Na Kambi Mbwana, aliyekuwa Handeni
LICHA ya baadhi ya vijiji kupitiwa na line za umeme kwenye paa
za nyumba zao, nishati hiyo muhimu kwa uchumi duniani kote inaendelea kuwa kitendawili
kwao. Nashangaa na kujiuliza maswali kila ninapoangalia nguzo hizo za umeme
vijijini humo.
Katika suala kama hilo, si tu watu wanashindwa kufahamu
utendaji kazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), linalojipambanua kutaka
maoni jinsi ya kujiendesha kwa mafanikio makubwa nchini, ila wao na serikali yao
wanaendelea kudharauliwa kutokana na sera zao na mipango yao kuwa kwenye
makaratasi zaidi.
Mkuu wa Mkoa Tanga, Chiku Galawa
Hakuna mipango zaidi ya porojo katika majukwaa yao, hasa wanaposema kuwa
kila kijiji au Mtanzania lazima apate huduma ya umeme. Ni kweli au
tunadanganya?
Hawawezi kufanya kazi kama
timu moja. Badala yake, wanayatatua kwa kupitia maandishi katika karatasi zao,
hivyo kushangaza umma. Nasema hivi huku nikijua baadhi ya vijiji havina umeme
bila sababu za msingi.
Kwa mfano, ukitoka katika wilaya Korogwe kwenda Handeni,
utashangaa kuona njia nzima kumepitishwa umeme unaopelekwa Handeni mjini.
Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu
Kwa sababu hiyo, vijiji vyote vilivyopitiwa na huduma hiyo,
hakika ni aibu kama hadi leo, wananchi wake
hawaipati, licha ya kuwa walinzi wa nguzo na waya hizo.
Kwanini nasema hivyo? Njia ya umeme inayokwenda Handeni,
ingeweza kuwanufaisha pia wananchi wa vijiji vyote hadi kufika Handeni Mjini, kama ilivyofanya hivyo kwa vijiji vya Sindeni, Misima na
Kwenjugo. Lakini, hadi leo, vijiji hivi vya Komsala na Kwakiliga huduma hiyo
hawaipati zaidi ya kuangalia kwa wenzao.
Kwa jinsi nilivyozungumza na wananchi hawa, wamechoshwa na
mwenendo huu, huku wakiona ajabu ya vijiji vyao kupitwa kimaendeleo na
kukumbukwa pia katika suala zima la nishati ya umeme yenye kuchochea maendeleo
kwa watu wengi.
Hapa ndipo ninapojiuliza maswali. Kwanini? Ni tatizo gani
linalokwamisha wananchi wa vijiji hivi wakose huduma hiyo muhimu? Wizara ya
Nishati na Madini inajua kuwa ili Taifa lao liwe na maendeleo, lazima huduma ya
umeme itumiwe na kila mtu.
Ni umeme tu unaoweza kuboresha kipato cha mtu mmoja mmoja.
Leo hii mwananchi anaweza kuuza hata maji baridi na akaingiza visenti. Leo hii
vijiji vya aina hiyo vinaweza kuboresha huduma za afya kwakuwa umeme upo
kijijini kwao.
Vituo vya afya, maduka ya dawa za binadamu na mifugo
vitapatikana kwa wingi. Lakini hali ikiendelea hivi, ina maana wananchi
hawataendelea.
Huduma zao zote watazipata katika wilaya ya Korogwe, hasa
kwa vijiji hivi viwili visivyokuwa na umeme kwa miaka 51 sasa ya Uhuru na
watendaji wakiwa wamefumba macho.
Hakuna sababu ya msingi. Ni uzembe na ubabaishaji wa aina
yake. Utashangaa kama kuna watendaji kutoka katika Shirika hili la umma la
Tanesco. Kiutendaji, vijiji vya Komsala, Kwamatuku na Kwakiliga vinastahili kuhudumiwa
na wilaya Korogwe.
Wamefanya hivyo kwasababu ni ngumu watendaji kutoka wilayani
Handeni hadi katika vijiji hivi ambavyo vipo karibu kabisa na Korogwe. Sawa.
Sio tatizo la kuangalia nani au wapi wanatakiwa uhudumia upande Fulani.
Ila wasiwasi wangu ni huu uzembe unaofanywa na watu bila
sababu za msingi. Ingawa vijiji hivi vipo wilayani kwao, lakini Handeni haina
sauti juu ya kero hii. Badala yake wanawaachia wilaya ya Korogwe, ambayo kwa
hakika ina mapungufu mengi.
Wao Korogwe walitakiwa waandike bajeti na kuviombea vijiji
hivi ambavyo kwahakika vinastahili kupata huduma ya umeme. Endapo Shirika la
Umeme halitakuwa na uwezo wa kutatua kero hiyo, basi wafikishe kwenye ofisi za Rural
Energy Agency (REU), waliopewa jukumu la kusambaza umeme vijijini.
Hichi ni kitengo kinachofanya kazi chini ya Wizara ya
Nishati na Madini yenye Waziri makini na mchapakazi, Profesa Sospeter Muhongo.
Hakuna asiyetambua utendaji wake. Lakini, watu waliokuwa katika baadhi ya
vitengo ni wadhaifu.
Kutokana na hilo,
kuna haja ya kujipanga upya. Hatuwezi kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania, kama hadi leo kuna vijiji ambavyo havina umeme na wapo
kwenye underline. Huu ubabaishaji unaletwa na nini?
Miaka 51 ya Uhuru Tanzania tunavuna nini? Haya lazima
watu wayajuwe. Mapema wiki hii nilipata kuzungumza na watendaji zaidi ya watatu
kutoka wilayani Handeni, Korogwe na Tanga, ambapo ndipo kwenye ofisi za mkoa.
Nisingependa kuwataja watu hao ambao kwa hakika wana sauti
na nafasi kubwa katika ofisi hizo za Tanesco katika kila wilaya na Mkoa kwa
ujumla. Maneno yao
niliyaelewa.
Maana wote wameonekana kulia na serikali na kukosa mbinu za
kiutendaji kwa ajili ya kufanikisha maisha bora kwa kuwafikishia kwanza huduma
ya umeme wananchi vijijini.
Mmoja alisema, “vijiji vingi vinashindwa kuunganishiwa umeme
kwasababu ya ukosefu wa bajeti kutoka serikalini. Kumbe?
Tatizo ni bajeti au kuna lingine? Nauliza hivyo kwasababu
vipo vijiji vilivyopitiwa na njia ya umeme na visivyohitaji gharama kubwa
kuwaunganisha kwenye huduma hiyo muhimu duniani kote.
Mbaya zaidi, wenzao wameipata huduma hiyo. Nadhani haya ni
matatizo makubwa na mfumo mbaya wa watendaji wetu. Watu wanaostahili waendeshwe
kwa viboko. Sio lazima mpaka watu waseme au kulia hata pale pasipostahili.
Akili ya kawaida tu, inaweza kumuongoza mtu kuamua namna ya
kuongoza kwa faida ya mwananchi mmoja mmoja na serikali kwa ujumla. Sina ugomvi
na REA.
Hawa wanapelekewa muongozo na maombi kutoka kwa ofisi za
Tanesco wilayani au mkoani kwa ajili ya kupeleka umeme vijijini hasa kama kwa fedha zao wenyewe wameshindwa.
Naamini fedha wanazo. Huo ndio ukweli. Katika kila nyumba
iliyounganishwa huduma ya umeme hapa nchini, anakatwa kodi asilimia 22. Kiasi
hiki kimeganywa katika makundi matatu ambayo ni VAT asilimia 18, REA asilimia 3
na EWURA wanapata asilimia moja.
Kwa maana hiyo, asilimia tatu hizi za REA zinazolipwa na
wananchi, lazima zitumike kwa mafanikio sambamba na kusambaza huduma hiyo
vijijini. Tanesco katika wilaya hadi mikoa lazima wafanye kazi yao
kama inavyotakiwa.
Watembelee kwenye vijiji visivyokuwa na gharama katika
uunganishaji wake. Huo ndio ukweli. Muda huu sio wa kupiga porojo ofisini huku
tukiwaacha watu katika umasikini wa kutupwa kutokana na utendaji wetu mbovu.
Watu wanashangaa. Haya maisha bora yanayosemwa yameshafika
au bado yanasubiriwa baada ya kuhubiriwa kila uchao na wanasiasa wetu? Kama bado tunafanya bidii kuyatafuta? Kwa njia gani? Ni
biashara, kilimo na viwanda.
Lakini biashara au viwanda haviwezi kwenda vizuri kama umeme wa uhakika haupatikani. Haya ni matatizo
makubwa. Nadhani Waziri wa Nishati na Madini, Muhongo angekutana sasa na
watendaji na kuwakemea vikali.
Ni aibu kubwa. Kama vijiji
ambavyo wapo kwenye underline na hawana umeme, vipi vile vijiji vinavyohitaji
kupelekewa njia kwanza, tena katika umbali mrefu na kutumia gharama za fedha na
muda kwa ujumla?
Haya lazima tujiulize. Tunawekaje mazingira ya kujiendesha
kwa mafanikio na sio kukaa ofisini kutumia fedha za umma bila mpango. Tanesco
Korogwe, Handeni na mkoa kwa ujumla waone hii ni aibu yao na jamii inawacheka.
Serikali ya Jakaya Mrisho Kikwete itakuwa na changamoto
nyingi, maana kati ya sera au urendaji kazi wake unakwamishwa na watu wake.
Anahubiri kweli maendeleo, lakini ndoto hii inaishia njiani na kuwaumiza watu
wengi.
Kwanza lazima tujuwe,
kijiji chenye hadhi ya kupata umeme na ikakosa, basi watalaamu wanajua jinsi
serikali imavyokosa mapato kutoka kwao.
Mbali na serikali kutopata mapato kwasababu ya vijiji hivyo
kutokuwa na umeme, bali pia wananchi wanaendelea kulowea kwenye umasikini maana
hawawezi kufanya biashara imayohitaji umeme.
Simu inapokwisha chaji, ina maana mwananchi huyo
inamlazimisha atoke kijijini kwao hadi wilayani Korogwe na kutumia muda mwingi
njiani. Matokeo yake mtu huyo anashindwa kufanya kazi nyingine za kimaendeleo.
Hii haiwezi kukubaliwa. Serikali kwa kupitia Wizara ya
Nishati na Madini, REA na ofisi za Tanesco katika wilaya hadi mkoa kuna haja ya
kujipanga kwa ajili ya kuondoa kero hizi kwa namna moja ama nyingine.
Ni rahisi sana.
Ni nzuri. Heshima kwa serikali itarudi, ukizingatia kwamba kiongozi wa serikali
kuzungumzia maendeleo anapata kazi kubwa, maana njia anayopita ni ndefu na
wananchi wanajua jinsi watu hao wanavyoweza kupiga soga.
Huu ndio ukweli wa mambo. Tuukubali kwa ajili ya kusonga
mbele kwa kuhakikisha kwamba watu wengi zaidi wanapata huduma ya umeme ili waangaze
maisha yao.
Vinginevyo kazi ipo.
Tukutane tena wiki ijayo.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment