Na Mwandishi Wetu, Handeni
MENEJA Utafiti wa Kampuni ya CANACO
inayojishughulisha na mambo ya madini wilayani Handeni, mkoani Tanga, Bavon
Mwaluko, amesema kwamba wanakusudia kuleta ajira kwa wananchi na wakazi wa eneo
lote la Magambazi, mara baada ya serikali kuruhusu kuendelea na shughuli hiyo.
Mkuu wa wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu
Serikali ilizuia kwa muda shughuli za uchimbaji
na utafiti wa madini katika eneo hilo mapema mwaka huu kwa ajili ya kuangalia
kwa kina mchakato mzima wa kazi hizo.
Akizungumza hivi karibuni wilayani Handeni,
Mwaluko alisema shughuli za uchimbaji wa madini zinahitaji nguvu kazi, hivyo
endapo wataanza kazi hiyo wanananchi watanufaika.
“Tuliingia katika eneo la Magambazi mwaka 2007
kwa ajili ya kuendesha shughuli za utafiti wa madini yaliyoko kama hatua za
awali kabla ya kuanza kazi ya ujenzi wa mashine kwa ajili ya uchimbaji.
“Tulikubaliana na wenyeji waliokuwa wakimiliki
maeneo hayo ambao walikuwa wanaendesha shughuli za uchimbaji mdogo na tulitumia
fedha nyingi kuwalipa fidia hivyo kwa sasa tunachosubiri ni ruhusa ya serikali
ili tuanze kazi ya uchimbaji na hakika tutaweza kuajiri watu wengi katika
kuendeleza mradi huo,” alisema Mwaluko.
Kwa mujibu wa Mwaluko, kabla ya kuanza zoezi la
uchimbaj ni lazima kufanya tafiti ili kujua tabia za miamba ukizingatia mingine
inaweza kuwa na milipuko au ni sehemu ya chanzo cha maji na kuchangia uharibifu
wa mazingira.
No comments:
Post a Comment