Mbunge wa Handeni, Abdallah Kigoda
Na Kambi Mbwana
KUTOKANA na uhaba wa ukosefu wa ajira, Tanzania
ingeweza kuwapatia ajira vijana wake, endapo ingewekeza kwa dhati katika
michezo, hususan huu wa mpira wa miguu unaotesa duniani.
Kama hivyo ndivyo, basi
kuwekeza huko kungeanzia katika vijiji, wilaya na baadaye mkoa, katika hali ya
kuona kwamba wenye vipaji vya michezo wanaingia kwa wingi na kujiendeleza
zaidi.
Hakika natamani kuandaa ligi ya aina hiyo, hasa kwa wilaya
ya Handeni ambayo nina uhakika vipaji vingi vipo, ingawa hakuna mwenye nia ya
dhati ya kuandaa mashindano hayo ya vijana.
Natamani kuandaa mashindano hayo, maana vijana wana vipaji
vingi ila wanakosa sehemu ya kuvionyesha. Nashindwa kuvumilia kila ninapoona
vipaji vinatokomea msituni, wakichimba mawe au kukata mkaa.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu
Inauma kuona wenye vipaji vyao wanaishia kulala kwenye
vichaka, maana hakuna mwenye lengo la kuwaendeleza. Huu ndio ukweli.
Wilaya ya Handeni, imesheheni vijana wenye vipaji.
Watoto hao wa masikini wanacheza soka la uhakika. Lakini
wanakufa njaa. Hakuna hata Kombe la Mbuzi linaloweza kuwaweka sawa wachezaji na
kutafuta maisha ya juu zaidi kutokana na michezo.
Kama kila diwani au Mbunge
angeandaa ligi yenye ubora katika wilaya hiyo, mambo yangekuwa mazuri zaidi.
Najua wapo watakaosema kwanini iwe Handeni tu na sio wilaya nyingine?
Tatizo ni mwanzo tu. Kila mmoja sasa na afanye juhudi zake
kwa nafasi yake ili kuibua vipaji na kuendeleza maisha ya wachezaji hao. Kama kila Kata ingekuwa na kombe imara, basi mambo
yangekuwa mazuri.
Kata hizo ni pamoja na Chanika, Kabuku, Kang'ata, Kiva, Komkonga, Kwaluguru, Kwamatuku, Kwakhonje, Kwamsisi, Kwasunga, Kwedizinga,
Mazingara, Mgambo, Misima, Mkata, Ndolwa, Segera, Sindeni na kata
ya Vibaoni.
Wilaya ya Handeni yenye kata 19 inaweza kuboresha maisha ya
vijana kama kungewa na mipango ya dhati. Ligi
ya Kata itakayozaliwa ya wilaya. Sipati picha hali ingekuwaje na vipaji
vingetangazwa vipi.
Ndio maana nasema natamani kuanzisha ligi ya Handeni, ingawa
mfuko wangu unanisuta. Nimeamua kuandika hivi, nikiamini wale wenye uwezo wao
ni wakati wa kulifikiria hilo
kwa kina.
Kila Kata ifanye mchanganuo wake kwa ajili ya kuwa na
mashindano ya vijana yenye nguvu, ambayo naamini vipaji vyao vitaongezeka na
kupata nafasi ya kuvionyesha machoni mwa watu.
Zipo timu nyingi mno ila jinsi ya kufika huko ndio tabu. Sio
Handeni tu bali na wilaya zote za Tanzania kuwa na mipango hiyo
ambayo kwa hakika ni dalili njema za kutangaza vipaji vya watu wao.
Sio Handeni tu katika Mkoa wa Tanga, bali mipango hiyo iwe
ya nchi nzima. Wakifanya hivyo, nadhani mambo yatakuwa mazuri zaidi. Tutakuwa na
wanamichezo mahiri na sio wachache wanaojulikana sasa.
Juhudi hizo zitakuwa na matunda makubwa, maana ukiangalia
kwa sasa, vipaji vyote vya mikoani huko, vinaishia kwenye kukata mkaa au kulima
kwa jembe la mkono, ingawa Mungu aliwapa vipaji.
Huo ndio ukweli wa mambo. Ningekuwa na uwezo huo ningefanya
sasa, maana kwakweli nimeshindwa kuvumilia. Siwezi Kuvumilia kuona vipaji
vinafanyiwa mzaha. Itakuwaje?
Je, ni kweli tumeamua kuzalisha wanasiasa wengi na sio
wanamichezo? Kama sio kweli, basi upo mbali na
uongo. Tuamuwe sasa na kuvaa vibwebwe kwa ajili ya kuendeleza vipaji vya
Watanzania wenzetu.
Kwakuwa najua ubora wa vipaji vya wananchi hao wa Handeni,
naamini wanakufa na vipaji vyao, maana hakuna mpango wa kuwaendeleza na kuwapatia maisha bora kwa kupitia michezo.
kambimbwana@yahoo.com
kambimbwana@yahoo.com
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment