Na Kambi Mbwana,
Handeni
JESHI la Polisi
wilayani Handeni, mkoani Tanga, limesema wilaya hiyo kwa sasa inakabiriwa na
changamoto ya matumizi ya bange na gongo, hivyo wanajipanga vilivyo kulidhibiti
suala hilo.
OCD wilayani Handeni, mkoani Tanga, Zuberi Chembera, akizungumza jambo na Handeni Kwetu Blog wilayani hapa.
Hayo yalisemwa na
Mkuu wa jeshi la Polisi wilayani humo, OCD Zuberi Chembera, alipotakiwa na
Handeni Kwetu Blog aelezee hali ya uhalifu katika maeneo yote ya Handeni.
OCD Chembera alisema
hali ya uhalifu kwa sasa wilayani humo imepungua kwa kasi na kubakia suala la
gongo na bange.
Alisema kutokana na
suala hilo, ofisi yake inajipanga imara kuhakikisha kuwa linaondoa kabisa hali
hiyo kwa ajili ya kuifanya wilaya hiyo ya aina yake katika mkoa wa Tanga.
“Hakuna matukio
makubwa ya uhalifu kwa wilaya hii kutokana na utendaji wa jeshi la Polisi
wilayani na Taifa kwa ujumla, hivyo hili tunajivunia na kuwashukuru wananchi.
“Hata hivyo, jukumu
letu tuliokuwa nalo ni kudhibiti pia matumizi ya bange na gongo kwasababu hayo
ndiyo kero kubwa na lazima tujipange kwa ajili ya kulitokomeza suala hilo,” alisema.
Kwa mujibu wa OCD
Chembera, vijana wake wamejipanga imara na kugawana vyema majukumu ya
kiutendaji hali inayopunguza matukio ya uhalifu wilayani hapa.
No comments:
Post a Comment