Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
BONDIA wa ngumi za
kulipwa hapa nchini, Japhet Kaseba, amesema kuwa maisha yamekuwa magumu kwa
wanamichezo, hivyo hatari inaweza kuwa kubwa kutokana na vijana hao kujiingiza
kwenye dawa za kulevya.
Kaseba ameyasema hayo
siku chache baada ya madai ya kukamatwa kwa wanamichezo Mkwanda Matumla na
Joseph Kaniki, aliyewahi kuwa nyota wa kandanda katika klabu ya soka ya Simba.
Akizungumza leo mchana
jijini Dar es Salaam, Kaseba alisema kuwa kutokana na kusumbuliwa na ukata,
baadhi yao wanajiingiza katika masuala hayo ya dawa za kulevya.
Alisema serikali
inapaswa kuwa makini zaidi katika suala hilo, ikiwa ni pamoja na kusimamia
vyema sera ya michezo ni ajira ili kuboresha kipato cha wanamichezo.
“Kijana anaona hana
cha kujivunia kutokana na ukata, hivyo wasiwasi wangu wengi wao wanaweza
kujiingiza kwenye suala la dawa za kulevya na kuathiri nguvu kazi ya Taifa.
“Kwangu mimi
nitaendelea kulia juu ya njaa za wanamichezo na lazima juhudi za ziada
zifanyike ili kuokoa vijana wetu ambao wamekuwa na vipaji vya aina yake,”
alisema Kaseba.
Sakata la kukamatwa
na dawa za kulevya kwa Tanzania limezidi kugonga hisia za wengi, huku kila
baada ya wiki moja kutokea tukio jipya la Mtanzania kunaswa na ubebaji wa dawa
za kulevya na kulitia aibu Taifa.
No comments:
Post a Comment