyekiti, na Katibu atakayewakilishwa na Katibu
Msaidizi. Nafasi za ujumbe wa Mkutano Mkuu na ile ya mwakilishi wa klabu
hazina uwakilishi kama mhusika hayupo.
No comments:
Post a Comment