Nidhamu iangaliwe upya na wanasoka
wetu
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WATAALAMU wengi katika mpira wa
miguu wanailezea nidhamu kama silaha ya kuwaletea mafanikio makubwa wachezaji
wetu. Sio Tanzania tu, bali na Dunia nzima suala la nidhyamu hupewa kipaumbele
na wanasoka wetu.
Bila nidhamu, wachezaji ni ngumu
kwao kuwika, ndio maana katika kila timu, wamewekwa watu wa kuwaongoza wana
michezo wetu, hasa wa mpira wa miguu, ili iwe nafasi yao ya kuonyesha makali
yao.
Licha ya kuwa na vipaji vya aina
yake, lakini wachezaji ambao nidhamu kwao ni mtihani mgumu, hakika hawana
sababu ya kukubalika katika soka. Ni watu wa kucheza nyumbani kwao. Wakivuka
mpaka, hushindwa na kurudi tena kwao.
Wakiwa kwao nao huvuma na
kusahaulika, kwakuwa makocha wenye kanuni zao haswa, kuwatumia wachezaji wa
aina hiyo ni ngumu sana. Hayo ni matatizo ya wachezaji wa Tanzania. Wengi wao
hawaipendi nidhamu.
Wapo tayari kukwepa mazoezi au
kusingizia ugonjwa. Wasipokwepa mazoezi, basi hujiweka bila kufuata ushauri wa
walimu wao, hivyo kuanza kuibua mzozo mzito unaosababisha vurumai katika
nyakati mbalimbali.
Kwa kulijua hilo, wachezaji wetu
wana kila sababu ya kuangalia malengo yao katika soka. Kama wana ndoto za
kucheza soka la kulipwa, basi wajuwe bila kuwa na nidhamu, kuwaheshimu
wachezaji wenzake na makocha wao ni ngumu.
Kuwa na nidhamu ndani na nje ya
uwanja, kunaleta mvuto na ufanisi mkubwa wa kujiweka juu katika ramani ya soka.
Angalia, mshambuliaji tegemeo wa Simba, Haruna Moshi Boban, amekuwa akiingia
lawamani kila wakati.
Juzi aliwaambia viongozi na kocha
wake kuwa ni mgonjwa, hivyo hataweza kwenda Tanga kucheza na Mgambo Shooting,
mchezo uliomalizika kwa timu hizo kugawana pointi.
Lakini, siku moja baadaye Boban
alionekana uwanjani akicheza kwenye timu za mchangani, jambo ambalo ni baya
sana. Hili haliwezi kumsaidia kamwe.
Ndio, huenda ameshajua kwa umri wake
ni ngumu tena kufikia mafanikio yaw engine duniani, lakini tabia yake inaharibu
kizazi cha wanamichezo, ukiwamo huo mpira wa miguu.
Wale wachezaji wadogo wanaopenda
kuwa kama yeye, wanajifunza nini kutoka kwake? Sio Boban tu, baali wachezaji
wengi wa Tanzania hayo ndio mapungufu yao. Mara kadhaa wanachofundishwa katika
mazoezi ni tofauti na wanachokionyesha.
Haya hayastahili kuchekewa kamwe.
Wachezaji wetu lazima wajuwe na namna ya kung’amua namna ya kujiendesha kama
kweli wanahitaji kuwa wana soka wa kulipwa. Bila hivyo wataendelea kupoteza
muda wao au kuishia vihela vya kula nyumbani kwao.
Ukiangalia kwa haraka, utagundua
kwamba kila anayevuma duniani nidhamu anayo. Mchezaji kama huyu Mbwana Samatta,
Thomas Ulimwengu, wanaweza kutimiza ndoto zao, maana nidhamu wanazo na wana kiu
ya mafanikio.
Mtu kama vile Henry Joseph Shindika
anayecheza soka la kulipwa Norway, nidhamu anayo, ndio maana alikuwa chaguo la
kocha Marcio Maximo na wengine waliorithi kiatu chake. Hatuwezi kukimbia
nidhamu. Yoyote anapaswa kuwa nayo, wakiwamo wanamichezo.
Wachezaji wetu wa Tanzania lazima
wajuwe kuwa mafanikio yao yatachangiwa na mambo mengi sana, ikiwamo hiyo
nidhamu inayoliliwa na kila mmoja wetu. Maximo, aliwahi kusema hilo mara kwa mara
kuwa wengi aliowafungia vioo hawana nidhamu.
Wachezaji kama vile Juma Kaseja,
Boban, Athuman Idd na wengine, aliwalilia sana. Waliokuwa hawataki uamuzi wake
huo, walilazimishwa kuukubali. Makocha hao wanafanya hivyo kwakujua kuwa ni
muhimu kwa ajili ya mafanikio yao.
Kinyume cha hapo, wachezaji wetu wa
Tanzania wasiopenda kuikumbatia nidhamu ndani na nje ya uwanja, wajaribu na
kazi nyingine maana kuvuna fedha nyingi kama wanavyofanya wengineo duniani,
hilo ni jambo gumu mno.
Kwa bahati mbaya, wapo wachezaji
ambao kitu kama hicho kwao ni kigumu na ndio maana wanashindwa kuwika.
Wanacheza soka la ndani miaka yote. Kuna wachezaji ambao husingizia wanaumwa,
lakini baadaye huonekana wakicheza soka la mchangani.
Ama wengine kutoripoti kambini kwa
wakati au kutoa visingizio vya kila aina, hivyo kuwaharibia kwa kiasi kikubwa.
Huu ni muda wa mabadiliko kwa wachezaji wetu. Na ndio maana siwezi kuvumilia
katika hilo.
Tukutane wiki ijayo.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment