Bingwa wa Kick Boxing, Japhet
Kaseba akionyesha ubabe wake
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MWANAMASUMBWI mahiri hapa nchini,
Japhet Kaseba, amesema filamu zake mbili anazoandaa zinamuweka 'busy' kiasi cha
kumfanya ashindwe kufanya mazoezi makali ya mapigano hadi hapo zitakapoingia
sokoni.
Kaseba ambaye pia ni mahiri katika
upande wa ngumi za meteke, maarufu kama Kick
Boxing, anakamilisha filamu zake mbili ambazo ni Mafia na Dhambi ya Baba
zinazotarajiwa kuingia sokoni mapema mwakani.
Akizungumza na Handeni Kwetu leo
mchana, jijini Dar es Salaam,
Kaseba alisema katika filamu hizo amewashirikisha wasanii wengi wenye uwezo na
majina ya kutisha, akiwamo Kelvin, Mchumia Tumbo, Muhogo Mchungu na wengineo.
Alisema mara baada ya
kumaliza programu za filamu zake hizo ikiwamo za studio, ataingia tena
ulingoni, akianza na mazoezi kwa ajili ya kulinda jina na hadhi yake katika
kona ya ngumi Tanzania, kama anavyojulikana na kuogopwa na wengi.
“Filamu zinahitaji muda
katika utengenezaji wake, hivyo ndio maana nimetingwa kwa shughuli za kazi
zangu mbili ninazotarajia ziingie sokoni mapema mwakani, huku nikiamini kuwa
zitakuwa moto wa kuotea mbali.
“Naamini wadau wote wataona makali
yangu, hivyo mashabiki wasiogope kwa hatua hii kwakuwa zote ni kazi zangu na baada
ya kumaliza hatua hii nitaingia tena katika kujiwinda kwenye masumbwi kama kawaida yangu,” alisema Kaseba.
Kaseba ni miongoni mwa mabondia
wenye uwezo wa kutisha katika tasnia ya mchezo wa masumbwi kutokana na uwezo
wake wa kurusha ngumi huku pia akiwahi kuwa bingwa wa Dunia wa Kick Boxing.
No comments:
Post a Comment