Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MSANII wa filamu hapa nchini, Elizebeth Michael maarufu kwa jina la Lulu,
ameanza kuona ahueni baada ya Mahakama ya Mkazi Kisutu, kuelezwa kuwa upelelezi
wa kesi ya mauaji dhidi ya msanii mwenzake, Steven Kanumba, umekamilika.
Kufuatia sakata hilo, Lulu sasa atasomewa
shtaka la kuua bila kukusudia badala ya mauaji jalada lake litakapofika
katika meza ya Mahakama Kuu.
Wakili wa Serikali, Ofmedy Mtenga alieleza mbele ya Hakimu Mkazi
Augustino Mmbando anayeisikiliza kesi ya msanii huyo aliyeacha gumzo katika
kuhusishwa na kifo cha Kanumba.
“Mheshimiwa Hakimu, kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa, hivyo upelelezi wake
umekamilika na mshitakiwa alitakiwa kusomewa muhtasari, ingawa Wakili wa
serikali, Tumaini Kweka hayupo,” alisema Mtenga.
Hata hivyo, Wakili wa mshitakiwa, Peter Kibatala aliiomba mahakama
kupanga tarehe ya karibu ili mshitakiwa asomewe muhtasari wa ushahidi dhidi ya
mashitaka yanayomkabili.
Hakimu Mmbando alikubali kuahirisha kesi hadi Desemba 21 mwaka huu kwa
ajili ya mshitakiwa kusomewa muhtasari wa ushahidi na kisha jalada la kesi
litafungwa, kesi itahamia Mahakama Kuu.
Mawakili wengine wanaomtetea msanii huyo
anayetingisha tasnia ya filamu kabla ya kufikwa na maswahibu hayo ni Kennedy Fungamtama,
Peter Kibatala na Fulgence Masawe.
Msanii huyo bado yupo rumande kwa miezi nane sasa kutokana na makosa ya mauaji kutokuwa na dhamana, huku akidaiwa kuwa Aprili 7 mwaka huu alimuua Kanumba, maeneo ya Vatican, Sinza, jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment