Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
HALI ya hatari imeanza
kuonekana baada ya kigogo mmoja serikali kutoka jiji la Dar es Salaam
kupendekeza Viwanja vya Leaders Club kuachwa kutumiwa katika masuala ya
kiburudani kwa madai kuwa yanabugudhi watu wanaoishi kwenye maeneo hayo.
Hawa ni baadhi ya wadau wakijadiliana mambo baada ya kufikishiwa habari za kusimamisha bonanza la michezo lililofanyika juzi katika viwanja vya Leaders Club, Kinondoni.
Sakata hili limejitokeza katika
siku za hivi karibuni, baada ya kutokea mvutano kwa baadhi ya wadau wa burudani
na Ofisi ya Utamaduni Kinondoni, kuvamia katika viwanja hivyo na kuzuia mambo
yanayofanyika hapo mara kwa mara.
Kwa wasiofika Leaders Club,
viwanja hivyo hutumika zaidi katika siku za Jumapili, ambapo bendi ya Twanga
Pepeta hufanya shoo ya mwisho wa wiki,
katika bonanza lake, wakati pia bendi za Msondo Ngoma na kujumuisha pia matukio
mbalimbali.
Aidha, Kampuni ya Prime Time
Promotion ya jijini Dar es Salaam sambamba na Clouds Media Group inafanya shoo
ya kila mwaka ya Fiesta inayofanyika pia katika viwanja hivyo.
Juzi, Clouds waliandaa bonanza
la michezo lililojumuisha pia Kampuni mbalimbali na wafanyakazi wao kuonyesha
uwezo wao.
Habari kutoka ndani ya Ofisi ya
Utamaduni Kinondoni zinasema kuwa kuna kigogo mmoja anayeishi katika maeneo
hayo, hivyo amepiga marufuku kwasababu hataki kelele.
“Suala la Leaders Club lazima
liende na mtu, maana bosi hataki kufanyike shughuli yoyote inayohusu mziki
katika eneo hili, wakati anajua fika Kinondoni hakuna viwanja vya wazi.
“Kwakweli naogopa, hivyo
tunapofuatilia suala hili lazima ijulikane kuwa sisi ni watu wadogo na maagizo
kama haya hutolewa na watu wazito na kuibua mgogoro mkubwa,” alisema mpashaji
huyo ambaye naye anatoka katika ofisi za serikali.
Viwanja vya Leaders Club ni sehemu pekee tulivu ambavyo vinaweza kukusanya watu wengi katika matukio mbalimbali na kujadiliana mambo ya kimaisha, yakiwamo yale ya kiburudani.
No comments:
Post a Comment