Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UHAMIAJI haramu ni ile hali ya mtu wa Taifa lingine kuingia kwenye
nchi nyingine bila kufuata sheria. Kwa mfano, raia wa Rwanda kuingia Tanzania
kienyeji.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.
Hafuati utaratibu uliowekwa na nchi huru yenye mamlaka zake. Huyo
anavunja sheria, hivyo kwa ujio wake huo, anaweza kufanya vyovyote anavyotaka.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bernard Membe.
Hali hii ya uhamiaji haramu si ngeni duniani. Kumekuwa na
mwingiliano na sababu nyingi zinazowafanya watu watamani kuingia katika nchi
nyingine bila kupiga hodi.
Kila siku wanasikika waliokamatwa baada ya jaribio lao la kuzamia
kushindwa. Wapo wanaorudishwa makwao bila kupenda na wale pia wanaowekwa
kizuizini.
Wakati tunaangalia jambo hilo, lazima tukubali kuwa sheria zetu,
utendaji kazi wetu umewapa urahisi watu wengi kuingia Tanzania soni.
Wahamiaji haramu wanaingia na kuweka makazi bila hata kuonwa na
kuendelea na maisha yao. Na wale wanaonekana, wakati mwingine hawafikishwi
popote, hasa kama watafanikiwa kutoa chochote kitu kwa watu wa uhamiaji au hata
polisi.
Akiwa mkoani Kagera katika ziara yake ya kikazi, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, aliwatangazia vita wahamiaji
haramu.
Aliwataka wote walioingia Tanzania bila kufuata sheria wabebe
kilichokuwa chao na kurudi kwenye nchi zao. Akaonyesha ukali zaidi kwa kuwapa
siku 14 kabla ya kuingia kwenye oparesheni ya kuwarudisha makwao.
“Nilitoa maagizo kwa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama yaani
JWTZ, Polisi, Usalama wa Taifa na Uhamiaji watengeneze mpango kabambe wa
kuyashughulikia matatizo hayo.
Watayarishe na kutekeleza operesheni maalum itakayo au
zitakazokomesha ujambazi, kuondoa wahamiaji wasiokuwa halali na kuondoa mifugo iliyoingizwa
nchini kinyume na utaratibu na ile iliyoko kwenye maeneo yasiyo stahili,” Rais
Kikwete aliyasema haya pia katika Hotuba yake ya kila mwezi.
Pamoja na kusema hayo, lazima watu tufahamu kuwa kasi inayapoonekana
mikoani ya wahamiaji haramu, ni zaidi katika majiji makubwa, hasa Dar es
Salaam.
Dar es Salaam ndio jiji pekee linaloweza kuwaficha wahalifu,
wahamiaji haramu bila kuonekana. Ni rahisi kuona mtu anaendelea na biashara
zake maeneo mbalimbali bila kuwa na kibali cha kuishi na ambaye pia hajafuata
taratibu za kuingia.
Ni tofauti na Mataifa mengine. Nchini Botswana, wameweka sheriaa
kali mno ya wahamiaji haramu. Hata wale waliofanikiwa kuwa na kibali cha kuishi
huko wanapata shughuli pevu.
Kwa mfano Mtanzania anayeishi nchini humo, anaposhindwa kufahamu
mwisho wa kibali cha kuishi humo, ni sababu yake ya kurudi kwao hata kama
hataki.
Hata atakapojisalimisha katika ofisi za uhamiaji, hatapata
ushirikiano wowote zaidi ya kurudi anapotoka. Ndio hapo anapotoka kwanza nje ya
mipaka ya nchi hiyo na kurudi tena kama mgeni, ambapo hapo atapewa siku kadhaa
za kuishi.
Haya ni tofauti na Tanzania. Nchi ya ukarimu na kitu kidogo. Ndio
maana maeneo mengi hasa Dar es Salaam yanakumbwa na ongezeko la wahamiaji
haramu.
Maeneo ya Kinondoni Shamba na mengine yote yana idadi kubwa ya
watu wasiokuwa raia wa Tanzania na ambao hawajafuata sheria. Huko utakutana na
watu wa Malawi wakiishi bila wasiwasi wowote.
Na inapotokea mjumbe au mwenyekiti anajua mtaa wake una wahamiaji
wasiokuwa na kibali cha kuishi, basi amepata uhakika wa kupata hela ya sukari
siku anapoamka mweupe.
Anachofanya ni kujichukulia visenti kutoka kwa watu hao na
kushindwa walau kuwashauri wafuate taratibu za kuishi nchini. Hili ni jambo la
kushangaza mno.
Rais Kikwete ameyasema hayo bila kujua kuwa maagizo yake mengi
yanaishia njiani. Ni zima moto. Hakuna mipango kabambe, hivyo matamko yake
kuishia kudharauliwa.
Siku 14 alizotoa kamwe haziwezi kuwa na faida. Zaidi zimeripotiwa
kuchochea uhasama kwa wale wanaoshi sehemu mbalimbali za Tanzania, hasa
vijijini, ambapo imeripotiwa baadhi ya watu hao kuingiza mifugo kwenye mashamba
ya Watanzania, kama ishara ya kukerwa na kauli ya Kikwete.
Muleba suala hili ni kama mkuki kwao. Kwa kupitia Mbunge wao wa
Muleba Kaskazini, Charles Mwijage, alizungumza kwa machungu pale aliposikia
malalamiko ya wapiga kura wake kutokana na wafugaji kutoka nchini Rwanda
kuingiza mifugo yao kwenye mashamba yao Watanzania.
Tamko la Mheshimiwa Kikwete lilielemea sana kwa Mikoa ya Kigoma,
Kagera na Geita, huku majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Tanga
yakiachwa.
Mkoa wa Tanga nao una idadi kubwa ya wahamiaji haramu wanaotoka
kwenye nchi zao na kuweka makazi ya kudumu au wanaofanya njia ya kuelekea
kwingine wanapohitaji.
Mapema mwaka huu, maafisa wa uhamiaji wa Tanzania mkoani Tanga
waliwakamata wahamiaji haramu 227 katika kipindi cha Januari hadi Novemba 2012.
Idadi kubwa ya wahamiaji hao walikuwa ni Waethiopia, lakini baadhi
walitokea nchi nyengine kama vile Pakistan, Bangladesh, Denmark, Zambia, China,
Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Guinea, Switzerland, Sri Lanka,
Uturuki, Msumbiji na Italia
Hivyo kauli japo kauli ya Rais Kikwete ni njema, iliyosababishwa
na raia wa Tanzania kukosa uhuru na usalama wa kutembea anavyotaka, ila juhudi
sielekezwe nchi nzima.
Ingawa si dhambi raia wa Kenya, Uganda, Msumbiji, Malawi, Zambia,
Congo na wengineo kuja kuishi Tanzania, ila muhimu ni kufuata sheria
zilizowekwa.
Na inapotokea mtu ameweza kuja kuishi Tanzania, isiwe sababu ya
kujifanya wapo juu ya sheria na kuanza kuwaletea kasumba zisizokuwa na maana
kwa wenye nchi yao.
Mwaka 1982, Rais wa awamu ya kwanza, hayati Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere aliweza kuwaruhusu wakimbizi wanaopenda kuwa raia wa
Tanzania.
Historia inaonyesha kuwa jumla ya wakimbizi 30,000 waliweza
kutumia fursa hiyo, wakati mwaka mwaka 2010 wakimbizi 160,000 wa kutoka
nchini Burundi nao walikuwa raia wa Tanzania.
Serikali iwabane zaidi watendaji wake na pia juhudi za kukomesha
uhamiaji haramu usibaki mikoa ya Kagera kama alivyotangaza rais Kikwete, maana
janga hilo lipo pia jijini Dar es Salaam.
Tusipokuwa makini, tunaweza kudhibiti uingiaji wa wahamiaji haramu
mikoa inayopakana na nchi jirani, lakini idadi kama hiyo kutokomea kwenye
majiji yenye mwingiliano mkubwa.
Kama mtu anaweza kuishi Dar es Salaam bila kufanywa chochote,
tamko la kudhibiti suala hilo lina mhusu nini? Kama leo hii mtu mwenye asili ya
China anaweza kuja na kuishi kama wanavyoishi wengine, kwanini aishi kwa
presha?
Sitaki kuamini kama watu wote wanaoishi jiji la Dar es Salaam ni
raia au wanaishi kwa kufuata sheria. Wakati wao wakiishi bila presha, lakini
kwao wao Mtanzania hawezi kuishi kwa raha kama atakuwa ameingia kienyeji kama
nzi wa chooni.
Leo hii Mtanzania hawezi kuishi China ovyo ovyo bila kuwa na
shughuli ya uhakika, ila wao wameweka makazi. Tena wengine wanafanya kazi
inayostahili kufanywa na Mtanzania.
Ndio hapo utakapowakuta wamesheheni katika miradi mingi ya
kimaendeleo, hasa ujengwaji wa barabara, ambapo nao wanashika chepe au
kuwasimamia Watanzania.
Na kama huo uhalifu utakwisha sehemu ya mikoani na kuhamia jijini
Dar es Salaam, hatauoni kama tunapoteza muda bure? Naheshimu utendaji kazi wa
Rais Kikwete ila mara nyingi anaangushwa na washauri wake. Wale wanaovunja
sheria kwa sababu ya kuneemesha matumbo yao.
Wale wanaojua fika kuwa operesheni za kudhibiti wahamiaji haramu
zina maanufaa kwao kwasababu waya Kagera, tumie Aidha, niliwataka Maafisa wa
Uhamiaji watimize ipasavyo wajibu wao.
Ukweli ni kwamba, mambo haya kuendelea kwa muda mrefu kiasi hiki
ni kwa sababu ya udhaifu wa mamlaka husika.
kambimbwana@yahoo.com
kambimbwana@yahoo.com
+255712053949
No comments:
Post a Comment