https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, September 20, 2013

Waziri Chizza aingilia kati mgogoro wa wakulima wa Chai wilayani Lushoto, mkoani Tanga



Na  Ray Said, Bumbuli
WAZIRI  wa  Chakula, Kilimo  na  Ushirika, Injinia Christopher  Chizza, amependekeza kuundwa kwa menejimenti ya muda katika kiwanda cha chai cha Mponde kama njia ya kusuluhisha mgogoro uliopo kati ya wakulima wa chai na mwekezaji wa kiwanda hicho, Kampuni ya Chai Lushoto.  
 Injinia Christopher  Chizza, katikati.
Akizungumza katika mkutano wa  hadhara  uliofanyika  katika  uwanja  wa  mazoezi katika kata ya Mponde, Chiza  pia aliahidi kushughulikia mgogoro uliopo kati ya wakulima hao wa chai na mwekezaji wa kiwanda cha chai cha Mponde, kilichopo Bumbuli, mkoani Tanga, ili kiendelee kutoa huduma bora.

 Alisema katika kumaliza mgogoro huo, atazungumza na Waziri Mkuu, Mizengo  Pinda kuhusu suala hilo ili kusaidia kupata ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huo.

"Nitaishauri  serikali  kuchukua  kiwanda  hicho  na  baadaye   kuwakabidhi  wananchi  ambao  ndio  wamiliki  wa  kiwanda  hicho," alisema.

Mgogoro kati ya wakulima na mwekezaji unatokana na madai ya wakulima hao kuelezea kuwapo kwa upotevu wa fedha kiwandani na viongozi wa Chama cha Utega, hivyo kupoteza imani kwa wakulima kwa madai kuwa wapo upande wa mwekezaji anayewanyonya wakulima wa chai.

Waziri huyo pia alisema  watapeleka wakaguzi kutoka  serikalini  kuchunguza  kama  kuna ubadhirifu wowote  kiwandani hapo ili  kuwasaidia wakulima wa chai kupata haki yao na kulisaidia zao hilo ambalo ndio kitega uchumi.

Waziri Chiza alisema kuwa ana imani uchunguzi utakaofanywa na  wakaguzi kutoka  serikalini utaleta  majibu mazuri kwa kuwa utaonyesha   kuna ubadhirifu.

Alisema  wao upande serikali  hawawezi  kuendelea  kuona  zao  la  chai  linaoza, hivyo  lazima  lithaminishwe  kwa  kuuzwa  kwenye viwanda  vingine na lazima mgogoro huo upatiwe ufumbuzi.

“Tutamaliza  mgogoro  huu  kwa  kupata  suluhisho  la  haraka  ili  wakulima  wapate  haki yao  ya  msingi  na  badae  waendelee  kulilinda  zao  la chai  kama  ilivyokuwa  zamani,” alisema  Waziri huyo.

Waziri huyo alisema kuwa Chama cha UTEGA lazima kifanye mkutano mkuu ili kujadili matatizo yanayokikabili na akaahidi kuwa serikali iko tayari kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia mkutano huo.

pia aliahidi kuwa Wizara yake na Wizara ya Viwanda na Biashara wa kushiriiana na Wizara ya Mambo ya Ndani watafanya ukaguzi wa Chama hicho ili kujua kama kinaendeshwa kwa mujibu wa kanuni na sheria za Tanzania.

Wakulima  hao wakizungumza  katika  mkutano huo  wa  kujadili kero mbalimbali ambazo zinawakabili, walisema kuwa wako tayari kukosa fedha kwa kipindi chote  ambacho kiwanda kitakuwa kimefungwa kuliko kuendelea kunyanyaswa na wawekezaji hao.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...