MGODI UNAOTEMBEA
Katibu Mkuu Chadema, Dk Wilbrod Slaa
Na Kambi Mbwana, Dar es
Salaam
KUKIKOSOA Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kunahitaji moyo wa uzalendo na kujitoa kwa
nguvu zote, hasa ukijua kuwa kadhia utakayoipata kutoka kwao ni kubwa mno.
Ni dhahiri, Chadema kama
vilivyokuwa vyama vingine vya siasa, nao hujiona kwamba katika kila wanalofanya
hapa chini ya jua, ni jema.
Akijitokeza mtu wa
kuwaonyeshea kidole, wataanza kulalama na kusema bila ukomo. Watasema yasemwayo
yanametokana na matakwa ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
Kuna siku moja niliwahi
kufanya mazungumzo kwa kupitia simu na Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene
na kugundua kuwa kila ambalo nimekuwa nikifanya kwa maslahi ya Taifa, aliona si
mazuri, hasa kama nimekosoa chama chao.
Kwa bahati nzuri nakumbuka
makala nyingi nilizowahi kuandika, iwe za kuikosoa CCM, Chadema au Chama Cha
Wananchi (CUF), zimekuwa zikielezea tatizo na suluhu yake, ukizingatia kwamba
vyama hivi ndio vinavyokubalika kwa Watanzania wengi.
Makene alifanya hivyo
kwakuwa ana haki na wajibu wa kuhoji juu ya mwenendo wa waandishi na wachambuzi
wa siasa, maana wapo kwenye meza yake.
Hata hivyo, kati ya majibu
niliyompa kwa wakati huo, nashukuru yalitoka katika kichwa changu na ukweli ni
kuwa ‘Mgodi Unaotembea’ haujaelemea kwenye chama chochote cha siasa na ndio
maana unasimama kwenye ukweli.
Wafuasi wa CCM
Kwanini nimeanza hivi?
Chadema ni dhahiri ngoma yao haitakesha kamwe. Nasema haya kwakujua kuwa,
baadhi yao wamekuwa wepesi sana kucheza wimbo unaopigwa na vyama vingine vya
siasa, hasa CCM na CUF.
Chadema ni rahisi sana
kuyumbishwa hata kwa sababu nyepesi, hivyo kuonyesha kuwa uwezo wao, upeo wao
wote unaweza kuamuriwa na kada au kiongozi mmoja tu kutoka kwenye chama kimoja
cha siasa nchini.
Ndio, maana hivi sasa
Chadema wanashikana mashati baada ya kauli moja tu ya Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa CCM, Nape Moses Nnauye. Nape alisema jijini Mwanza kuwa Katibu Mkuu
wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa ana kadi ya CCM.
Wafuasi wa CUF
Sawa huenda kweli anayo.
Lakini wote hawajui kuwa Slaa ana kadi ya CCM. Nape alisema kwakuwa ndio wakati
wake. Yeye ndio Katibu wa Uenezi na alifanikiwa kueneza, maana aliyosema
yanaleta balaa kwenye chama hicho.
Wafuasi wa Chadema
Viongozi makini na
wanachama wanaojitambua, hawapaswi kuanza kuparuana wakimtaka Katibu wao, Slaa
eti ajiuzulu. Kwanini? Kwamba ana kadi ya CCM? Hivi Chadema hawajui kuwa Slaa
alikuwa kada wa CCM?
Sawa alipaswa kuirudisha
au kuichoma moto kama wanavyotaka wao wanaopenda siasa za kujionyesha
majukwaani, lakini hii njia wanayopita ni sahihi kwa ajili ya chama chenye
nguvu na malengo ya kushika dola?
Pia tujiulieze maswali.
Ingekuwaje Slaa angekuwa rais wa Tanzania baada ya Uchaguzi uliofanyika mwaka
2010 na kumsumbua Rais wa Tanzania, Dk
Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM?
Je, Nape kama kawaida yake
angesema kuwa Slaa ana kadi ya CCM? Wanachama na wafuasi wa Chadema leo hii pia
wangetaka ajiuzulu?
Maswali haya najiuliza
baada ya kugundua kuwa licha ya wapinzani kukubalika kwao, vichwa vyao, nafasi
zao, upeo wao kisiasa bado ni mdogo kiasi cha kushindwa kufahamu masika au
kiangazi katika maisha ya vyama vyao.
Kumbe Nape ni hodari mno
kuliko vichwa vya umoja wa vijana wa Chadema na viongozi wengine, hasa kwa hoja
yake hiyo inayoweza kusababisha chama hicho kusambaratika kwa kasi.
Bila hata kusimama upande
mmoja, CCM wenyewe wanajua kuwa kichwa cha Slaa ni mahiri na kinaweza
kuwasumbua wakati wowote. Katika hilo, wapo wanaopewa jukumu la kuhakikisha
kuwa Chadema haitulii.
Na kwa vipi isitulie? Ni
kuhakikisha kuwa kinavurugika kuanzia katika nafasi ya Katibu Mkuu, ambaye ni
dhahiri Watanzania waliokuwa wengi wanazidi kuona Slaa anafanikiwa kuongoza
Watanzania katika Uchaguzi ujao.
Kwa kufanikisha madai yao
ya Slaa ajiuzulu kwa sababu eti ana kadi ya CCM, Chadema itamchagua nani
kurithi mikoba yao? Ndio wapo, lakini watakuwa salama? Je, atakayerithi
hajatokea katika mikona ya CCM?
Ukiangalia suala hilo,
utagundua kuwa ni wazi kuwa chama kitakwenda mwisho wake kitaanguka. Kwa
kuanguka kwake leo au kesho kwasababu ya kuanzishiwa zogo na kulifanyia kazi
kama majuha, ngoma yao haitakesha.
Wahenga wa zamani walisema
siku zote kuwa ngoma ya kitoto haiwezi kukesha. Ni kweli kabisa. Chadema
wanaweza kufuata nyayo hizo. Kwa kuwategemea wafuasi na makada au viongozi wa
CCM, wakiongozwa na Nape.
Mwishoni mwa wiki, Baraza
la Vijana la chama hicho (BAVICHA), kwa kupitia Katibu wa mkoa wa Mwanza, Salvatory
Magafu, lilivalia njuga suala la kadi ya Slaa na kutangaza maandamano ya
kumng’oa madarakani.
Kauli ya Magafu ilipingwa
vikali na Mwenyekiti wake, Liberatus Mlebele, kwa madai kuwa sio msemaji wa
umoja huo, ambao kwa hakika ni msimamo wa kunyoosheana vidole kutoka kwa
viongozi wa chama hicho.
Kwa bahati mbaya, maneno
ya Magafu yalizua utata kwa baadhi ya makada na wapenzi wa Chadema, hasa kwa
kuyapayukia baadhi ya magazeti na waandishi wao kwa madai kuwa wanafanya kwa
nia ya kukiharibu chama chao.
Hii ni tabu sana. Watu
wengi wamekuwa wakiangalia walipoangukia badala ya walipojikwaa. Kwa mwendo huu
upinzani kushika dola itakuwa ngumu. Kinyume chake CCM itaendelea kuwa watalwa
wa Taifa hili.
Wanajua wanachofanya.
Wanajua ili kukineemesha chama chao basi ni kuwaimbia wimbo wowote ambao nao
bila kujua, wapinzani watauchukua na kuuimba pamoja na kucheza. Hakuna
maelewano ya aina yoyote.
Na wanajua pia baada ya
Slaa kupotea litaibuka tena la mbio za urais za Mbunge wa Kigoma, Zitto Kabwe,
Freeman Mbowe na Slaa. Njia hii inajenga uhasama kwa viongozi wa juu wa
Chadema, ambao nao wana matawi yao.
Na kama maelewano
yanakosekana, nani anaweza kujenga hoja ya kukijenga chama wakati hakuna
anayempenda wala kumheshimu mwenzake? Sawa, lakini njia hii ni tunu kwa CCM.
Kila mwana CCM anafurahia matokeo ya sasa.
Mvurugano uliopo ni ishara
kuwa ngoma ya kitoto haikeshi na ndoto ya upinzani kushika dola kwa vyama hivi
bado. Watanzania wataaminishwa uongo, maana ukiangalia mfumo mzima wa Chadema
katika kila mkoa utagundua msigano usiokuwa wa lazima.
Na kwakuwa wataalamu
kutoka CCM wanaweza kuwachezea wanavyotaka, ni dhahiri kila litakalosemwa
litakuwa kubwa na kuwachanganya zaidi wapinzani hao, huku ajenda yao ya
kujiuzulu ikikolezwa zaidi.
Tunasema hili kwakuwa
baadhi yao tunajua kuwa kwa kuwapo vyama vya siasa vya upinzani, walau yapo
maendeleo makubwa kwa Taifa hili, maana inajulikana wapinzani ndio wakosoaji wa
serikali iliyokuwapo madarakani.
Makala ya Mgodi Unaotembea, huchapishwa na gazeti la Mtanzania kila Jumatano na Jumapili.
kambimbwana@yahoo.com
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment