Siwezi Kuvumilia
Aden Rage, mwenyekiti wa Simba
Na Kambi Mbwana, Dar es
Salaam
JESHI la Polisi kwa kupitia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni,
Charles Kenyela, halijawatendea haki wanachama wa Simba, zaidi ya 698
waliopanga kufanya mkutano wao jana, Travertine Hoteli, Magomeni.
Jeshi hilo
ambalo kimsingi linatakiwa kutoa ulinzi kwa kila Mtanzania, lilijitetea kuwa
wameupinga mkutano huo kwa madai eti wanachama hao hawajafuata sheria na
taratibu.
Sawa, huenda wanachama hao walikosea, lakini kitendo cha kukaa kimya
hadi kutoa uamuzi siku moja kabla ya mkutano hakikubaliki.
Ni dhahiri Jeshi la Polisi limechukua uamuzi wa kuukataa mkutano huo,
kwasababu ya kupokea barua kutoka kwa uongozi wa Simba, walioomba mkutano huo
uzuiwe kwa sababu wanazojua wenyewe.
Hii sio haki na siwezi kuvumilia kuona baadhi ya watu wanafanya mambo
kama Taifa hili ni lao peke yao.
Kwanini nasema hivi? Jeshi la Polisi linapaswa kujua kwa mujibu wa Katiba ya
Simba, mkutano ule ulikuwa sahihi.
Wanachama hao waliitisha mkutano wao kwa kubebwa na Ibara ya 22,
kifungu cha pili cha Katiba yao,
ukizingatia kuwa tayari walishatoa taarifa za siku 30 za kutaka viongozi kwa
kupitia Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, iitishe mkutano wa wanachama wote.
Simba kwa kupitia mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage, walikataa hata kwa
kujibu kwa maandishi kama wao walivyotumiwa na
wanachama hao, badala yake walipita uchochoroni au kwenye vyombo vya habari na
kusema wanachama hao ni wahuni. Kweli wanachama hawa ni wahuni?
Ikumbukwe kuwa wanachama hawa wanaoitwa ni wahuni ndio walioshiriki
kwa namna moja ama nyingine, kumuweka madarakani Rage na viongozi wengine wa
Simba.
Lakini pamoja na huo uhuni wao, wanachama hawa katika kuandaa mkutano
wao walikuwa sahihi, wakitoa taarifa halali, hivyo polisi wao walipaswa kutoa
ulinzi tu na sio kuingia kwenye dhambi ya viongozi wa Simba.
Sina lengo la kuunga mkono kundi hilo
linalotaka mkutano wa Simba, lakini pia sio kawaida yangu ya kuchekea hata yale
mabaya yanayofanywa na waliokuwa madarakani.
Huwa sipendi kuchekea vitu ambavyo vinaongeza chuki kati ya viongozi
na jamii, ikiwamo jeshi la polisi ambalo kwa hakika limefanya uamuzi wa
kufurahisha watawala badala ya watawaliwa, ukizingatia kila mmoja ana haki sawa
kama Katiba ya nchi inavyoeleza.
Kenyela, aliamua kuupinga mkutano huo kwa kuusaidia uongozi wa Simba,
walioandika barua ya kuomba msaada Desemba 28, ikiandikwa na Katibu Mkuu,
Evodius Mtawala bila hata kupima kuangalia mchakato ulivyokuwa.
Kweli? Kenyela kumbuka upo kwenye nafasi ya kutumikia Watanzania wote
na sio viongozi wachache wa Simba, akiwamo Rage ambaye pia ni mbunge wa Tabora
Mjini.
Kama kweli ulikuwa na
nia ya kuukataa mkutano huo, basi usingesubiri hadi upelekewe barua na Simba.
Najiuliza, kama Simba wasingepeleka barua hiyo
ya kuomba msaada kwa jeshi la polisi, mkutano huo usingefanyika?
Kwa mtindo huu, tunaweza kuibua hisia hasi kutoka kwa viongozi wa
Simba na wanachama. Sakata kama hili lipo pia katika siasa.
Mara nyingi polisi wamekuwa wakitumia mbinu mbovu za kupambana na
vurugu. Njia hiyo si sahihi. Lazima Polisi kwa kupitia Kenyela wajuwe
wanachokifanya kipo kwa ajili ya watu wachache au la.
Kwa mujibu wa Katiba ya Simba, wanachama wanapofikia idadi ya watu 500
wanaweza kuitisha mkutano, kama wanataka kuijadili klabu yao.
Hili lilifuatwa. Rage na jopo lake hana
uwezo wa kupinga mkutano ule, maana uliandaliwa kwa kufuata sheria zote,
ikiwamo taarifa Makao Makuu.
Kama Rage angekuwa na utawala wa sheria na ushirikiano na wanachama
wake, angekuwa muungwana kwa kuwa miongoni mwa watakaohudhuria mkutano huo.
Lakini anakimbia kivuli, huku akijificha nyuma ya kofia za polisi,
akijua kuwa wataweza kufanyia kazi ujanja wake, nasema hivi kwakuwa namfahamu
vyema Rage.
Pamoja na kumfahamu Rage, pia naelewa kuwa wengi wasiomjua Rage
wanaweza kujikuta wanaingia katika lawama bure na kuleta mgogoro mkubwa zaidi.
Tuombe Mungu wanachama wa Simba wawe waelewa, lakini kama
sio hivyo, kuna siku balaa kubwa linaweza kujitokeza, hasa kwa kupewa vizingiti
kwasababu zenye matege.
Kenyela anasema, ‘Jeshi la Polisi haliwezi kufanya kazi kwa kupitia
nakala,’ mwisho wa kunukuu. Kama kweli,
kwanini kauli hiyo isitoke tangu mwanzo wa tarehe iliyopangwa hadi wasubirie
barua ya Simba?
Kenyela usiingie kwenye dhambi ya kutumikishwa na viongozi wa michezo
wasiokuwa na majibu sahihi kwa wanachama wao, na usijaribu kujiingiza kwenye
vurugu na askari wako, ulinzi shirikishi kwasababu ya mtu mmoja.
Kenyela uamuzi wako hauna nia ya kuzima moto zaidi ya kuuwasha,
wanachama waliozuiwa kufanya mkutano wao, wakati wamefuata taratibu zote
watashindwa kukubali matakwa ya mtu mmoja yawaendeshe.
Kinyume cha hapo, labda Kenyela uniambie kuwa sheria ya saa 48 ya
kupeleka barua rasmi jeshi la polisi, inaweza kutumika kama wanachama hao
watakuletea barua yao
leo jumatatu na wakikubaliwa wakutane Jumatano.
Wakati mwingine uamuzi wetu tunaochukua inabidi tutumie busara na
kuangalia matokeo yake, maana si sahihi kuuzima moto kwa kunyunyiza petroli juu
yake.
Rage habebeki, ndio maana anaona kuruhusu wanachama hao wafanye
mkutano wao kwa haki kama Katiba inavyosema,
anaweza kukalia kuti kavu.
Wasiwasi Kamanda Kenyela anajua janja hii? Siwezi Kuvumilia, ndio
maana nimeamua kuandika ukweli huu nikiamini kuwa, Kenyela ni mwelewa na
atakuwa makini zaidi siku nyingine kadhia kama
hii inapojirudia.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment