https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Thursday, December 13, 2012

Wameamua kuwa wasanii wa hapa hapa



Mkali kutoka Tanzania, Ali Kiba
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SANAA inazidi kufanya vyema nchini, kutokana na baadhi ya wasanii kujiwekea malengo ya dhati ya kupiga hatua, nje na ndani ya nchi.

Vijana hao wanafanya juhudi kubwa kujitangaza, ingawa baadhi ya wadau wanawakatisha tama kwa kuwafanyia ghiriba za kjila aina, hali inayowasononesha.

Juma Nature a.k.a Kiroboto

Wasanii hao wapo, hasa wale wanaotumia muda wao mwingi kuhakikisha kwamba mambo yao yanakuwa mazuri. Ukiwataja hao kwa majina, hakika hili la Msafiri Kondo, maarufu kama Solo Thang, litashika namba moja.

Mbali na Solo Thang, pia wamo wengine ambao kwa hakika wanafanya kila wawezalo kujitangaza, akiwamo Ali Kiba, Fresh Jumbe, pamoja na wasanii wanaotoka katika nyumba ya kulea vipaji, yani Tanzania House of Talents, (THT).

P-Squere wakionyesha poziii
 
Sawa, hao wapo na wanafanya bidii hiyo, Ila, vipi wale wengine katika nchi hii? Nasema hivyo maana najua wasanii ni wengi na wanaofanya sanaa kwa ujumla.

Wapo ambao hawana namna yoyote ya kupata tabu kwa ajili ya kujitangaza Kimataifa.

 Wasanii kutoka THT

Wao wameamua kuwa wa hapa hapa. Kazi yao kubwa ni kufanya hata yale yasiyofaa, ili jamii iwaone kwa kupitia vyombo vya habari, ambavyo baadhi yao vimejiweka katika mlengo wa uchafu na kuzalilisha vijana wetu, wale wanaojiita wao ni kioo cha jamii.

Hapo ndipo utakaposhangaa na kujiuliza maswali. Je, hizo ndio njia za kujitangaza ndani na nje ya nchi? Je, kuandikwa kwenye magazeti ya udaku ndio kujitangaza?

Kama hivyo ndivyo wanavyoamini wao na wadau wao, hakika wamechelewa mno. Kwa bahati mbaya, wametangulia stendi wakati nauli wameachia wenzao.

Msemo huu nimeutumia kama njia ya kuwajulisha vijana hao kwamba jamii yao, ama kazi yao bado ni ndogo mno. Wapo vijana ambao, leo hii tayari wanajiona wamefika, wakati hata Tanga, wapo ambao hawawajui.

Na wale waliojulikana, zama zao zimepita, kitu kinachoonyesha kwamba bado vijana hao wanatakiwa waweke mbele nidhamu ya kazi, iwe ni kuimba ama kucheza.

Huo ndio ukweli jamani. Tuuseme tu, maana bila hivyo, ni kama tunatwanga maji kwenye kinu. Tujiulize, msanii analipwa shilingi ngapi kwa shoo za nje ama ndani ya nchi.

Akishapata hesabu hiyo, arudi kutafakari wingi wa shoo hizo na jinsi anavyozitendea haki, kiasi cha kuwafanya watu wawatambue wao na nchi zao.

Itashangaza Rihanna atakapokuja Tanzania na kukosa watu ukumbini, kama sio uwanjani. Lakini, kizazi chetu hiki sidhani kama anaweza kujaza watu anapofanya shoo nje ya nchi.

Hapa wewe utashangaa. Mbaya zaidi utanisema kwa kuwafananisha wasanii wa Tanzania na wanaoshi Ulaya. Jamani, kuna tofauti gani kati ya wasanii wa Ulaya na Tanzania?

Au ni lugha tu ndiyo tatizo? Nasema hivyo huku nikiamini kuwa, hata leo Jennifer Lopez, akiimba wimbo kwa lugha ya Kiswahili, bado atajaza watu na kushangiliwa na wengi.

Nasema hivyo maana sio kweli kwamba mashabiki wote wa R-Kelly, 50-Cent wanajua Kingereza.

Wapo warabu, wachina, ambao hata lugha hiyo ni ngeni kwao, lakini wanapagawa vikali na burudani za wasanii hao, ambao baadhi yao wanaofahamu mtandao wa internet, wanaonekana wanavyoonyesha hisia zao.

Ila walichofanya wao ni kuwekeza zaidi kwenye ufanyaji wa shoo zao, utunzi wenye mpangilio na mengineyo.

Ndio wanabebwa zaidi na mafanikio ya nchi zao, ila nao wamejibeba, ndio maana walijipandisha na kuanza kulipwa fedha nyingi katika shoo zao.

Si tunao hapa waliokuwa wakilipwa shoo moja kwa milioni moja, lakini sasa baadhi yao wanaimba bure. Hutaki? Usiniulize Mr Nice alikuwa akilipwa sh ngapi  miaka mitatu iliyopita alipotingisha Afrika Mashariki na Kati.

Sasa hali ni mbaya. Hii lazima tuseme kwa ajili ya kuokoa maisha ya wasanii wetu, maana nao ni watu kama walivyokuwa wakina P-Square na wengineo.

Hili tulijadili kwanza kabla ya kuanza kuhoji nani anaibiwa kazi zake na wahindi, ama wakina nani wanauza CD ovyo, maana siku zote kutojitambua ni dalili mbaya na adui mkubwa katika maisha ya mwanadamu.

0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...