Na Salum Vuai, Maelezo
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema wahitimu wa
fani mbalimbali za afya wanaosomeshwa na serikali hawana budi kubaki nchini na
kuitumikia jamii yao. Dk. Shein ametoa wito huo jana baada ya kuzindua majego
mapya ya dahaklia ya wnafubzi wa kike na jengo la madarasa, katika Chuo cha
Taaluma ya Sayansi za Afya, Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,alipokuwa akitoa hutuba yake kwa
Wananchi na wanafunzi (hawapo pichani) wakati wa Sherehe za Uzinduzi wa
jengo la madarasa ya Chuo cha Taaluma za Sayansi
ya Afya, lililogharamiwa na Serikali ya Oman kwa kushirikiana na
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, huko Mbweni Mkoa wa Mjini Magharibi
Unguja jana. Kushoto ni Waziri wa Afya Juma Duni Haji na Mshauri wa Mambo
ya Afya, Wizara ya Afya ya Oman, Dr. Sayeed Sultan Bin Yarub Bin Qaatan
Al- Busaid, (kulia).
Mshauri wa Mambo ya Afya,Wizara ya Afya
ya Oman,Dr.Sayeed Sultan Bin Yarub Bin Qaatan Al- Busaid,akitoa salamu
zake wakati wa sherehe za uzinduzi wa madarasa mapya ya kusomea
katika Chuo cha Taaluma za Sayansi ya Afya,yaliyojengwa na Serikali
ya Oman,na ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.[Picha
na Ramadhan Othman,Ikulu.
Akizungumza na wanafunzi
na wananchi mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo, Dk. Shein alisema, serikali
inatumia gharama kubwa kuwasomesha wanafunzi wake, hivyo nao wanapaswa kutimiza
ihsani na utu kwa kufanya kazi nchini badala ya kukimbilia nje. Amesema kwa bahati mbaya, wapo
baadhi ya wananchi na watumishi wa umma wakiwemo wafanyakazi wa sekta ya afya
ambao husomeshwa kwa fedha nyingi za serikali lakini baada ya kumaliza masomo
yao huondoka nchini na kukwepa wajibu wao wa kuwatumikia wananchi wanyonge
waliogharamia fedha hizo
“Hili siyo jambo zuri
kwani siku zote ni vyema binadamu azingatie ihsani anayofanyiwa na wenzake”,
alisisitiza. Akitoa mfano kwa kunukuu hadithi ya Mtume Muhammad (S.A.W), Rais
Shein aliwanasihi vijana wote wanaopata fursa ya kusomeshwa na serikali, kuwa
na uzalendo na mapenzi kwa jamii yao inayowategemea kuihudumia. Alisema kwa
hadithi hiyo, alisema Mtume Muhammad (S.A.W) anautanabahisha umma juu ya ubaya
wa kuwaacha watu wanaoutegemea kwa kusema:
“Yatosha kwa mtu kupata
dhambi kwa kumtupa yule anayemtegemea” Hata hivyo, alisema kama mtu anataka
kuondoka kwenda kutafuta kazi nje ya nchi, serikali haimzuii, lakini kwanza ni
lazima alipe fedha zote zilizotumika kumsomesha, kwa mujibu wa agizo la
serikali kwa wizara zake zote. Alifahamisha kuwa, iwapo mtu atashindwa kulipa
gharama hizo, wazee au familia yake italazimika kufanya hivyo.
Akizungumzia kukamilika
kwa ujenzi wa majengo hayo pamoja na kupatikana vifaa vya kisasa, alisema hiyo
ni njia moja ya kuimarisha mazingira ya utoaji mafunzo kwa vijana wanaojiunga
na chuo hicho kwa masomo mbalimbali yanayotolewa hapo. Pamoja na kuwapongeza
vijana waliobahatika kujiunga na chuo hicho katika huduma tafauti za afya, Dk.
Shein alisema ni imani yake kuwa wanachuo wanaojiunga hapo, huchaguliwa kwa
kutimiza sifa, na kwamba nao huamua kujiunga kwa kuelewa ugumu wa kazi yenyewe
baada ya kumaliza masomo yao.
Alisema utoaji bora wa
huduma za afya, lazima utanguliwe na huruma na ubinadamu, na kwamba kazi hizo
humtaka mhudumu kuzingatia wito wa kuwahudumia wagonjwa kwa upendo pamoja na
maadili ya taaluma yenyewe. “Kwa bahati mbaya, wapo baadhi ya wafanyakazi wa
sekta ya afya ambao huweka pembeni vigezo hivyo na matokeo yake hutokea
manung’uniko kwa wagonjwa wanaohudumiwa”, alieleza Dk. Shein Alisema, mlahaka
mzuri na lugha nzuri kwa mgonjwa ni miongoni mwa mambo muhimu katika
kumuhudumia mgonjwa.
Pamoja na changamoto
mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo na chuo hicho, Dk. Shein aliwapongeza
viongozi na wafanyakazi wa hospitali za Unguja na Pemba na taasisi za afya kwa
kujitahidi kuondoa udhaifu huo kwa lengo la kuwahudumia vizuri wagonjwa
Alieleza kuwa, siku zote mgonjwa anahitaji huruma na imani kutoka kwa
anaemuhudumia wakiwemo wanafunzi wanaohitumu kwenye chuo hicho.
Aliwahakikishia wanafunzi
na watendaji wa sekta hiyo, kuwa daima serikali inatambua na kuthamini mchango
wao kwa jamii, na hivyo inajitahidi kuimarisha maslahi yao kila uwezo
unapopatikana. Aidha, alisema serikali inaendelea na sera yake ya kutoa matibabu
bure kwa wananchi, ingawa katika baadhi ya maeneo, inapokwazwa na ufinyu wa
bajeti huwataka kuchangia, lakini si nia ya serikali kuona wananchi wanapata
shida.
Pia alifahamisha kuwa,
katika kutanua wigo wa taaluma chuoni hapo, serikali imeamua kukiweka chini ya
Chuo cha Taifa Zanzibar (SUZA), pamoja na kuanza kutoa digriii ya uuguzi
kuanzia mwaka huu.
Aliishukuru serikali ya
Oman chini ya uongozi wa Sultan Qaboos Bin Said, kwa uamuzi wake wa kujenga na
kukiendeleza chuo hicho, akisema hiyo ni dalili ya mahaba makubwa kwa wananchi
wa Zanzibar, ambao wana uhusiano wa miaka mingi na wenzao wa Oman.
Mapema, akitoa taarifa za
ujenzi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Saleh Mohammed Jidawi, alisema
hadi kukamilika kwake, ujenzi huo umegharimu dola za Kimarekani milioni 2.36,
na samani zake dola 277,000.
Naye Waziri wa Afya Juma
Duni Haji, alisema kujengwa chuo hicho na kuongezwa kwa dakhalia hizo,
kutawaondoshea wanafunzi na walimu usumbufu kwani saa watapata nafasi ya kusoma
na kufanya kazi kwa utulivu. Mkuu wa chuo hicho Dk. Haji Mwita, aliishukuru
serikali kwa kushirikiana na uongozi na bodi ya chuo katika jitihada za
kukiendeleza huku akiainisha changamoto kadhaa zinazohitaji kupatiwa ufumbuzi
zikiwemo uhaba wa walimu, usafiri, vitendea kazi na uvamizi wa eneo la chuo
unaofanywa na watu mbalimbali.
Kwa upande wake, Mshauri
wa masuala ya afya wa serikali ya Oman, Dk. Sultan Al Busaidy, akitoa salamu
sake kwa niaba ya nchi yake, alisema nchi yake inaona fahari kubwa kuiona
Zanzibar ikipiga hatua katika kustawisha hali za watu wake, hasa katika sekta
ya afya na elimu.
Alisema serikali ya nchi
yake, inajivunia uhusiano wa dhati na udugu wa damu uliopo kati ya wananchi wa
nchi mbili hizo, na akawaombea Wazanzibari mafanikio zaidi katika kuleta
maendeleo. Ujenzi wa majengo hayo uliofanywa na kampuni ya Mazrui Building
Contractors, uliwekwa mwezi Januari 2011, baada ya kuwekwa jiwe la msingi na
Rais Dk. Shein tarehe 6 ya mwezi huo.
No comments:
Post a Comment