Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KIUNGO wa Simba, Jonas Mkude ameitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars
kinachojiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Gambia
itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu jijini Banjul.
Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen
amemuongeza mchezaji huyo ili kuimarisha sehemu ya kiungo. Taifa Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imeingia kambini tangu Agosti 29
mwaka huu kwenye hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Boniface Wambura, timu hiyo imefanya mazoezi leo asubuhi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu
ya Karume wakati kesho Jumatatu (Septemba 2 mwaka huu) saa 10 jioni itafanya
mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, Chama cha Mpira wa Miguu cha Ujerumani (DBU) kimetuma maombi ya
Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa wachezaji wawili wa Tanzania ili
wajiunge na klabu mbili tofauti za nchini humo.
Maombi hayo yaliyotumwa kwa Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) ni kwa ajili ya wachezaji Henry Claud Egito aliyezaliwa
Desemba 31, 1984 jijini Dar es Salaam, na Dominic Johnson aliyezaliwa Agosti
14, 1991 jijini Tanga.
Wachezaji hao wanaombewa ITC kama wachezaji wa
ridhaa. Egito anaombewa hati hiyo ili ajiunge na klabu ya FSV Lokomotive
Dresden wakati Johnson anatakiwa na klabu na TSV 1967 Schwabbruck.
Aidha, usaili wa waombaji
uteuzi kwenye uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi
ya Ligi Kuu (TPL Board) unaendelea na unatarajia kukamilika leo (Septemba 1
mwaka huu).
Kamati ya Uchaguzi ya
TFF chini ya Mwenyekiti wake Hamidu Mbwezeleni ilianza usaili juzi (Agosti 30
mwaka huu) ambapo matokeo ya usaili yanatarajiwa kutangazwa keshokutwa
(Septemba 3 mwaka huu).
Kati ya Septemba 4 na 6
mwaka huu, Kamati ya Uchaguzi kupitia Sekretarieti ya TFF itawasilisha kwenye
Kamati ya Maadili ya TFF mashauri yote ya maadili ili kujadiliwa na kutolewa
uamuzi na kamati hiyo.
Vilevile kati ya
Septemba 4 na 6 mwaka huu ni kipindi cha kukata rufani kwenye Kamati ya Rufani
ya Uchaguzi kwa masuala yasiyo ya maadili. Kwa watakaokata rufani wanatakiwa
kuambatanisha na ada ya rufani kwa Katibu Mkuu wa TFF kabla ya saa 10 kamili
jioni ya Septemba 6 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment