https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Sunday, December 23, 2012

Walimu Handeni wachachamaa



Na Amina Omari, Handeni
WANACHAMA wa Chama Cha Ushirika na mikopo cha Walimu (SACCOS), wa Wilaya za Handeni na Kilindi, wametishia kumfikisha Mahakamani Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani TangaHassan Mwachibuzi, kutokana na madai kwamba ameshindwa kuwalipa wanachama hao zaidi ya Sh 100 milioni.
Hayo waliyasemwa mapema wiki hii wakati wa mkutano Mkuu wa Mwaka wa Saccos hiyo yenye wanachama 900, uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Bwawani, wilayani Handeni.
Wajumbe hao walitoa mapendekezo hayo kufuatia taarifa ya Saccos hiyo iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake Mawazo Mohamedi, ikisema kwamba kati ya wanachama 200 waliokatwa makato ya mikopo pamoja na ya kawaida ya kila mwezi ni 14 pekee ndio fedha zao zimewasilishwa kwenye Saccos hiyo.
Mawazo alisema kwamba kufuatia fedha hizo kukaa kwenye akaunti ya Halamashauri hiyo kwa kipindi kirefu wamekuwa wakipoteza mapato yao, ambapo kila mwezi huwakopesha wanachama wao kiasi cha zaidi ya Sh 100 milioni kwa mwezi.
“Pesa hizo ni nyingi ingeweza kutusaidia kuwakopesha wanachama, faida ya Benki kwani fedha hizo zingekuwa kwenye akaunti yetu, badala ya kuwepo kwenye akaunti za halmashauri zikiendelea kutunisha faida ya akaunti yao.
“Swali tunalojiuliza halmashauri ya Kilindi wameweza kulipa fedha hizo je wao wanatumia mtandao gani na Handeni wanatumia upi,” alisema Mohamed .
Akizungumza katika mkutano huo Katibu Tawala wilayani hapa John Tiky, aliupongeza uongozi wa Saccos hiyo kwa kuweza kuimarisha mapato ya chama hicho kwa kujipatia faida ya Sh 56 milioni katika kipindi cha mwaka 2011/012.
Tiky aliwataka walimu kukopa kwa busara wakiwa na malengo na sababu za msingi kwa shughuli za maendeleo, ikiwemo kulipia ada na kujenga nyumba, badala ya kutumia fedha za mikopo kwa mambo yasiyo na tija.
Akijibu tuhuma hizo kwa njia ya simu wakati akizungumza na Gazeti hili, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Hassan Mwachibuzi, alisema kwamba kilichosababisha malipo hayo ni kutokana na mawasiliano katika Mtandao kuwa na matatizo.
“Ni kweli wanatudai lakini fedha zao hazijaliwa, tatizo ni kwamba huu mfumo mpya wa malipo kwa kutumia mtandao ulikuwa na tatizo, lakini sasa nadhani huenda wiki hii tatizo hilo halitakuwepo.
“Si wao tuu hata Afya pia wana fedha zao ambazo pia zimekwama kutokana na tatizo hilo, lakini Mwekahazina tulimtuma Dodoma kwenda kuweka mambo sawa. Wawe na subira tunatambua changamoto zinazowakabili,” alisema Mwachibuzi.


No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...