SIWEZI KUVUMILIA: Yanga ijiandae kushindwa na kushinda
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KATIKA mchezo wa soka, suala la kushinda,
kutoka sare na kushindwa ni jambo la kawaida, hivyo klabu za soka Tanzania,
ikiwamo Yanga, Simba lazima zijiandae kwa matokeo hayo.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, pichani.
Si ajabu timu kufungwa au
kushinda. Lolote linaweza kutokea maana ni jambo la kawaida kwenye mchezo wa
soka. Wakati nasema haya, nagundua jinsi baadhi ya timu zinaposhindwa kukubali
matokeo ya kufungwa au kutoka sare ndani ya uwanja.
Huwa naumia kichwa ninapoona timu
moja inashindwa kukubali matokeo ya kufungwa au kutoka sare. Siku zote wanataka
washinde. Inapofungwa au kupata sare inalalamika mno.
Hili si jambo jema. Na ndio maana
siwezi kuvumilia, hasa kwa kuanza kusikia malalamiko kutoka kwa baadhi ya
mashabiki wa soka Tanzania, hasa wale wa Yanga.
Mara baada ya kupata sare ya bao
1-1 dhidi ya timu ya Mbeya City, mkoani Mbeya, Yanga walitangaza nia ya kukata
rufaa wakipinga matokeo ya mchezo huo wa ligi.
Yanga walifanya hayo kama vile
walijiandaa zaidi kushinda na sio sare au kufungwa, ukizingatia kuwa ni jambo
la kawaida katika mpira wa miguu duniani kote.
Na sio Yanga tu, ila hata Simba
mara kwa mara imekuwa ikiingia kwenye wasiwasi wa aina yake kutokana na
mashabiki wake au viongozi kukaa chini na kusubiria ushindi.
Hii sio haki hata kidogo. Katika
mchezo wa soka, hata viongozi au mashabiki lazima waelewe kuwa lolote
linawezekana. Kama wao wanataka washinde, hata wenzao nao wanataka ushindi.
Hakuna timu inayoingia uwanjani
huku ikitaka ifungwe. Inapotokea tofauti, basi huwa matokeo ya kawaida ndani ya
uwanja, hivyo kwa timu zetu lazima zijiandae.
Ili timu iweze kushinda uwanja
lazima ijipange. Ijipange kwasababu kila timu inahitaji ushindi. Huu ni wakati
wa timu hizo kujitambua kwa ajili ya kukuza soka letu.
Inauma sana Yanga kulalamikia
matokeo ya Mbeya City kama vile wameonewa na walistahili kushinda. Kwanini?
Kwani Mbeya City nao si timu ya kushinda mbele za wengine.
Au hawa Mbeya City wamekuja
kwenye ligi kushiriki na kusindikiza wengine ndani ya uwanja? Yanga, Simba na
timu nyingine zote zinapaswa kuwa makini na kucheza soka lao la uhakika.
Inapotokea inafungwa au kutoka
sare haipaswi kuanza kutafuta mchawi maana katika mpira wa miguu lolote
linawezekana. Huu ndio ukweli wa mambo na lazima tuukubali.
Japo tunazipenda sana timu zetu,
ila si wakati muafaka wa kuleta chokochoko inapopata matokeo mabaya. Hakuna
sababu ya kulia na kutoa lawama.
Ndio inawezekana kabisa mwamuzi
akawa ameibana timu, ila tusilione jambo hilo kwasababu tumefungwa au tumepata sare.
Japo wapo watu wanaodharau timu zilizopanda daraja, lakini nazo zinautaka
ushindi na ndio kilichowaleta kwenye ligi Kuu.
Nafikiri Yanga na timu nyingine
zote zinapaswa kuwa makini katika kucheza soka lao la ushindani na sio kuanza
kutoa lawama kwasababu wamefungwa au wametoka sare.
Huu ndio ukweli wa mambo, hivyo
siwezi kuvumilia kuona baadhi ya timu zinajiandaa zaidi kushinda na inapotokea
tofauti kunaibuliwa mkanganyiko usiokuwa na kichwa wala miguu.
Tubadilike kwa ajili ya kuokoa
soka letu. Tunahitaji soka la ushindani ndani ya uwanja. Katika hilo, kila timu
icheze soka lake ili ipate matokeo mazuri ndani ya uwanja.
Na inapotokea tofauti basi
mkubali matokeo na mjipange kwa mechi zijazo, maana ni dhahiri kufungwa,
kushinda na kutoka sare ni jambo la kawaida katika ligi yoyote duniani.
No comments:
Post a Comment