UKITAKA kuuliza wilaya
gani ya Tanzania ambayo hadi
leo haijaharibiwa na vyama vya siasa, hakika Handeni itashika nafasi ya kwanza kama sio ya mwisho. Wilaya hii yenye vijiji 112 kata 19
na tarafa saba CCM imekuwa ikifanya vizuri mno.
Sio kama hakuna vyama vya
upinzani kwa wilaya hiyo yenye kabila la wazigua hakuna, vipo, ingawa havina
nguvu wala mashiko. Vijiji vyote vya wilaya hiyo vinatawaliwa na CCM, huku
wananchi mmoja mmoja wakishindwa kufanya mabadiliko ya aina yoyote.
Mwenyekiti wa CCM wilayani Handeni, Athumani Malunda
Hali hii ni changamoto kwa
CCM. Ni pale watakapoweza kukaa kimya na kushuhudia wapinzani wakishika wilaya
hiyo hasa kwa kusimamisha wenyeviti wa vijiji, madiwani au wabunge, hivyo kuwa
jambo baya kwao.
Kwanini nasema hivi? CCM
kuendelea kutamba katika wilaya ya Handeni ni heshima kubwa kwa wananchi wao,
wakiona chama hicho kinastahili kushika dola. Kwasababu hiyo, vitu kama vile shule za msingi na sekondari, vituo vya afya,
kilimo na shida ya maji ni mambo yanayotakiwa yaangaliwe upya.
Katika mazungumzo yaliyofanyika wilayani Handeni hivi karibun, mwenyekiti
wa CCM wilaya, Athumani Malunda, anasema kwamba kukubalika zaidi kwa chama chao
Handeni ni silaha ya kuendeleza mazuri yanayowapa imani na moyo wananchi wao
kwa ajili ya kuwa na imani nao zaidi.
Anasema moja ya mambo
wanayofanya ni kuhakikisha kuwa wenyeviti wa vijiji vya wilaya hiyo wanafanya
kazi zao kwa ushirikiano na wananchi wao, huku wakiwa wakali na wale wanaofanya
kazi kwa matakwa yao.
Kwa wenyeviti na watendaji
wengine wa vijiji ambao wamekuwa wakiogopwa kama
simba, hao watakula nao sahani moja kwa kuhakikisha kuwa wanabadilisha mwenendo
wao kwa ajili ya kufanikisha maisha bora kwa kila Mtanzania.
“Kwa mfano, kuna baadhi ya
wenyeviti wa vijiji ambao sera zao zinashangaza na hakika hawapendwi na
wananchi wao jambo linaloweza kukiangusha chama katika siku za usoni, hivyo
nimepangana na wenzangu kulisimamia hilo.
“Jambo hili nililifanya
mara baada ya kutangazwa kuwa mwenyekiti wa CCM Handeni, nikijua kuwa nitafanya
kazi kwa moyo wote kwa kushirikiana na viongozi wenzangu wa wilaya, akiwamo
Katibu wangu, Salehe Kikweo, bila kusahau viongozi kutoka ofisi za mkoa na
Taifa kwa ujumla, chini ya mwenyekiti wetu, Jakaya Mrisho Kikwete,” alisema.
Malunda anasema katika
wilaya yao
kumekuwa na ajenda za siri zinazofanywa na baadhi ya watumishi wakifanya mambo
kinyume ambayo wakati mwingine wanafanya kwa nia ya kukihujumu chama chao siku
za usoni.
Baadhi ya watumishi wa
umma katika wilaya hiyo wamekuwa wakishindwa kusimamia vyema miradi ya
maendeleo ya serikali, yakiwamo matatizo ya maji yanayowakabiri watu wa Handeni
na Vitongoji vyake.
Anasema wapo watu
wanaokubali uchimbaji visima vya maji kwa madai kuwa vipimo vyao vimegundua
uwepo wa maji katika eneo husika, lakini baada ya fedha kuwekwa kwa ajili ya
kufanikisha suala hilo,
hugundua kuwa mahala hapo hakuna maji.
Malunda anasema tabia hiyo
inaongeza shida ya maji pamoja na kejeli kutoka kwa watu ambao daima malengo yao ni kuona serikali ya CCM inashindwa kuwapatia maisha
bora Watanzania, licha ya kulipanga hilo
katika ilani zake.
“Hatuwezi kuchekea
matatizo ya aina hii, hivyo tutakwenda nao sambamba kwa ajili ya kuona
watendaji hao wanafanya kazi zao kama
inavyotakiwa, maana wapo chini ya serikali inayoongozwa na rais Jakaya Kikwete.
“Kama hawataki au siasa
zinawabana kwenye majukumu yao
waamuwe moja ili tukutane katika majukwaa ya siasa na sio kuwahujumu watu wa
Handeni kwasababu ya kukipaka matope chama chetu kinachopendwa na kuheshimika
Handeni nzima,” alisema Malunda.
Kama watendaji wote
watafanya kazi kwa kufuata sheria na sera za CCM zinazotekelezeka, hakuna
sababu ya wananchi wao kukiweka pembeni chama chao zaidi ya kukipa heshima
zaidi.
Juu ya suala la ardhi
inayoporwa kama njugu na watu kutoka nje ya Handeni, Malunda anasema
wanafurahia uwepo wa Mkuu wa wilaya wao mpya, Muhingo Rweyemamu kwa kufanya
kazi nzuri, ikiwamo kusimamia ardhi na elimu kwa watoto wa kike.
Mengine wanayofanya kwa
ajili ya Handeni yenye maendeleo ni kuhakikisha kuwa wajumbe wote wa CCM
Handeni wanafanya kazi za chama kama inavyotakiwa pamoja na kuvunja makundi
yao.
Aidha Malunda anasema
kwamba wenyeviti wao wote wamewaagisa kuongoza kwa kufuata weredi na
ushirikiano wao, ukiwapo kufanya mikutano ya mara kwa mara na wananchi wao,
hasa kwa kusoma mapato na matumizi.
Nafasi ya mwenyekiti wa
CCM wilaya ni ngumu, huku akiamini peke yake hawezi kuifanikishia chama chao
bila kupata ushirikiano kutoka kwa viongozi wengine wa chama wilaya, mkoa na
Taifa.
Kitu kinachompa imani ya
chama chao kuendelea kufanya vizuri katika wilaya yao ni kuona viongozi na
wanachama wao wote wapo kitu kimoja, jambo linalomfanya aone mazuri yataendelea
kupatikana.
Mwenyekiti huyo anasema
amekulia katika mikoa ya CCM tangu utoto wake, hasa kwa kuwa kwenye skauti na
kushiriki shughuli za kichama hadi anakuwa Mwenyekiti wa wilaya kwa kura
nyingi.
Wapo watu walioshindwa
kuelewa kuwa atafanikiwa kushika nafasi hiyo, huku kanuni zake za uzalendo,
mapenzi na moyo wa kukitumikia chama akikiweka mbele, jambo linalomfanya afanye
kazi ya chama wakati wowote.
Kuhusu maendeo ya pamoja
ya wilaya ya Handeni, Malunda anasema kwamba huruma na moyo wa dhati wa Mbunge
wao, Dk. Abdallah Omari Kigoda kunasababisha waone mazuri mengi, ikiwamo
barabara za kuunganisha wilaya na mikoa, vituo vya afya, shule za msingi na
sekondari zinazojengwa kila Kata.
Kwa wananchi na wadau
wengine wa Handeni wanapaswa kumpa ushirikiano mbunge wao huyo aliyeoingoza
Handeni kwa mafanikio makubwa, tangu alipopata nafasi hiyo miaka 15 iliyopita
na kupendwa na kila mtu.
Wapo watu ambao kwa namna
moja ama nyingine wanaweza kuiendeleza wilaya hiyo ya Handeni, lakini wanabaki
kimya wakiwa na hamu ya kuona mabaya ya kukosoa, jambo linalostahili kupingwa
na kila mtu.
“Handeni ni yetu wote
hivyo yoyote mwenye mapenzi mema anapaswa kushirikiana na uongozi kwa kupitia
sisi tuliopewa majukumu ya kichama, mbunge wetu Kigoda na ofisi za serikali
zikiongozwa na Mkuu wa wilaya, Muhingo.
“Naamini tukifanya hivyo,
neema itakuwa ya aina yake, hivyo kizazi chetu cha leo na kesho kuja kuishi
mahali pazuri, hasa kwa kudhibiti kwa vitendo suala la ardhi, elimu kwa watoto
wetu, kilimo bora na kukwepa uvunaji wa misitu ovyo,” alisema Malunda.
Bila shaka viongozi wa CCM
na Taifa kwa ujumla wanapaswa pia kuitumia nafasi hiyo ya watu wa Handeni
kuwapa nafasi za kuwaongoza, wafanye pia yale yanayoweza kulingana na fadhira
za watu wao, ukizingatia kwamba wameendelea kuwaona wao ndio wanaostahili
kuwapo madarakani kwa kupitia chama hicho kikongwe hapa nchini.
No comments:
Post a Comment