Francis Cheka akipima uzito
Na Rahimu Kambi, Arusha
BONDIA
mwenye makali ya kutisha hapa Tanzania,
Francis Cheka, jana usiku aliendeleza ubabe wake baada ya kumtandika kwa pointi
bondia kutoka Malawi,
Chimwemwe Chiotcha na kuleta shangwe kwa Watanzania.
Pambano
hilo lilipigwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha na Cheka
kushinda kwa pointi 118 kwa 114, 114 kwa 112 na pointi za mwisho kutolewa ni 120
kwa 115 dhidi ya Mmalawi huyo aliyekutana na mbabe wa Tanzania.
Mmalawi Chimwemwe Chiotcha
Ushindi
wa Cheka ni mwendelezo wa makali yake hasa akiwa na hamu zaidi ya kucheza
mapambano ya Kimataifa, baada ya kuona Tanzania amekosa mpinzani na
kuwapiga kila siku mabondia wazawa.
Kwa siku
kadhaa, Cheka alikuwa akijiwinda kwa ajili ya pambano hilo lililokuwa na upinzani wa hali ya juu,
kwani ingawa ameshinda, lakini Mmalawi huyo hakuwa lele mama na kulazimisha
apigwe kwa pointi.
Pambano hilo lilikuwa na upinzani
wa hali ya juu, kwani tangu asubuhi walipokuwa wakipima uzito katika Hoteli ya Naura
Springs, wababe hao walikuwa wakionyeshana umwamba na shari ya kutaka kudundana
kavu kavu.
Hali
hiyo iliongeza joto na msisimko wa pambano hilo lililomalizika usiku katika Uwanja huo
na kuleta shangwe kwa Watanzania, kutokana na bondia wao mwenye maskani yake
mjini Morogoro kuendeleza majigambo yake kwa kutoa dawa kwa kila anayekutana
naye.
No comments:
Post a Comment