Na
Kambi Mbwana, Dar es Salaam
CHAMA
Cha Muziki wa Injili Tanzania,
jana kimeandaa kikao cha pamoja na waimbaji wake kwa ajili ya kuangalia
changamoto zinazowakabili, wakishirikiana na Mfuko wa Pensheni wa LAPF na Grace
Production inayotengeneza bidhaa mbalimbali za vipodozi.
Mkutano
huo ulifanyika jana katika Hoteli ya Wanyama iliyopo Sinza Mori, jijini Dar es Salaam, huku
ukikutanisha wasanii wengi akiwamo Bahati Bukuku.
Akizungumza
jana jijini Dar es Salaam katika kikao hicho cha pamoja cha kujadili maisha ya
wasanii miaka ya baadaye, Rais wa Chama hicho, Addo November, alisema kwamba maisha
ya wasanii hayaonyeshi kesho nzuri, hivyo wameamua wakutane kulijadili jambo hilo.
Alisema
kumekuwa na tatizo kubwa la wizi wa kazi za wasanii huku serikali yenyewe ikiwa
haina majibu ya moja kwa moja, hivyo kwa kufanya kikao hicho wakiwa na wadau
wao, wakiwamo Grace Production, LAPF na wengineo wanaamini watakuwa na jibu la
msingi kwa watu wote.
“Huu
ni wakati wa kuangalia namna gani tunaweza kufanya mambo yenye kuleta maendeleo
kwa watu wote wakiwamo wasanii ambao baadhi yao wanaishi kwa tabu kutokana na kazi zao
kunufaisha watu wengine.
“Naamini
hapa watapewa elimu kubwa ya kuhusu maisha yao ya leo na kesho, ukizingatia kwamba lengo
letu ni moja la kuwakomboa wasanii nchini,” alisema.
Naye
mwimbaji mahiri wa muziki huo nchini, Bahati Bukuku, aliitaka serikali kuingia
kwa undani zaidi kwenye matatizo yao badala ya
kuwaacha kama walivyo.
Bahati
kwa sasa anatamba na wimbo wake wa Dunia Haina Hurumu huku ukifanya vyema
katika chati za muziki huo hapa nchini na kumuweka juu zaidi.
No comments:
Post a Comment