Rais wa TFF, Leodgra Tenga.
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema
hakuna hila yoyote katika nia ya kutaka marekebisho matatu kwenye katiba
kabla ya uchaguzi na kuwataka wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kuridhia
mabadiliko hayo kwa maslahi ya maendeleo ya mchezo huo.
Tenga
alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kufafanua
juu ya waraka wa kuomba ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF
kuridhia mapendekezo matatu ya mabadiliko ya katiba yanayohusu uingizaji
wa kipengele cha utoaji leseni kwa klabu (Club Licensing); kuundwa kwa
Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi wa TFF na kuondoa nafasi ya Makamu wa Pili
wa Rais wa TFF.
Hatua
ya kutuma waraka wa kuomba ridhaa ya mabadiliko hayo imetafsiriwa
tofauti na baadhi ya wadau, wengine wakisema ni mbinu za uongozi wa sasa
kutaka uendelee kukaa madarakani wakati wengine wakitaka ufafanuzi wa
vipengele hivyo.
“Hakuna
hila hata kidogo. Yote ni mambo ya maendeleo na nia yetu ni kufanikisha
ili mambo yaendelee,” alisema Rais Tenga kwenye ukumbi wa mikutano wa
TFF.
“Tusifikie
sehemu tukaanza kulaumu kwa nini mtu ametaka maelezo. Lakini
sikutarajia kuwa mtu wa mpira akiambiwa hili ni agizo la FIFA
(Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu), atasita; akiambiwa hili ni
agizo la CAF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika), atasita, au
akaambiwa huu ni uamuzi wenu wenyewe, akasita.”
Tenga
alisema nia ya Kamati ya Utendaji ya TFF ilikuwa ni kuitisha Mkutano
Mkuu kwa ajili ya mabadiliko hayo ya katiba, lakini akasema
baada
ya kutafakari kwa kina na kuangaliwa uwezo wa Shirikisho, Kamati iliona
haiwezi kuitisha mikutano miwili kwa sasa kwa kuwa TFF haina fedha.
“Tumetoa
maelezo kuwa tunafahamu kuwa katika mazingira ya kawaida tungeitisha
mkutano mkuu; tuje tuzungumze na baadaye siku ya pili watu waondoke
halafu tuwaite tena kwa ajili ya mkutano wa uchaguzi,” alisema Tenga
ambaye alibainisha kuwa gharama za chini za mkutano mkuu wa TFF ni kati
ya sh. milioni 90 na sh. milioni 110.
“Lakini
tumeeleza bayana kuwa uwezo huo hatuna, tungelikuwa nao wala
tusingefika mahali hapa; vijana wetu wanahangaika hadi tunatafuta watu
watusaidie. Kwa hiyo tukasema kuna dhambi gani kuwa wakweli. Katiba
inasema mkitaka kufanya mabadiliko ya katiba, itisheni mkutano mkuu.
Unaita Mkutano Mkuu kwa sababu gani, ili mlete wajumbe wa mkutano mkuu
ambao ndio watakaopitisha mabadiliko hayo na ndio maana tumeona dhana
hiyo ya kutuma waraka.”
Kuhusu
mabadiliko hayo, Tenga alifafanua kuwa maagizo kuhusu utoaji leseni kwa
klabu (Club Licensing) na kuundwa kwa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa
TFF yalitolewa mwishoni Julai, ikiwa ni baada ya kikao cha Kamati ya
Utendaji cha Julai na hivyo suala hilo kulazimika kuzungumzwa kwenye
kikao cha Septemba.
Alisema:
”Pamoja na kwamba Tanzania ilishaingiza kwenye kanuni za ligi masharti
ya utoaji leseni, CAF imekuja na maagizo kwamba ni lazima itamkwe kwenye
katiba kuwa TFF itatoa leseni kwa klabu kwa mujibu wa maagizo ya CAF na
msipofanya hivyo klabu zenu hazitaruhusiwa kushiriki mashindano ya
klabu ya Afrika mwakani,”
Simba
na Azam FC zitaiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Klabu Bingwa ya
Afrika na Kombe la Shirikisho, hivyo kutopitishwa kwa mabadiliko hayo
mapema kutasababisha wawakilishi wa Tanzania wazuiwe kushiriki michuano
hiyo.
Kuhusu
kuundwa kwa Kamati ya Rufani, Tenga alisema baada ya kuomba ufafanuzi
wa utata uliojitokeza katika vyombo vya maamuzi vya TFF, FIFA ilisema
ili kuondoa mgongano wa kimaslahi, ni muhimu ikaundwa Kamati ya Rufani
ya Uchaguzi wa TFF badala ya mfumo wa sasa ambao Kamati ya Rufani
hujigeuza kuwa Kamati ya Rufani za Uchaguzi inapofikia wakati wa
uchaguzi mkuu wa TFF.
“Kwa
hiyo tunachoomba hapa ni ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kwamba iwepo
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF ili kama mtu hatatendewa haki na
Kamati ya Uchaguzi ya TFF, basi akate rufani kwenye Kamati ya Rufani ya
Uchaguzi badala ya chombo kimoja kushughulikia mambo mawili,” alisema
Tenga.
Kuhusu
kuondoa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais wa TFF, kiongozi huyo alisema
suala hilo lilitokana na uamuzi wa Mkutano Mkuu uliopita kuwa Ligi Kuu
na Ligi Daraja la Kwanza ziendeshwe na chombo huru.
“Baada
ya hapo Kamati ya Utendaji iliziambia klabu kuwa tunaunda Kanuni za
Kuendesha chombo huru cha ligi, tunaomba mapendekezo yenu. Na ndipo
walipotuletea mapendekezo yao kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi atoke
kwenye klabu sita za juu na kwamba kiwango cha chini cha elimu kiwe
Cheti cha Elimu ya Kidato cha Nne kama ilivyo kwenye katiba,” alisema.
“Maana
yake ni kwamba sifa hizo hazikidhi utashi wa kikatiba wa sifa za
mgombea wa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais wa TFF ambazo ni Elimu ya
Chuo Kikuu, lakini klabu zikasema hazina haja na nafasi ya Makamu wa
Pili wa Rais na ndio maana tunaomba ridhaa sasa ya kuondoa nafasi hiyo.”
“Napenda
kusema jambo hili ni la maendeleo na hakuna hata moja ambalo si la
maendeleo. Tumepata barua kutoka Kagera ikieleza kuwa utaratibu huu
haufai, Katibu Mkuu amepata na atawajibu. Pwani nao wameomba ufafanuzi
na tutatoa waraka wa ufafanuzi kwa wote.
“Watu
wana haki ya kuhoji na sisi ni wajibu wetu kuwaelimisha. Ombi langu ni
tushirikiane ili twende kwenye mkutano mkuu wetu unaokuja ili
tuchaguane. Tukichaguana tutakuwa tumetimiza jambo muhimu kweli kweli.”
Tenga
pia aliwasihi wajuimbe wa Kamati ya Utendaji kuendelea na jitihada za
kuelimisha wajumbe ili waridhie mabadiliko hayo na shughuli za maendeleo
ya mpira wa miguu ziendelee kama kawaida.
No comments:
Post a Comment