https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, September 16, 2013

SIWEZI KUVUMILIA:Bila kuwajali waamuzi kimaslahi watafungiwa kila siku


Na KambiMbwana, Dar es Salaam
SIKU zote mbwa ambaye ananyimwa chakula pale anapofugwa au kupewa kile asichoshiba, kamwe hawezi kukaa kwa furaha badala yake atatafuta namna ya kujikimu.
Msemaji wa TFF, Boniface Wambura, pichani.
Kubwa analoweza kufanya, ni kwenda katika nyumba za jirani kuokoteza makombo au kwenda jalalani kula mifupa na vitu vingine, vikiwamo vinyesi.

Hawa ndio wanaoitwa mbwa koko. Chochote kinachokuwa mbele yao wanakula. Kwa bahati mbaya, mbwa hawa wanafanya hivyo kwasababu hawana kingine cha kula.

Kama ilivyo kuwa kwa binadamu, hata wanyama nao wakiwamo mbwa hakuna asiyependa kitu kizuri. Nasema hivi kama mfano juu ya sakata la maisha duni ya waamuzi wa Tanzania. 

Hawa wamekuwa wakilalamikia sana kucheleweshewa posho zao kila wakati. Kwa bahati mbaya, licha ya kucheleweshewa fedha hizo, bado wanatakiwa wachezeshe mechi zenye ushindani au upinzani.

Hii siwezi kuvumilia asilani. Ni wakati wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuweka mipango ya kuwapatia chochote kitu hawa, tena kwa wakati muafaka ili kuwapa ugumu wa kuchukua hongo.

Tukifanya hivyo, tunaweza kukuza soka letu. Soka linaloweza kudumaa kama sharia 17 hazitafuatwa kwasababu mbalimbali, hasa ugumu wa maisha ya waamuzi wetu.

Kwa mfano, mwamuzi anatoka mkoani Mwanza na kwenda Arusha kuchezesha mechi ya JKT  Oljoro na Coastal  Union au nyinginezo, hali ya kuwa hajui familia yake itakulanini.

Huyu akifika Arusha lazima awe na mawazo. Tena wakati mwingine hata asipopewa hiyo rushwa inayotajwa kila wakati, atakuwa na msongo wa mawazo.

Hata chezesha kwa moyo kama inavyostahili. Kama wafanyakazi wa idara kadhaa wanagoma kila siku wakishinikiza malipo yao, vipi kwa hawa waamuzi?

Nini hatimaya maisha yao? Juzi tu TFF imemfungia mwaka mmoja mwamuzi Martin Saanya.

Saanya amefungiwa kwasababu ya kuchezesha chini ya kiwango au akiwa na lengo la kuibeba moja ya timu kati ya Yanga na Coastal Union.
Sawa, ila aliangaliwa tatizo lake la msingi?  Je, kabla yakupewa kazi hiyo wadau wanajua mfumo wa utendaji kazi wao? 

Sina haja ya kuwabeba zaidi waamuzi, ila ukweli ni kwamba lazima TFF iweke mifumo imara kwa sekta hiyo.

Mwamuzi anayelipwa ujira mdogo, asiyepewa kwa wakati, lazima apindishe sharia za soka. Tena Tanzania hii inayoona Simba na Yanga ndio kila kitu?

Hata kama akishindwa kufanya hivyo kwa Simba na Yanga, atakuja kuwa bana moja wapo ya timu itakayohitaji mbeleko ya mwamuzi katika patashika ya ligi ya Tanzania Bara.

Huu ni wakati wa kuzinduka, maana hakika siwezi kuvumilia kuona kila siku malalamiko ya waamuzi yamekuwa wimbo wa Taifa. Japo si wote wenye tabia hiyo, lakini upo msemo wa wahenga unaosema kuwa usipojenga ufa utajenga ukuta.

Tukarabati ufa wetu kwa sekta ya mpira wa miguu ili harakati hizi ziwe na tija na kuokoa mpira wetu. Tanzania ni nchi inayofanya vibaya kwa medani yakandanda.

Kimataifa sisi ni wa moja kabisa. Hatuwezi kuvaa miaka tika kipindi hiki kinachochagizwa na kasumba za kila aina. Tuhuma za rushwa kwa waamuzi ni tatizo.

Wanapatikana washindi wa kubebwa wasiokuwa na jipya, hivyo kulifanya soka letu libaki kama lilivyokuwa. Hii si haki.

Na hakika siwezi kuvumilia, hivyo kuna kila sababu ya wadau wa soka kujipanga, wakiwamo TFF ambao ndio baba wa mpira wa miguu hapa nchini.

Moja wapo ya mipango inayotakiwa kufanywa na TFF ni kuwawekea mazingira mazuri ya kimaisha waamuzi wetu. Walipwe vizuri kulingana na makubaliano yao.

Wasishawishiwe na watu kwasababu ya njaa zao. Ni ajabu mwamuzi kulipwa kwa kusuasua wakati anachezesha mechi ya Simba na Yanga itakayoingiza Milioni 300.

Hili ni jambo lisiloweza kufanywa kwa Dunia ya leo inayoweka mbele maslahi na ndio maana tuna shindwa kuona burudani nzuri ya soka, hasa kama mkono wa mtu umepita.

Kwa mtindo huu tutaendelea kulalamikia soka letu lisiloweza kuchanua kila siku ya Mungu, ukizingatia kuwa hatuna mipango imara ya kuweza kusonga mbele.

Tuzinduke sasa na kugundua makosa yetu ili iwe njia ya kuelekea kwenye kilele cha mafanikio.
Hii siwezi kuvumilia na tukutane wiki ijayo.
+255 712053949

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...