Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WIKI iliyokwisha ilikuwa na mshike mshike mzito kutoka kwa
klabu ya Yanga, baada ya kusemekana kuwa uongozi ulikuwa na lengo la kumuajiri
Katibu Mkuu Mkenya, baada ya nafasi hiyo kukaimiwa kwa muda sasa na Lawrence
Mwalusako.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, pichani.
Ulikuwa ni mshike mshike mkubwa mno. Kila mmoja alisema
lake, huku majibizano hayo yakichangiwa na habari hizo za Patrick Naggi kupewa
nafasi hiyo nyeti ndani ya Yanga.
Ili kukoleza joto hilo, Baraza la Wazee kwa kupitia Katibu
wao Ibrahim Akilimali, alitangaza hali ya hatari kwa Naggi kuwa asipoangalia
atatolewa madirishani.
Hiyo ni kutokana na wao kupinga vikali, hivyo raia huyo wa
Kenya afungashe virago vyake kama kweli alikuwa ameajiriwa na klabu yao ya
Yanga, moja ya timu kongwe kabisa barani Afrika.
Yanga iliyoanzishwa rasmi mwaka 1935, haikuwahi kuongozwa na
Katibu Mkuu mgeni, akiwapo Naggi mwenyewe. Hii ndio kusema kuwa, endapo hilo
lingefanikiwa, basi ndio wangeanza mwanzo wa mwendelezo huo kwa maslahi ya
klabu yao.
Inawezekana si tatizo kwa timu kama Yanga au Simba kuwa na
Katibu Mkuu ambaye si raia wa Tanzania. Inawezekana kabisa Mkenya, Mganda na
wengineo kupewa nafasi hiyo.
Kwani kuna ubaya gani? Mbona nafasi za makocha zinapewa
wageni? Tunapotaka kuzungumzia soka la Kimataifa na mikakati yake, Siwezi
kuvumilia kuona licha ya Dunia kuendelea, lakini baadhi ya klabu zetu
zinajiendesha ndivyo sivyo.
Hata hivyo, hata huyo Yusuph Manji na jopo lote la uongozi
wa Yanga haliwezi kufanya lolote zaidi ya kuwasikiliza wanachama wao. Wanachama
ambao kwa sababu wanazojua wao, eti wamekuwa wakiwaweka mbele kuliko kitu
kingine.
Kama leo tutalaumu kwanini wazee wa Yanga wametoa tamko zito
la kumtoa Naggi dirishani endapo atathubutu kuwa Katibu Mkuu wao, tulaumu pia
uongozi kwa kushindwa kuwa makini na kutetea misimamo ya kimaendeleo.
Ni juzi tu Yanga walitangaza kuitisha Mkutano Mkuu wa
dharula. Mkutano huu ulikuwa na nia ya kuwapa nafasi wanachama wao wapitie
mkataba wa Azam TV.
Wajuzi wa mambo ya soka walishangaa. Shirikisho la Soka
nchini (TFF) nalo likashangaa. Hawa Yanga, chini ya viongozi wao waliowachagua
kwa ridhaa yao wanashindwa kutoa uamuzi hadi waitishe mkutano?
Kuna nini katika suala hilo? Hizi fedha za kuandaa mkutano
huo zingetoka wapi na kwa manufaa gani? Jibu lilishapatikana kwa Yanga. Ni pale
waliposema hawawezi kukubali mechi zao zionyeshwe kwenye luninga ya klabu
ambayo nayo ni mshindani wao, yani Azam.
Sawa, hilo lilikubaliwa ndio maana wakaambia pia katika
mechi zao ambao wao ni wenyeji watasikilizwa, ila pale ambapo wao ni wageni
hawatakuwa na sauti ya kugomea wasionyeshwe.
Jasho likawatoka. Wakaona wameshindwa kudhibiti hilo, maana
timu zote 13 zimeridhia isipokuwa wao tu. Wakati hayo yanaendelea, ndipo
serikali nayo ilipoingia na kuwataka mwanasheria wao apitie upya mchakato huo
na Yanga kuamua kusitisha mkutano wao huo uliopangwa kufanyika katika Ukumbi wa PTA Sabasaba.
Ni kutokana na hilo, Yanga hii, yenye viongozi kama Manji
kamwe haiwezi kuamua lolote la haja. Inawezekana kabisa wapo wasomi Tanzania
ambao ni wanachama wa Yanga wanaweza nafasi ya Mwalusako, ila inapotokea nafasi
ya kumuajiri mgeni asikataliwe.
Pamoja na hayo, inahitaji maelewano, ukizingatia kuwa klabu
hizi zinazojiita kongwe, zinazolingia wanachama, zimesheheni watu wa kila aina
na wenye mitizamo tofauti.
Ndio maana nasema, kwa Yanga hii si ya kuwa na Katibu Mkuu
mgeni bila kuelimishana faida inayoweza kupatikana katika hilo.
Ukiacha hilo, Yanga pia imekuwa ikiwaweka mbele wanachama
wao kwa kuwasikiliza na kuwapa nafasi ya kuamua, kama vile walivyowapa nafasi
ya kuamua juu ya Azam tv.
Kinyume cha hapo kunaweza kuibuka mgogoro mzito utakaoweza
kuathiri klabu hiyo ya Yanga. Hilo likitokea kamwe sitaweza kuvumilia.
+255 712053949
No comments:
Post a Comment