Mwanamuziki Badi Bakule akiwa jukwaani
Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
MWANAMUZIKI mahiri wa muziki wa dansi wa The African Stars,
Twanga Pepeta, Badi Bakule, amedaiwa kutaka milioni saba ili aweze kujiunga na
bendi ya Victoria Sound ya Mwinjuma Muumini.
Hitaji la Bakule limejulikana muda mchache baada ya kutajwa
kutakiwa na uongozi wa Victoria Sound kwa ajili ya kuiboresha zaidi bendi hiyo
inayopigania umaarufu kwenye medani ya dansi nchini.
Habari kutoka kwa mtu wa karibu na bendi ya Victoria Sound
zilisema kuwa awali waliketi na Badi kuzungumzia ujio wake kwenye bendi hiyo,
lakini alitangaza dau lake la Milioni saba, kama
ada ya uhamisho wa kutoka Twanga Pepeta.
Ada
hiyo ilimshinda Muumini na kumuacha aendelee na maisha yake Twanga Pepeta,
ingawa sauti na uwezo wa mwanamuziki huyo inahitajika katika bendi hiyo
iliyoongezwa pia kwa mwimbaji mwenye sauti ya mvuto, Waziri Sonyo.
“Badi Bakule anataka fedha nyingi sana,
milioni saba ndio aweze kujiunga na bendi yetu, hivyo hatuwezi kukubaliana naye
zaidi ya kumuacha abaki kwenye bendi yake ya Twanga Pepeta, maana huwezi
kumlazimisha mtu,” alisema mdau huyo wa Victoria Sound.
Alipoulizwa Badi juu ya ada hiyo alisema, “sijafanya
mazungumzo yoyote na Muumini juu ya kutaka niende kwenye bendi hiyo, lakini
mimi kazi yangu ni muziki sidhani kama
nisingeweza kukutana nao kuangalia maslahi yangu,” alisema Badi.
Badi Bakule ni miongoni mwa wanamuziki wenye uwezo wa juu
katika ramani ya muziki wa dansi hapa nchini, huku sauti yake ikipendeza zaidi
anapofanya kazi pamoja na Mwinjuma Muuni, tangu enzi za Tam Tam.
No comments:
Post a Comment