https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Sunday, September 01, 2013

Simba kuwatambulisha nyota watatu wapya kesho, akiwamo Henry Joseph



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KLABU ya Simba inayodhaminiwa na Bia ya KILIMANJARO inapenda kutoa taarifa ifuatayo kwa vyombo vya habari ili hatimaye taarifa hii iwafikie wapenzi na washabiki wake popote pale walipo.
Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga
Mara baada ya safari ya mikoa ya Tabora na Arusha kwenye mechi mbili za awali za Ligi Kuu ya Tanzania, timu ya Simba imerejea salama jijini Dar es Salaam ikiwa na kikosi chake kamili tayari kujiandaa na mechi ijayo ya ligi dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro iliyopangwa kuchezwa Septemba 14 mwaka huu.
 
Kama sehemu ya maandalizi ya mechi hiyo, kikosi cha Simba kitashuka dimbani katika Uwanja Mkuu wa Taifa siku ya kesho, Jumatatu Septemba 2, kucheza na Mafunzo ya Zanzibar katika mechi ambayo ina faida nyingine zaidi ya kuwa ya kujiandaa na mechi ya Mtibwa.

Mosi, mechi hiyo itatoa nafasi kwa wapenzi na wanachama wa Simba, pamoja na washabiki wa soka kwa ujumla wake, kupata fursa ya kuwaona kwa mara ya kwanza wachezaji wapya watatu wa klabu ambao hawajawahi kuonekana wakicheza jijini Dar es Salaam.
 
Wachezaji hao ni Henry Joseph Shindika aliyetoka Kongsvinger ya Norway, Gilbert Kaze na Amissi Tambwe waliotoka katika klabu ya Vital’o ya Burundi. Ingawa hawa ni wachezaji wa Simba lakini hawakutambulishwa katika Tamasha la Simba Day kama ilivyo ada kwa wachezaji wote wapya.
Mechi ya Mafunzo itatoa fursa hiyo ya kutambulishwa na kuonekana wakiitumikia klabu kwa mara ya kwanza jijini hapa.
 
Pili, mechi hiyo itatumika na klabu kwa ajili ya mchezaji wake, Kiggi Makassi, ambaye atawaaga washabiki rasmi kwa ajili ya safari yake ya kwenda nchini India anakokwenda kwa matibabu ya goti lake. Kiggi anatarajiwa kuondoka jijini Septemba tisa mwaka huu.
 
Kwa vile Septemba 2 inaangukia siku ya kazi, waandaaji wa pambano hilo wamepanga ianze saa 11 jioni ili kutoa nafasi kwa wapenzi wengi zaidi kuhudhuria pambano hilo.
 
VIINGILIO
 
KATIKA pambano hilo viingilio vitakuwa ni Sh 20,000 kwa VIP A, Sh 10,000 kwa VIP B, Sh 8,000 kwa VIP C na Sh 5,000 kwa mzunguko.
Maandalizi yote kwa ajili ya mechi yamekamilika na timu zote tayari ziko jijini Dar es Salaam.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...