Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SERIKALI kwa kupitia Wizara ya
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, imetangaza rasmi kuwa kuanzia kesho Desemba
31, Tanzania
itaanza kuingia kwenye mfumo mpya wa urushaji wa matangazo wa kutoka Analogy
kwenda kwenye Digitali.
Taarifa ya Naibu Waziri, January Makamba, ilisema kuwa uamuzi huo
unatokana na kurejea tangazo lao la Februari 23 mwaka huu juu ya usitishwaji wa
matangazo ya televisheni kwa kutumia teknolojia ya analojia kwenda teknolojia
ya dijitali.
Makamba alisema maandalizi ya kuzima mitambo ya
analojia kuanzia 31 Desemba 2012 yamekamilika kwa mujibu wa makubaliano ya nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hata hivyo, serikali ilitangaza kuwa uzimaji wa mitambo
ya analojia utafanyika kwa awamu kama ifuatavyo, ikianzia na jiji la Dar Es
Salaam-31 Desemba, Dodoma & Tanga, Januari 31, Mwanza Februari 28, Moshi
& Arusha Machi 31, wakati Mbeya
itakuwa ni Aprili 30.
“Tumeamua kuanza kuzima mitambo
hiyo kwa Jiji la Dar es Salaam kwanza ili kutoa fursa kwa makampuni yenye
leseni kusimika mitambo ya utangazaji wa dijitali katika mikoa mingine, huku
tukiamini kuwa makampuni hayo yamejipanga kukamilisha usimikaji wa mitambo hiyo
katika mikoa minane katika miezi minane ijayo.
”Mitambo ya analojia itakayozimwa kesho ni ile iliyopo
Kisarawe na Makongo. Vituo ambavyo siku ya tarehe 1 Januari 2013, vitapaswa
kuanza kutangaza matangazo kwa mfumo wa dijitali ni TBC1, ITV, EATV, Channel
10, StarTV, DTV, CapitalTV, TumainiTV, ATN, MlimaniTV, C2C, CTN, CloudsTV na
Efatha,” alisema.
Alisema Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inafanya
jitihada za kutosha kuhakikisha kwamba makampuni yenye leseni za kusambaza
ving’amuzi yanakuwa na ving’amuzi vya kutosha na vingine vimeagizwa ili kukidhi
mahitaji ya baadaye na vile vilivyopo sokoni vina ubora unaokubalika.
Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania
itahakikisha kwamba zoezi la uhamaji linafanyika bila usumbufu na kero kwa
wananchi. Makampuni yanayouza ving’amuzi yameagizwa yaimarishe huduma kwa
wateja wakati wa kuuza ving’amuzi na hata baada ya ununuzi iwapo wananchi
watakuwa na matatizo na ving’amuzi.
”Zoezi hili la uhamaji ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Tutakapokuwa
tumekamilisha uhamaji, huduma za mawasiliano na utangazaji zitapanuka na kuwa
bora zaidi. Kwa mfano, itawezekana sasa kuangalia televisheni kupitia simu zetu
za mikononi.
“Vilevile, itawezekana, kwa bei
nafuu kabisa, kwa mtu mwenye uwezo wa kutengeneza vipindi kukodisha chaneli
yake na kutangaza vipindi vyake. Vilevile, bei za mawasiliano na utangazaji
zitashuka, na tutakuwa tumepiga hatua kubwa kwenye mapinduzi ya teknolojia
duniani, ambayo nchi yetu haiwezi kubaki nyuma,” alisema.
Makamba alisema serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uhamaji huu na kutarajia
kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau wa sekta ya utangazaji na
wananchi kwa ujumla katika kipindi cha uzimaji wa mitambo ya utangazaji wa
televisheni ili kufanikisha zoezi la uzimaji wa mitambo ya utangazaji ya
teknolojia ya analojia.
Uhamaji huu hautahusu televisheni za wananchi
zinazopata matangazo kupitia madishi (nyungo) (satellite) au nyaya (cables).
Hivyo, wananchi wanaopata matangazo kupitia DStv, Zuku, na nyinginezo
wataendelea kupata matangazo yao kama kawaida.
No comments:
Post a Comment