Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
WATANZANIA wenye
mapenzi mema na mchezo wa ngumi lazima waheshimu mchango wa bondia Francis
Cheka. Huyu ni bondia mwenye makali ya kutosha.
Bingwa wa Dunia, Francis Cheka, pichani.
Kila anapoingia
ulingoni amekuwa akifanya vitu vya kufurahisha wadau wa ngumi kutokana na
kufanikiwa kuibuka na ushindi, hivyo kuzidi kukuza jina lake.
Baada ya kuwapiga
mabondia mbalimbali kutoka Tanzania na nchi kadhaa za Afrika, Ijumaa iliyopita,
Cheka alifanya tena maajabu kwa kumtandika Phil Williams, bondia kutoka nchini
Marekani.
Pambano hilo la
Ubingwa wa Dunia mkanda wa (WBF) na kufanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee,
Cheka alishinda kwa pointi.
Pamoja na kuheshimu
mchango wa Cheka, bado malalamiko yangu yapo kwa serikali na wadau wenye uwezo
wa kuwekeza zaidi kwenye mchezo huo.
Serikali yenye uwezo
wa kukuza na kuendeleza mchezo huo, sanjari na kutambua mchango wa Cheka na
mabondia wengine wa Tanzania.
Hii si mara yangu ya
kwanza kuandika makala inayoelezea kumuunga mkono bondia huyo mwenye maskani
yake mkoani Morogoro.
Nimeshawahi kusema
mara kadhaa, huku kilio changu kikitokana na umahiri wa bondia huyo
anayestahili kulindwa ili afike mbali zaidi.
Tunahitaji sapoti ya
Cheka ili aendeleze ubabe katika Mataifa makubwa, kama vile Marekani,
Uingereza, Ujerumani na mataifa mengine.
Hivi karibuni Cheka
alizungumzia mpango wake wa kupunguza kupanda ulingoni kwa mabondia wa
Tanzania. Alisema hivyo kwakuwa lengo lake ni kupiga hatua ya juu zaidi katika
mchezo huo wa masumbwi.
Hata hivyo, uamuzi
huu kwa Cheka unaweza kuwa na changamoto, ukizingatia kuwa bondia anaingiza
pesa anapopanda ulingoni.
Kama hivyo ndivyo, je
wadau wa ngumi wanajipanga vipi kuhakikisha kuwa mkali huyo anapata pambano ya
Kimataifa zaidi kwa manufaa yake?
Hakika siwezi
kuvumilia kuona mabondia wetu wenye makali tunashindwa kuwathamini. Hii si mara
ya kwanza. Tanzania inapenda zaidi kuvuna kabla ya kupanda.
Kwanza tupande ili
kesho tuvune. Hatuwezi kupiga hatua kama hatuna mipango. Bila shaka huu ni
wakati kuwekeza zaidi kwa mabondia wetu, akiwamo Cheka.
Ni wazi ana heshima
na nguvu za kutosha. Kwa kulijua hilo, sote tutasonga mbele. Katika mchezo wa
masumbwi, kuna changamoto nyingi.
Wakati mwingine
bondia anapanda ulingoni akiwa hajui kinachoendelea juu ya fedha. Wakati
mwingine wanapanda bila kutanguliziwa pesa zao.
Bondia anakuwa na
pambano bila kujua namna gani atalipwa fedha zake. Huu ni wakati wa kuwa makini
zaidi. Kinyume cha hapo mchezo wa masumbwi utashindwa kupiga hatua na kufifisha
ndoto za mabondia.
Licha ya kuwa na
wakali kama vile Cheka, ambaye ana uwezo wa kulitangaza Taifa, lakini nguvu zao
huenda zikaisha kama hawatawezeshwa kusonga mbele.
Nafikiri ni wakati wa
kuangalia changamoto zetu ili kesho mabondia wetu wapige hatua. Binafsi naunga
mkono juhudi za mchezo huo.
Naheshimu mno ujuzi
wa Cheka na hakika lazima wadau wote, wakiwamo viongozi wa serikali kuona namna
gani ya kuweka mipango kabambe.
Michezo ni ajira.
Michezo ina uwezo wa kuwapatia maisha bora vijana wetu, hivyo lazima tujiweke
sawa kwa ajili ya kuangalia namna ya kulifanyia kazi suala hilo.
Huu ndio ukweli wa
mambo. Kwa wale mabondia wenye makali, akiwamo Cheka, ni wakati wake wa
kuendelezwa, kusimamiwa na kushauriwa namna ya kuwa bora zaidi.
Ningefarijika siku
moja kusikia serikali imemgharamia Cheka aende japo katika nchi mbili ili
kuangalia mapambano makubwa ya Dunia, ukizingatia kuwa huo ndio mpango mzuri wa
kupanua mtandao wake kimasumbwi.
Kinyume cha hapo
nitaendelea kuona mipango butu ya viongozi na wadau wa mchezo wa masumbwi hali
inayochelewesha maendeleo ya mchezo wa ngumi hapa nchini.
Tukutane wiki ijayo.
+255 712053949
No comments:
Post a Comment