Na Kambi Mbwana, Handeni
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi
wilayani Handeni, Athuman Malunda, amesema kuwa baadhi ya wenyeviti wa serikali
ya vijiji ni watu wanaopenda kujiweka juu na kushindwa kuongoza kwa ufanisi.
Hali hiyo inaweza kuwaangusha kama
hawataweza kujirekebisha kwa faida ya vijiji vyao, chama na serikali kwa
ujumla, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa, baadaye mwakani.
Akizungumza jana mjini hapa na
Handeni Kwetu, Malunda alisema wenyeviti hao wanajiona wao ni miungu watu kwa
kutaka waabudiwe, sambamba na kushindwa kuitisha mikutano ya vijiji vyao, hivyo
ni jambo baya.
Alisema kwakuwa wenyeviti hao wapo
chini ya chama chao, watahakikisha kuwa wanawaongoza vizuri kwa ajili ya
kufanya kazi zao kwa ufanisi ikiwa ni hatua nzuri ya kushinda katika uchaguzi
huo wilaya nzima.
“Wenyeviti wa aina hiyo hatuwezi kuwachekea
kwa kuwafanya wawachukize wananchi wao, badala yake tunataka wajishushe kabisa
kwa wananchi, ukizingatia kuwa ni hatua nzuri katika hali ya kuleta maendeleo.
“Bila hivyo, wananchi watakuwa na
chuki nao, hivyo kushindwa kuleta maisha bora sambamba na kukiangusha chama
chetu kinachopendwa na kuheshimiwa na Watanzania wote, ndio maana Handeni
hakuna mwenyekiti wa upinzani wa vijiji vyetu,” alisema.
Wilaya ya Handeni ni miongoni mwa
wilaya za Tanzania Bara ambazo vyama vya Upinzani vimeshindwa kufurukuta katika
chaguzi mbalimbali, tangu kuingia kwa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.
No comments:
Post a Comment