https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Thursday, December 13, 2012

MKALI WETU




Mwimbaji wa Samboira anayetikisa anga za Bongo fleva
Ben Pol, pichani
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KUNA nyimbo ambazo zinaweza kupigwa katika vituo vya redio na televisheni bila hata kuchezesha kichwa, lakini si kwa wimbo wa ‘Samboira’.  Wimbo huu uliombwa na msanii mahiri wa muziki wa kizazi kipya, maarufu kama Bongo Fleva, Ben Paul ‘Ben Pol’, unatamba katika vituo vya redio na televisheni nchini.

Samboira una maana ya Jichinnge umeimbwa kwa lugha ya Kinyambwa, yenye asili ya Tanzania, inayounganisha makabila zaidi ya 120. Ben Pol, anatamba pia kwa sauti yake tamu inayopita katika mioyo ya mashabiki wake kadhaa.

Kijana huyu, ametokea kupendwa kwa mashabiki weke wengi, huku aina yake ya uimbaji ukiwa kivutio kwa watu wengi. Katika mazungumzo na Handeni Kwetu, hivi karibuni, Ben Pol anasema kwamba muziki ni kipaji chake.

 Ben pol akiwa jukwaani

Anasema hali hiyo inadhihirisha katika aina ya utunzi wake, uimbaji wake sambamba na manjonjo anayokuwa nayo katika kuhakikisha kuwa mashabiki wake wanapata kitu adimu kutoka kwake na kufurahia kazi zake.

“Muziki ni kipaji changu nilichozaliwa nacho kutoka kwa Mungu, huku nikiamini kuwa utanipatia maisha mazuri pamoja na heshimu kama wengine.

“Naamini katika hilo nitafanya kila niwezelo katika kuandaa mashairi mazuri pamoja na nyimo ambazo watu wengi watavutiwa nazo, ukizingatia kwamba muziki unahitaji umakini na utundu wa hali ya juu,” alisema Ben Pol.

Mwaka jana Ben Pol aliingiza sokoni albamu yake ya kwanza iliyokwenda kwa jina la ‘Maboma’ iliyokuwa na jumla ya nyimbo 10. Baadhi ya nyimbo hizo ni pamoja na Maumivu, Maneno, Ninalinga, My Numbe 1 Fun, Samboira na nyinginezo.

Ben Pol kwa sasa anatamba na wimbo wake wa Pete aliyeimba kwa hisia kali na kuburudisha mashabiki wake kutokana na uimbaji wake.

Msanii huyo aliyezaliwa jijini Dar es Salaam mwaka 1989, anasema kwamba asili yake ni mkoani Dodoma, huku muziki wake akianza rasmi mwaka 2009, aliposhiriki katika shindano la Nyuki Djs, akiwa na Linah Sanga.

Katika mashindano hayo aliweza kufanikiwa kutangaza kipaji chake, hivyo kujiweka katiika mazingira mazuri, ambapo mwaka 2010, alikuwa kwenye nafasi nzuri kuonyesha uwezo wake huku akiwa ni mwanafunzi wa kidato cha sita, katika Shule ya Sekondari ya Azania.

Anasema hakuwa na usumbufu katika ufanyaji wake wa muziki, maana wazazi wake wote walikuwa wanapenda yeye awe msanii, ingawa walitumia pia muda wake kumpa ushauri wa kuendeleza zaidi elimu na muziki.

Anasema mwaka huo alifanikiwa kuachia wimbo wake wa kwanza wa Shining Star, akirekodi katika Studio za Man Walter, jijini Dar es Salaam, hivyo kumpa nafasi nzuri zaidi, hasa alipopata (label), mkataba wa ufanyaji muziki katika Studio za M-Rabu.

Katika mkataba huo, alirekodi tena wimbo wake wa pili, uliokwenda kwa jina la ‘Pata Raha’, katika kipindi cha mwaka mmoja tu, akiwa na ndoto za kuwika katika anga za muziki wa kizazi kipya hapa nchini.

Ben Pol anasema kwamba malengo yake ni kufanya kazi nzuri zaidi, ili kutangaza uwezo wake na kuwaziba midomo wasiopenda maendeleo yake.

“Muziki wangu nashukuru unapendwa na kila mtu, ndio maana wimbo wangu mpya wa ‘Pete’ nao umepokelewa kwa shangwe na wadau wote hapa nchini.

“Hata shoo zangu zinapendwa na watu wengi, hivyo naamini nitazidi kushika nafasi za juu katika anga za muziki wa kizazi kipya pamoja na kuchanua zaidi katika nchi mbalimbali duniani, ikiwamo Ulaya na kwingineko,” alisema Pol.

Msanii huyo anasema kuwa hajapata tabu kutoka kwa wazazi wake juu ya yeye kuingia kwenye muziki, maana walipenda mtoto wao afanye muziki kwa ajili ya kutafuta maisha yao.

Pia anasema katika familia yao, akiwamo baba yake, alikuwa msanii ingawa hajapata nafasi ya kufikia nafasi aliyokuwa nayo yeye. Hali hiyo inamfanya aone kuna kila sababu ya kupiga hatua katika tasnia ya muziki wao nchini.

“Haya ni malengo yangu, nikiwa na hamu ya kuwa msanii nyota pamoja na kutafuta nafasi ya kusoma zaidi elimu mbalimbali kadri nitakavyopata nafasi.

“Nawaomba wazazi na wadau wote waendelee kuniunga mkono kwa kuzipenda nyimbo na shoo zangu ili twende sambamba, maana sauti na kichwa changu kinachangia kunifikisha hapa nilipo na kuongeza bidii zaidi,” alisema Ben Pol.

Msanii huyo anasema kwamba muziki umekuwa na ushindani wa aina yake, huku wasanii wenye kuumiza kichwa, wakizidi kupata nafasi ya kuwika zaidi. Kijana huyo anasema kuwa anaamini ataendeleza mikakati yake ya kuwika zaidi.

Ben Pol anasema kuwa ushindani wa muziki uliopo unatokana na sanaa hiyo kuwaingizia kipati kikubwa wasanii wote nchini, hivyo kuonyesha kuwa sanaa ni kazi.

Katika tamasha la Fiesta linalofanyika kila mwaka hapa nchini, Ben Pol ni miongoni mwa wasanii waliofanya vizuri katika shoo hizo, huku akikonga nyoyo za mashabiki wake katika baadhi ya mikoa aliyotembelea.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...