Felister Phillip Maginga-Lady Black
Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
KUTOKANA na mafanikio katika kona ya muziki wa kizazi kipya
maarufu kama Bongo Fleva, vijana wengi wamekuwa wakijiingiza katika sanaa hiyo
kwa ajili ya kujitafutia maisha yao.
Katika hilo,
wapo wengi wanaofanikiwa kwa namna moja ama nyingine, jambo linalofanya wasanii
wachanga kukimbilia kwa wingi katika tasnia hiyo ya muziki nchini.
Miongoni mwa wasanii hao wachanga ni Felister Phillip
Maginga. Binti huyo mwenye asili ya Shinyanga, amepania vilivyo kuhakikisha
kuwa anaweza kujipatia maisha yake kwa kupitia sanaa ya muziki wa kizazi kipya.
Dada huyo anajulikana kama
Lady Black. Tayari amesharekodi wimbo wake unaopigwa katika baadhi ya vituo vya
redio hapa nchini. Wimbo huo unaitwa Dis Me, aliyoimba kwa mtindo wa Hip Hop,
muziki unaohitaji ubunifu mwingi.
Katika mazungumzo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki
iliyopita, Lady Black, anasema kwamba ameamua kujiingiza katika muziki wa Hip
Hop ili aboreshe kipaji chake na kutafuta maisha yake kwa kupitia muziki.
Anasema amezaliwa na kipaji cha muziki tangu akiwa na umri
mdogo, hivyo kwa kitendo chake cha kuamua kushika kipaza sauti, ni kuweka mambo
sawa na kufanikisha kutimiza moja ya malengo yake aliyojiwekea.
“Napenda sana
kuimba tangu zamani hasa muziki wa Hip Hop hapa nchini, huku moja ya watu
ninaotamani kufanya nao kazi ni Ney wa Mitego.
“Naamini haya yote yatafanikiwa kwasababu nimejipanga imara
katika kuweka malengo yangu na jinsi gani ya kuanza vyema safari hii
ninayoipenda na kuweka mikakati kabambe katika kuhakikisha kuwa natimiza
malengo yangu,” alisema Lady Black.
Dada huyo anasema licha ya kuachia wimbo huo wa Dis Me,
lakini unapigwa kidogo kidogo kutokana na ugeni wake katika ramani ya muziki wa
Hip Hop nchini, huku akiamini kuwa nyimbo zitakazofuata mambo yatakuwa mazuri.
Anasema licha ya kuimba muziki wa Hip Hop, lakini kipaji
chake kimekuzwa na muziki wa asili, akimpenda zaidi mwimbaji Saida Karoli
aliyewahi kutamba ndani na nje ya nchi na nyimbo zake nyingi ukiwamo Chambua kama Karanga.
Lady Black anasema kwamba wimbo wake wa kwanza ameurekodi
katika Studio za Ukombozi zilizopo Yombo, huku ukifanikiwa kumuweka katika
ramani nzuri kutokana na ugeni wake katika tasnia ya muziki huo nchini.
Msanii huyo anasema kipaji chake kilizidi kushika kasi baada
ya kutua jijini Dar es Salaam, akitokea kijiji kwao Ilola, kilichopo Shinyanga
Vijijini mwaka 2002, ambapo pia safari yake ilitokana na wazazi wake kuhamia
jijini humu.
Anasema kwamba baada ya kutua Dar es Salaam, alijiunga na
vikundi mbalimbali kwa ajili ya kujiwekea mazingira mazuri ya kibiashara,
akijua kuwa katika mtindo huo, vijana waliweza kustawisha vipaji vyao.
Mwanadada huyo mwenye mwonekano wa kisanaa anasema kwamba
kwa sasa anachofanya ni kuweka mazingira mazuri ya kibiashara kwa kutunga na
kurekodi nyimbo nzuri kwa ajili ya kumnemeesha zaidi.
“Huu ni wakati wangu wa kufanya kazi nzuri zaidi kwa ajili
ya kuniweka katika nafasi nzuri, ukizingatia kwamba nimeamua kufanya kazi ya
muziki, hivyo lazima nivumilie na kuweka mikakati kabambe nifikie malengo
yangu.
“Naamini mambo yatakwenda sawa kwa kuhakikisha kuwa natunga
nyimbo na kuwapelekea mashabiki wangu kazi nzuri zenye ujumbe na mtindo wa
kuwafurahisha zaidi, ukizingatia kwamba nimeamua kuishi kisanaa,” alisema Lady
Black.
Mwanadada huyo anasema kwamba kwa sasa anafanya kazi bila
kuwa na kundi lolote, ingawa ana ukaribu na wasanii kadhaa akiwa na lengo la
kufanya kazi kwa ushirikiano na wasanii waliotangulia na kusoma nyendo zao.
Binti huyo aliyezaliwa mwaka 1987, anasema kwamba anafanya
kila awezalo kuhakikisha kuwa anafanikiwa kisanaa, bila kuangalia changamoto
gani anakutana nazo katika tasnia ya muziki huo nchini na yenye mafanikio
mengi.
Lady Black anasema kwamba maisha ya sanaa yanahitaji
uvumilivu wa aina yake, ikiwamo wakati mwingine kuonekana muhuni kutoka kwa
baadhi ya watu wanaoamini kuwa sanaa inatakiwa ifanywe na wanaume na si
wanawake.
Licha ya kuanza zamani kupenda muziki, lakini mwaka 2008,
kipaji chake kilizidi kushamiri pamoja na kupata hamu ya kufanya kazi ya muziki
kwa mafanikio makubwa, akiwa na lengo la kuonyesha makali yake.
Anasema anashukuru kwa kuweka mkazo katika suala hilo, nyota yake imezidi
kukua kiasi cha kuanza kuona dalili njema katika maisha yake ya sanaa, hasa kwa
kufanikiwa kuingia studio na wimbo wake kupigwa katika vituo vya redio.
Dada huyo anasema kwamba muziki wa kizazi kipya unalipa hasa
kwa wasanii wanaojitambua na wenye uwezo wa kufanya kazi kwa umakini, hivyo
anaamini kwa upande wake atafikia malengo yake ya kuwa msanii nyota.
Anasema katika hilo
anafanya kazi kubwa ya kuhakikisha anawaweka mashabiki wake katika mtego wa
kuona hawawezi kuwa mbali na yeye, kutokana na utunzi wa nyimbo zake zote
zitakazofuata.
“Muziki ni mzuri lakini ni ngumu sana
kuendelea kuwa juu kama mtu anashindwa kutunga
nyimbo nzuri, ndio maana kuchelewa kwangu kuibukia katika sanaa ya muziki wa
kizazi kipya, nimejifunza mambo mengi mazuri kwa ajili ya sanaa yangu.
“Naamini katika hili mambo yatakuwa mazuri, maana kwa
kutunga nyimbo nzuri pamoja na aina ya uimbaji wangu, wadau wataniunga mkono na
kunifikisha mbali, ukizingatia kuwa msanii anahitaji mipango ya hali ya juu,”
alisema.
Mwanadada huyo anasema kwamba licha ya kuweza kuimba kwa
utundu na kughani mashairi yake, pia ana uwezo wa kucheza, akikumbukia wakati
wa uwepo wa ma-camp mengi na kutembelea
kwa ajili ya kuonyesha makali yao.
Anasema kuingia kwake kwenye camp ni kutafuta namna ya
kutoka kisanaa, akisema wakati huo kila camp lilikuwa
likialikwa na wenzao pamoja na kutoa nafasi ya wasanii kupanda jukwaani
kuonyesha cheche zao.
Lady Black anamalizia kwa kuwataka wadau na mashabiki wa
muziki wa kizazi kipya hapa nchini kukaa makini na kusubiria nyimbo zake,
akiamini kuwa ni nzuri zitakazowapatia shangwe na amani katika mioyo yao.
No comments:
Post a Comment