Baadhi ya
ndugu wa marehemu, Erasto Msuya awaliofurika katika mahakama ya hakimu mkazi
Moshi, Mkoani Kilimanjaro, wakimpakiza Mama yao (jina halikufahamika
maramoja) kumkimbiza katika Hospitali ya KCMC baada ya kuanguka na kupoteza
fahamu mahakamani hapo.
|
Na Mwandishi wetu, Moshi
KESI ya
mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Erasto Msuya (43), imelazimika kusikilizwa
katika mahakama ya ndani baada ya kutokea sintofahamu huku mmoja wa waandishi
wa habari aliyekuwa akifuatilia kesi hiyo akishambuliwa na ndugu wa Marehemu.
Kesi hiyo iliyotajwa kwa mara ya kwanza katika
mahakama ya hakimu Mkazi Moshi, Agosti 21 mwaka huu, ilipangwa kusikilizwa
katika mahakama ya wazi lakini kutokana na kuwepo kwa umati mkubwa mahakamani,
kesi hiyo ilihamishiwa mahakama ya ndani jambo lilowakera ndugu wa marehemu.
Baada ya kuambiwa kesi hiyo imehamishiwa mahakama ya
ndani, Ndugu wa Marehemu walionesha kukerwa na kitendo hicho na kuanza kufanya
vurugu na kulazimisha maaskari wa mahakama kuingilia kati wakisaidiwa na wale
wa kutuliza ghasia (FFU).
Katika tukio hilo, waandishi wa habari wachache
walioruhusiwa kuingia kusikiliza kesi hiyo walijikuta katika wakati mgumu, huku
mmoja wao, Venance Maleli wa kituo cha Redio cha Moshi FM akishambuliwa na
wanandugu hao ambao pia walitishia kumnyang’anya kamera yake.
Tukio hilo halikuishia hapo kwani, Mwandishi wa
Gazeti hili, alifanyiwa fujo na ndugu wa Marehemu ambao hawakutaka kupigwa
picha wakati wakifanya juhudi za kumkimbiza hospitalini Mama yao, aliyepoteza
fahamu baada ya kupata taarifa za kuahirishwa kwa kesi hiyo.
Aidha baadhi ya waandishi wa habari waliokuwa
mahakamani hapo walilazimika kuondoka kwa kujificha kwa kuhofia usalama wao.
Katika kesi hiyo dakika hiyo iliyochukua takribani
dakika 25 tu, watuhumiwa wengine wanne waliunganishwa katika shtaka hilo la
mauaji kwa kukusudia kinyume na kanuni namba 16, kifungu cha 196 ya sheria za
makosa ya jinai.
Watuhumiwa hao ni Joseph Damas maarufu Chusa mkazi
wa Jijini Arusha, Jalila Zuberi Said (28), mkazi wa Babati, lakini pia anakaa
Manyara na Kondoa , Sadiki Mohammed Jabir “msudani” au “mnubi”(32), mkazi
wa Dar es salaam na Langata wilayani Hai na Karim kihundwa (33) mkazi wa kijiji
cha Lawate wilayani Siha na kufanya jumla ya watuhumiwa kufikia 7 mpaka sasa.
Hata hivyo maelfu ya wananchi waliofurika mahakamani hapo kufuatilia kesi hiyo,
walionesha kukerwa na kitendo cha kutoruhusiwa kusikiliza kesi hiyo ambapo mara
tu baada ya kesi hiyo kuahirishwa walionekana kukimbilia mlango wa kutokea.
Watuhumiwa hao wote 7 waliondolewa mahakamani hapo
kwa ulinzi mkali wa Jeshi la polisi wakiwa wamepakizwa katika Gari ya polisi,
namba za usajili T 743 ADC iliyokuwa na Madirisha Meusi (tinted).
Kesi hiyo inayoendeshwa na wakili wa Serikali,
Stella Majaliwa akisaidiwa na Janeth Sikule katika Mahakama ya Hakimu Mkazi,
Ruth Mkisi imeahirishwa hadi October 2 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa tena.
|
No comments:
Post a Comment