Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UMUHIMU wa elimu ni pale inapotumika kwa maslahi ya wananchi
wote, hata wale wasiobahatika kufikia kiwango hicho. Kama mtu mwenye elimu
anafanya mambo yasiyokuwa na faida, jibu lake ni kuwa elimu yake hiyo haina
msaada na haina tija.
Watanzania kama hawa wanahitaji maisha bora ili wawe na uhakika wa mlo kamili na sio wengi wao kuzuunguka bila mafanikio. Wabunge na watendaji wengine wa serikali wakiunganisha vikundi kwa watu hawa wanaweza kujikimu kwa kufanya biashara mbalimbali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.
Mtu wa aina hiyo ni kama yule anayetembea bila kuvaa nguo,
ingawa mguuni mwake ametinga kiatu kizuri, akijidanganya kuwa amejikinga na
kukanyaga vinyesi au misumari na miiba.
Kadri ya siku zinavyozidi kwenda mbele, kumekuwa na mihemko
kutoka kwa watu wanaoamini kuwa ili mbunge awe na faida kwa wananchi lazima awe
ni profesa au dokta.
Hata hivyo haitoshi, watu hao wanafika mbali zaidi wakiamini
kuwa watu wa aina hiyo wana uwezo wa kuwawakilisha vyema wananchi wao, jambo
ambalo si kweli.
Japo sipingi wabunge wenye elimu au wale wanaotaka kuwania
nafasi hiyo wawe na kiwango kikubwa kama kinavyohitajiwa na wengi, ila muhimu
ni kuwataka watu hao wahakikishe kuwa elimu zao zinawanufaisha Watanzania na
wapiga kura wao wanaoishi maisha ya kubahatisha, huku wao wakiishi kifalme.
Kwa mfano, mbunge wa Korogwe Vijijini, Profesa Stephen
Ngonyani, maarufu kama Maji Marefu ameonyesha utofauti mkubwa na wabunge wenzake,
wakiwamo wapya na wa zamani.
Maji Marefu amekuwa karibu mno na wapiga kura wake. Ukienda
Kororgwe Vijijini utafahamu mazuri anayofanya mbunge huyo aliyeingia madarakani
mwaka 2010.
Binafsi naupongeza mchango wa Maji Marefu, huku nikitangaza
vita na wabunge wengine wasiokuwa na jipya wala faida kwa wapiga kura wao miaka
nenda rudi.
Kwa mfano, kazi ya kwanza ya mbunge ni kuwaunganisha
wananchi wake ili ajuwe namna ya kuwaletea maendeleo. Hii si mpaka mbunge
asubiri mipango kutoka ofisi nyingine ya serikali.
Mbunge anaweza kuanza kuunganisha vikundi vya wananchi, kama
vile wakulima, wafugaji, wafanyabiashara katika masoko mbalimbali kwa nia ya
kuwaweka pamoja.
Baada ya kufanya hivyo, kama mfuko wake hauna fedha za
kuendesha vikundi hivyo, anaweza kubuni njia nyingine ya kuwasaidia ukiacha
utaratibu wa kuomba misaada kutoka kwa wahisani.
Kikundi chochote kilichokuwa na wafanyabiashara hata wa
nyanya sokoni, wakajiunganisha watu wasiopungua 50 hadi 100 wanaweza kujiwekea
njia ya utajiri mkubwa mno.
Hawa wakiamua kuchangishana hata 10000 kwa mwezi ni sawa na
120,000 kwa mwezi mmoja. Watu hao wakiendelea na utaratibu huo kwa mwaka mmoja
watavuna jumla ya Sh Milioni 120.
Fedha hizo sidhani kama zitashindwa kuwasaidia na kuwawekea
mfumo mzuri wa kimaendeleo. Watu wa aina hii wapo wengi. Mbunge makini na
mwenye mtazamo wa mbali kwanini ashindwe kufanya mpangilio huu kwa ajili ya
maendeleo ya wapiga kura wake?
Serikali inaamini kuwa ili iweze kuwasimamia wananchi wake
na hata kuwakopesha lazima wajiunganishe kwa vikundi. Je, nani wa kufanya hayo?
Tunahitaji elimu ya Chuo Kikuu kubaini fursa nyingi zinazoishia hewani?
Kwa bahati mbaya, mara kadhaa inapotokea wananchi wenyewe
wanahitaji kujiletea maendeleo kwa kuunganisha vikundi, hutokea mgawanyiko
unaoshangaza wengi.
Mara kadhaa wabunge na wanasiasa wengine wamekuwa wakihofia
nafasi zao, hivyo kutumia hila kuwasambaratisha. Huu sio mpango mzuri. Hatuwezi
kuendelea kama hatuna uthubutu.
Watu wanaishi maisha magumu. Kule kwetu wilayani Handeni,
mkoani Tanga, kila siku ni malalamiko. Mbunge wa Handeni, Abdallah Omari
Kigoda, ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara anakutana na shughuli pevu
mno.
Wengi wanaamini katika kipindi cha miaka 20 alichokaa
bungeni hakuna cha maana alichofanya, japo kuwa kuna barabara nzuri sasa kutoka
wilayani Korogwe kwenda Handeni na ile inayotoka Handeni kwenda Mkata. Hata
hivyo, malalamiko hayo kwa viongozi hayawezi kukosekana hata kidogo.
Kama tunavyojua, mema mengi hufichwa na baya moja tu, hivyo
hata kama afanye mema mangapi, lakini kama kuna anayelala analala njaa, anayeshindwa
kupata huduma muhimu za afya, anayekosa vitu vyenye kuongoza maisha yake, huyo hawezi
kukaa na kushangilia, hasa katika kipindi hiki ambacho wananchi wamekuwa na
ujasiri wa kuuliza au kuwajibisha viongozi wao.
Kama watu wanakosa mbinu mbadala za kupambana na shida ya
maji, njaa kila mwaka, vijiji vingi hata vile vilivyokuwa kwenye (underline)
vinakosa huduma muhimu ya umeme, kamwe wananchi wake hawawezi kufurahia mfumo
na uongozi wao.
Huu ni wakati sasa wa kukaa na kutafakari mwenendo wa
uongozi, hasa wabunge ambao ndio wawakilishi wa wananchi. Kwa bahati mbaya,
wengi wa wabunge hao wanaolalamikiwa wanatokea katika Chama Tawala, yani Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
Kama hivyo ndivyo, ugumu wa maisha, kulala kwa baadhi ya wabunge
wake ni pigo kwa CCM. Mwaka 2015 huenda ukawa mgumu kwa baadhi ya majimbo
ambayo wabunge wao wamekosa mbinu mbadala za kuwakomboa wananchi wao.
Kwa mtindo huo, CCM itakuwa inakosea sana kama itaamini kuwa
wabunge wao hao wanabebeka. Lazima itafute namna ya kuwadhibiti au kuwasimamia
hasa katika miaka miwili hii iliyobakia.
Katika kila jimbo au wilaya, lazima kutakuwa na kero sugu
ambayo inaumiza watu wengi. Maeneo mengine ni barabara za uhakika na kwingine
ni maji au umeme.
Huduma hizi, yani barabara, maji na umeme ni muhimu.
Yanagusa maisha ya mlalahoi kabisa. Tajiri hawezi kulalamika. Kama barabara
haipitiki, yeye haimuhusu kwasababu muda mwingi anaishi mjini.
Kama tatizo ni maji, yeye anaweza kuchukua maji mahali
popote apendapo kwa ajili ya maisha yake. Kama tatizo ni umeme, anaweza kununua
solar power na kutumia kadri apendavyo.
Akiugua hana shida ya kutibiwa katika zahanati ambayo tangu
ijengwe haijawahi kuwa na dawa za kutosha. Hata zile za kupunguza makali ya
homa ya matumbo wanazipata zikiwa zimeshaharibika kutokana na kutohifadhiwa
sehemu nzuri na salama.
Haya yote yanafanyika katika maeneo yenye wabunge
waliochaguliwa kwa mtindo wa kura. Tena baadhi yao wanajipitisha kwa wananchi
au katika vyombo vya habari wakijitangaza kuwa wao ni machaguo halisi ya wapiga
kura wao.
Ni sahihi kujiita hivyo. Lakini mtu huyo anapaswa kupima
viatu vyake. Ni vyema pia akafikiria namna wananchi wake wanavyoteseka. Ni
vyema akafikira nafasi yake bungeni.
Tangu alipoingia madarakani, ni mara ngapi ameweza kusimama
kuuliza maswali yanayowahusu wananchi wake? Je, tangu alipoingia madarakani,
ameweza kutekelekeza mambo mangapi?
Kipi kipaumbele chake? Je, ipi mipango yake katika kipindi
cha miaka miwili hii iliyosalia? Kimahesabu, bado mwaka mmoja tu. Tena ule ambao
utakapoingia utakuwa na mlolongo mrefu.
Ni mwaka wa Uchaguzi wa serikali za mitaa. Uchaguzi ambao
kila chama utatumia kujiimarisha na kujiwekea mikakati ya kushinda uchaguzi
Mkuu mwaka 2015.
Kama hivyo ndivyo, namna gani wabunge hao wataweza kujipanga
kwa ajili ya kuwakomboa wapiga kura wao? Hakuna njia ya mkato. Katika hili kila
mtu lazima atomize wajibu wake.
Japo wasema kweli wataonekana ni wachochezi lakini bora
waseme ili wajisahihishe. Hii ni kwasababu hata CCM wenyewe wanaamini kuwa wao
sio malaika.
Katika utawala wao kuna mabaya na mazuri. Yale mabaya
wanaamini watayafanyia kazi kwa ajili ya kuwapatia maisha bora wananchi wao
katika kipinddi chote cha utawala wao.
Kuna mengi yanayostahili kufanywa, ila kubwa ni kuhakikisha
kuwa wabunge wao wanakuwa wawakilishi wa wananchi wao. Waone ile thamani ya wao
kulipwa mshahara mnono na mazuri mengi kutoka bungeni.
Wabunge hawa wauchukie kwa vitendo umasikini. Watumie muda
wao kuwa karibu na wananchi wao. Waanzishe miradi ya kimaendeleo, kama vile ufugaji
wa nyuki, ufugaji wa kuku wa kisasa na kienyeji, kuvua samaki na mengineyo.
Wasimamie vyema sera ya kilimo kwanza ili kiwe na tija.
Wafanikishe kupatikana kwa pembejeo za kilimo na kuwakopesha wananchi wao
sanjari na kuwadhibiti katika uuzaji wa mazao yao.
Wabunge hawa watafanya hayo kwa kutumia wataalamu wa
serikali waliozagaa kila wilaya kwa ajili ya kusimamia sera hizo na fursa za
kimaendeleo.
Wakifanya hivyo, hata elimu zao zinazopigiwa chapuo
zitaonekana ni muhimu, maana zinafanikisha maisha bora kwa Watanzania wao, hasa
wale waliosimama mstari kuwapigia kura.
Aidha, sera hii itakuwa ni tunu kwa Watanzania wote,
ukizingatia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho
Kikwete, anaamini kuwa katika kipindi cha uongozi wake, lazima wananchi wake
wayapate maisha bora.
Hili linaweza kufanikiwa kwa vitendo kwa kuhakikisha kuwa
wabunge wao wanashirikiana vyema na wananchi wao na sio wale wanaotumia muda
mwingi kujenga makundi yao. Wale
wanaotumia muda mwingi kufanya biashara zao.
Wale wasiokuwa hata na muda wa kuzungumza na wananchi wao
kuona namna gani ya kuwapatia mwangaza wa kimaisha kwa kupitia wao walioomba
fursa ya kuwaongoza.
Tusipofanya hivyo, wananchi watakuwa na chuki na viongozi
hawa hasa katika kipindi cha Uchaguzi ambapo hakika uwezekano wa kupiga kura za
chuki ni mkubwa mno.
+255712053949
Mwisho
No comments:
Post a Comment