https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543

Recent Post

Monday, September 09, 2013

Miaka miwili kifo cha Kasaloo Kyanga, sauti yake itabaki kuwa luluNa Mohsini Juma, Dar es Salaam
ZILKUWA ni taarifa za kushitusha kwa wadau wa muziki wa dansi tarehe kama ya LEO Septemba 9, 2011 majira ya alfajiri mara ilipotangazwa kuwa mwanamuziki nguli wa muziki huo mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zamani Zaire, Muganza Katanga Kasaloo Kyanga amefariki.
Kasaloo Kyanga, pichani
Kifo cha mwanamuziki huyo ambaye sasa ametimiza miaka miwili tangu umauti umkute akiwa ametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya muziki  wa dansi nchini kutokana na ubora wa tunzi zake na sauti nzuri kilishitua wadau wengi kutokana na kutokuwepo kwa taarifa za kuumwa kwake.

Kasaloo ambaye ni pacha wa mwanamuziki mwingine ambaye alishatangulia mbele ya haki Kyanga Songa alifariki Septemba 9, 2011 katika Hospitali ya Mwananyamala Kinondoni Jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa mapafu kujaa maji ambapo alizikwa kesho yake katika Makaburi ya Sinza mazishi yalihudhuriwa na mamia ya wadau wa muziki nchini.

Swali ni je baada ya Kasaloo kufa nini kinafanyika kumuenzi au kusaidia familia yake ambayo bado imepiga kambi nchini, lakini pia kwa kuacha kuwaenzi wanamuziki tunautendea haki muziki wa dansi ambao ulifanya

kazi kubwa katika harakati mbalimbali za maendeleo Tanzania ilizopitia.
Mwanamuziki huyo aliingia nchini mwanzoni mwa miaka ya 1980 akiletwa nchini na aliyekuwa Mkurugenzi wa

Super Matimila Mzee Kavula na kujiunga na bendi hiyo akiwa na Skasy Kasambula ambapo alishiriki na Matimila kwa mafanikio makubwa.

Miongoni mwa wanamuziki aliokuwa nao Matimila ni Abuu Semhando ‘Abuu Lokasa’, Kyanga Songa, Ramadhani Mtoro Ongala Dk. Remy, Hamza Kalala Issa Nundu na mpiga solo mahiri Moses Fan Fan ambapo waliipaisha bendi katika medani ya muziki huo  nchini.

Akiwa na Matimila mwanamuziki Kasaloo aliweza kuonyesha umahiri wake wa kuimba na kurembesha sauti uliokuwa ukiwasisimua mashabiki na wapenzi wa muziki wa dansi katika nyimbo kama ‘Mwanaidi’ akishirikiana vyema na gwiji mwingine Issa Nundu na kujikuta akiipa mafanikio bendi hiyo na kujizolea umaarufu.

Alitamba na Matimila iliyokuwa ikitumia mtindo wa ‘Talakaka’ kwa muda kabla ya baadae kuitosa bendi hiyo ambapo alijiondoa kwa kuambatana na Skasy Kasambula, Abuu Semhando, Kyanga Songa, Hamza Kalala na kwenda kuiasisi bendi ya Orchestra Tomatoma iliyokuwa ikimilikiwa na mfanyabiashara  Timmy Thomas.

Alitamba na bendi hiyo kwa miaka miwili ambapo alishiriki katika nyimbo mbalimbali na miongoni mwa nyimbo zilizompatia umaarufu ni ‘Bishada’ kabla ya kuitosa na kutokomea jijini Nairobi akiwa na Kasambula, 

Semhando ambapo walikuwa wakifanya shughuli za muziki  kwa miaka kadhaa na kurejea nchini ambako alinyakuliwa na Marquis Original.

Kasaloo ambaye  ameacha mke na watoto sita alitamba na Marquis Original katika nyimbo mbalimbali akiwa na waimbaji kama kama Tshimanga Kalala Assosa, Mutombo Odax, Kasongo Mpinda ‘Clyton’ Kikumbi Mwanza Mpango, Mbuya Makonga ‘Adios’ Issa Nundu.

Wapiga vyombo wakiwa Nguza Mbangu Viking, (Solo) (Banza Mchafu, (besi) Ilunga Ilunga Said (Rythm) Mafumu Bilal Bobembega (Saxaphone) ambapo alifanikiwa kutunga wimbo wa ‘Kalubandika’  ambao umeendelea kuliweka jina lake kwenye ramani ya muziki huo nchini hadi leo.

Nyota ilizidi kung’ara zaidi katika wimbo wa ‘Clara’ ambao anamzungumzia mwanamke ambaye alikuwa na matarajio ya kuwa mke wake lakini baadae akaja kumgeuka ambapo aliimba kwa sauti ya masikitiko huku akitupiana sauti na Issa Nundu kitu ambacho kiliunogesha wimbo huo ambao ukipigwa hadi leo bado umebeba ladha na ubora uleule.

Kama ilivyo kawaida ya wanamuziki kuhahama katikati ya miaka 1980 alijitoa Marquis Original ma kujiunga na bendi ya Kampuni ya kukata madini ya Almasi ya Mkoani Iringa na na kushiriki kuiasisi bendi ya Tuncut Almasi

akiwa na wanamuziki Kawele Mutimona, John Kitime, Kibambe Ramadhani, Kalala Mbwembwe,Mafumu Bilali,Jery Mfaume Andul Salvador ‘Father Kidevu’ Hashim Kasongo, Zacharia ambapo ha[po nako hakufanya ajizi katika nyimbo kama ‘Masafa Marefu’ ‘Nimemkaribisha Nyoka’ na Jane Butinini’ ‘Kashasha’  ambao ulikuwa ni jina mke wake akiwa dada wa mchezaji mpira wa zamani wa Reli ya Morogoro Duncun Butinini.

Alitamba na bendi hiyo hadi miaka 1990 kabla ya kufanya uamuzi wa kutokomea jijini Nairobi Kenya kuendelea na shughuli za muziki ambako alikaa kwa miaka zaidi ya 20 kabla ya kurejea nchini akiendelea na shughuli za muziki lakini akakumbwa na maradhi yaliyochukua uhai wake.

Kwa wasiojua Kasaloo ndiye aliyemtunga jina mpiga dramu wa zamani wa bendi ya Vijana Jazz Orchestra na African Stars 'Twanga Pepeta' marehemu Abuu Semhando akamwita ‘Lokasa’ akimaanisha anapiga vizuri dramu hadi zinanoga akifananisha na mafuta ya mawese ambayo hutokana na mbegu za mchikichiki.

‘Kila nafsi itaonja Umauti’, ‘Bwana Ametoa na bwana ametwaa’  na ‘Jina la bwana Lihimidie’
+255 754-629298

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...