Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
VIJANA na wakazi wa kijiji cha Komsala, Kata ya Kwamatuku,
wilayani Handeni mkoani Tanga, wanaoishi kwa kazi ya kuvunja mawe sasa
watakutana na kazi nzito ya kulipishwa ushuru kutokana na kazi yao hiyo
inayotumia nguvu nyingi kuifanya.
Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu.
Kwa mujibu wa mkazi mmoja wa kijijini hapo, serikali ya
kijiji imeweka bango la kuonyesha kuwa kila tripu moja ya mchanga, kokoto na
mawe makubwa italazimika kulipiwa ushuru.
Mkazi huyo alisema kuwa tangazo hilo linaanzia kwa shilingi
5000, huku likitajwa kuwa kama mzigo mwingine mzito kwa wananchi hao wa kijiji
ambao wengi wao wakiwamo vijana wanaishi kwa kazi ya kuvunja mawe mlimani kwa
zaidi ya miaka 50 sasa.
Ni tofauti na maeneo mengine ambayo wananchi wake hasa
vijana wanaishi kwa kazi ya kulima vibarua, kukata mkaa na nyinginezo, Komsala
wao wanaishi kwa kuvunja mawe yanayouzwa katika wilaya ya Korogwe na
kwingineko.
Tayari hatua hiyo imedaiwa kuibua mkanganyiko mkubwa, ikiwa
ni mwendelezo wa malumbano kati ya serikali ya kijiji na wananchi wake, hasa
vijana.
Ni mapema mwaka huu idadi kubwa ya vijana iliporudisha kadi
za uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa madai kuwa inachoshwa na
uendeshwaji mbovu wa kijiji hicho pamoja na maamuzi ya kutoka ngazi ya wilaya.
“Hatujui kitakachoendelea baada ya tangazo hili kuwekwa
maana ni dhahiri halitawafurahisha vijana kwasababu fedha hizo ni nyingi na
hawa wananchi wanafanya kazi ya mawe kwa kutumia nguvu zao nyingi, sasa
inashangaza mtu anaweka ushuru bila hata kuwasaidia japo vifaa vya
kuwafanikishia kaziz hiyo.
"Hapa watu wanaumia, wanamwaga jasho jingi, sasa inashangaza
kuona fedha zao zinahitajika, wakati kuna vyanzo vingi vya mapato, kama vile
migahawa, magenge, maduka na mengineyo, ikiwamo ardhi,” alisema.
Kwa bahati mbaya hatukuweza kupata sauti ya Mwenyekiti wa
kijiji hicho, lakini jitihada zinafanywa ili azungumzie sakata hilo la kuweka
ushuru wa mawe kwa kila tripu itakayouzwa kutoka mlimani.
No comments:
Post a Comment