Na Kambi Mbwana,
Dar es Salaam
NYOTA
njema huonekana alfajiri. Msemo huu maarufu hapa nchini Tanzania umezoea
kutumiwa kila mtu anapotaka kuelezea jambo zuri linaloanza kuonekana mapema,
hasa kwa watoto.
Mwamuzi chipukizi wa mpira wa miguu, Nadin Leonard Dim, pichani.
Mtoto
anayefanya mambo mazuri licha ya umri wake huo, ni rahisi mtu kuweka msemo huo,
kama ishara ya kubariki mwenendo wa kitu kinachoonekana mbele yake na
kinachosubiriwa kwa hamu.
Ndio,
msemo huu naweza kuutumia ninapomzungumzia Nadin Leonard Dim, mtoto mwenye
miaka 16 anayefanya kazi nzuri katika fani ya kupuliza filimbi, yani mwamuzi wa
kati.
Ni
mwepesi mno, Anahaha uwanja mzima. Hana hata chembe ya uonevu anapokuwa dimbani
akichezesha mechi, jambo linaloonyesha shauku ya kuona mazuri mengine ya kijana
huyo wa baadaye.
Kwa
waliobahatika kumuona Nadin, hasa katika mechi mbalimbali anazokuwa dimbani,
hasa zile za kirafiki katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam,
atakubaliana na mimi kuwa ni hazina.
Mapema
mwaka huu Nadin alichezesha mechi ya kirafiki kati ya Ashanti United na Moro
United na kuwakuna wengi. Nadin ambaye kwa sasa ni mwamuzi wa daraja la tatu,
wilaya ya Ilala, Ijumaa iliyopita alichezesha mechi ya kirafiki kati ya bendi
ya Mapacha Watatu na Mashujaa Music.
Alifanya
vitu vikubwa katika mchezo huo na kuamsha mijadala ya kila aina kutoka kwa
wadau wa michezo waliodhuhuria mchezo huo katika Viwanja vya Leaders Club,
Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Katika
mazungumzo yake aliyofanya na Handeni Kwetu Blog, Dim anasema kuwa anapenda
sana kazi hiyo ya kuchezesha soka kwasababu kila mtu anamsapoti anapokuwa
dimbani.
Anasema
kuingia kwake kwenye kazi hiyo kunatokana na yeye kupewa filimbi tangu
alipokuwa katika shule ya Sekondari Azania, jijini Dar es Salaam, akiendelea na
elimu yake ya sekondari.
“Wakati
naendelea na masomo yangu, shule iliamini naweza mno kusimama dimbani kucheza
mechi mbalimbali, jambo ambalo baadaye nilipata ushauri kuwa niingie rasmi.
“Mwalimu
wangu wa michezo ninayemfahamu kwa jina la Kaboneka, alinishauri pia
nitafute kozi kwa ajili ya kupata elimu inayohusiana na mambo ya mwamuzi ili
nifike mbali zaidi,” alisema Dim.
Anasema
baada ya kupewa ushauri huo, aliamua kuufanyia kazi na kushiriki katika kozi ya
ukocha kwa watoto iliyoandaliwa na Chama Cha Soka Kinondoni (KIFA) mapema mwaka
huu.
Hatua
hiyo imempa mwangaza zaidi na kufanikiwa kupenya na kupata daraja la tatu
wilaya Ilala. Kwa hatua aliyofikia sasa, Dim anaweza kuitwa na kupewa mechi
mbalimbali za vijana na zile za kirafiki.
Anasema
hana woga anapokuwa uwanjani kwasababu lengo lake ni kuchezesha kwa haki bila
kuangaliana usoni. Dim anasema hata kama katika moja ya timu anayochezesha kuna
mtu anayempenda, hawezi kumpa wepesi ili amfarahishe na kumnyonya mwingine.
“Nahitaji
kufika mbali zaidi katika mchezo wa soka, hivyo kwa sasa ninachotaka kuifanya
ni kuona nachezesha mechi kubwa zaidi zinazoshiriki ligi Kuu, kama vile Simba,
Yanga, Mtibwa Sugar na nyinginezo.
“Naamini
mpango huu utakuwa na mashiko katika harakati zangui za kimaisha, ukizingatia
kuwa nina hamu ya siku moja nionyeshe namna soka linavyopaswa kuchezeshwa
uwanjani,” alisema Dim.
Dim
anayesoma kidato cha pili shule ya Sekondari Azania, amezaliwa mwaka 1997
katika Hospitali ya Mbezi Juu, jijini Dar es Salaam. Kwa sasa anaishi na wazazi
wake Vingunguti jijini hapa.
Dim
anayevutiwa na soka la Mbwana Samatta, mshambuliaji wa timu ya TP Mazembe ya
Congo, ana mipango kabambe ya kuhakikisha kuwa anafika mbali ndani nan je ya
nchi.
Mtoto
huyo anayevutia kumuangalia anapochezesha soka, anaitaka TFF kufanyia kazi
malalamiko ya waamuzi ili kuondoa kero sugu za ugumu wa maisha unaowakabili na
kufikia kudai hongo.
“Huu ni
wakati wa kuwaza namna gani ya kukuza soka letu, hivyo hakuna njia ya mkato
katika hilo na ndio maana naendelea kujipanga ili mambo yaende vizuri katika
soka la Tanzania.
“Naamini
kwa kufanya hivyo soka letu litasonga mbele na kufikia malengo yetu, hasa kwa
kuhakikisha kuwa TFF wanasimamia vyema mfumo wa utendaji kazi wa waamuzi hasa
katika maslahi yao,” alisema.
Katika
hatua ya kushangaza zaidi, Dim mwamuzi chipukizi na mwenye ndoto lukuki,
anasema hana anayempenda katika idadi ya waamuzi wote Tanzania na kusema ndoto
zake zitatimia kwasababu wengi wanamuunga mkono na kumpenda asimame langoni.
No comments:
Post a Comment