MGODI UNAOTEMBEA
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KABLA ya kuanza kufikiria labda kuna mkono wa mtu au Taifa
kutoka nje ya nchi yetu, vyema tukaelewa kuwa siku zote mvunja nchi ni
mwananchi mwenyewe, hasa kwa kuangalia jinsi baadhi yao wanavyokosa uzalendo na kutenda yasiyokuwa ya kiungwana.
Watu hao wamekuwa wakiendeleza kufanya vitendo vya
kushangaza na kuogopesha kwa kiasi kikubwa, ikiwa ni njia moja wapo
inayolitangaza Taifa letu vibaya nje ya nchi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.
Tangu kupata Uhuru uliopatikana kwa harakati za viongozi
wetu, akiwamo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na wapambanaji
wengine, Tanzania ilijipambanua kuwa ni kisima cha amani. Soma zaidi....
Katika kulinda msingi huo, wananchi walielimishwa au kupewa
kauli mbiu ya namna gani wanavyotakiwa waishi kwa ajili ya kuishi kwa amani na
upendo ili kukuza uchumi wa nchi yetu.
Ni kweli kabisa. Kiu hiyo ilidumu kwa miaka mingi, ingawa
sasa naanza kuona kuwa hali hiyo imekwisha. Anayesema kuwa nchi hii bado ni
kisiwa cha amani, hakika anatumia lugha nzuri kwa kuhofu anayewaeleza hivyo
wataondoa woga kwa sababu moja ama nyingine.
Kwanini nasema hayo? Taifa letu sasa lipo kwenye matatizo
makubwa ya vurugu za kidini, siasa na mambo mengine ambayo yote kwa pamoja
yanawaweka wananchi kwenye wasiwasi mkubwa.
Kumekuwa na matukio mengi ya kutisha. Katika kulielezea
jambo hilo la machafuko ya Tanzania, wengi watawataja watu maarufu au wale
ambao matukio yao yamegusa watu wengi.
Lakini ukweli ni kwamba hao wanaotajwa ni wachache kati ya
wengi ambao labda kwa kutokuwa maarufu kwao, au kutojulikana kwa madhira
yaliyowakuta, kunawafanya wasionekane yale yaliyowatendewa.
Ingawa watu watawataja watu kama vile Mwandishi Daudi
Mwangosi, mtu
aliyepoteza maisha kwa staili ya kutisha kupita kiasi. Mbali na
Mwangosi, bado wapo watu kama vile Daktari Stephen Ulimboka, Mhariri wa
Mtendaji wa Kampuni ya New Habari 2006 (Ltd), Absalom Kibanda ambao matukio yao
ya kutekwa na kuteswa yamewagusa watu wengi na kuendeleza msemo kuwa Tanzania
sasa si kisiwa cha amani.
Mbali na watu hao, ambao kwa mapenzi ya Mungu wameendelea
kubarikiwa uhai, wapo ambao wamepoteza maisha, akiwamo Padri Evarist Mushi wa
Kanisa Katoliki Visiwani Zanzibar.
Padri huyu aliuagwa na kuibua hisia nzito sambamba na kuzidi
kueneza chuki kwa miongoni mwa jamii ya Kitanzania. Pamoja na yote hayo, bado
wapo wananchi ambao wamekuwa wakiishi bila kuvumiliana kwa sababu za ajabu,
hasa huu wimbo wa kuchinja unaoendelea kuimbwa kwa lugha za chuki na kukiathiri
kizazi cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tangu kuzaliwa kwa Taifa hili, likipita katika vipindi
tofauti kwa viongozi tofauti waliokuwa na mapenzi makubwa kwa wananchi wao,
watu waliishi kwa upendo na kuvumiliana kupita kiasi.
Si kama ukatili haukuwapo, huenda ulikuwapo, ila si kama
ulivyokuwa sasa kiasi cha watu kushikwa na mihemko na kutenda bila hata kuogopa
vyombo vya Dola katika mazingira wanayotaka wao.
Hii si njia nzuri ya kuzalisha amani kwa Watanzania. Zaidi
tunaendeleza chuki, fitina, majungu na kusababisha sumu mbaya ya vurugu ambazo
kuna siku zitashindwa kumalizwa.
Katika kutafuta nufumbuzi juu ya machafuko ambayo mengi
huibuka kwa kupita mgongo wa dini na siasa, baadhi ya watendaji wa serikali,
wanashindwa kutumia busara, hekima na utu juu ya kumaliza migogoro hiyo.
Kuna siku tutashuhudia watu wakiingia barabarani kufanya uhalifu,
maana tayari walishazoea na kuona kuwa hakuna wa kuwazuia kwa namna moja ama
nyingine.
Katika kuliangalia Taifa lenye amani, hatupaswi kuchekea
kauli za uchochezi zinazotoka kwa mtu yoyote, iwe ni mwanasiasa au kiongozi wa
dini ambaye hana uzalendo na wananchi wake.
Huo ndio ukweli. Mihemko yako haiwezi kutufanya tuone upo
sahihi hata pale utakaposimama kwa kupitia cheo chako cha kidini au kisiasa
kuhamasisha vurugu hatari kwa Taifa hili.
Hatuwezi kwenda hivyo. Bado hatuna uchumi unaotufanya
tulinge kuwa tutakuwa pazuri hata kama baadhi ya watu watafanya vurugu,
wataharibu miundo mbinu yao kwasababu ya kuhamasisha ujinga kutoka kwa mtu
mmoja asiyekuwa mzalendo.
Kwa mfano, wapo watu ambao wanabishana juu ya nani yupo
sahihi katika suala zima la kuchinja. Sakata hili lilibuliwa na Waziri Stephen
Wasira, alipokuwa anazungumza jijini Mwanza.
Mengi yaliendelea kuibuka hasa pale Wasira alipojikuta
akitoa ufafanuzi kuwa mwenye mamlaka ya kuchinja ni Waislamu. Kauli ya Wasira
isingeleta matatizo kama watu watatumia akili na uzalendo kufuatilia suala
hili.
Kuna uwezekano mkubwa kuwa huenda Wasira amezungumza hivyo
kwasababu ndio utaratibu uliozoeleka kwa Watanzania wengi. Hata wachungaji,
mapadri walikuwa wakitaka kufanya shughuli inayoshirikisha watu wa jamii tofauti,
vitoweo vyao vilikuwa lazima vichinjwe na Waislamu.
Pamoja na yote hayo, watu ambao ni jamii ya Wakristo
hawakulazimishwa pia wachinjiwe na Waislamu kama hawajaona hilo linafaa, ingawa
tatizo litakuwa pale wanapochinja wao na kuwalisha wengine.
Kumbe leo wapo watu wanaotaka wachinje, basi sakata hilo
linastahili viongozi wakae na kushirikisha makundi ya kijamii hasa kwa viongozi
wao wa dini, Mashekhe, Mapadri na wengineo.
Wakati hayo yakiendelea, watu wanahoji. Je, vurugu hizo
mwisho wake ni wapi? Ingawa wapo wanaosema kuwa vurugu hizi zina mkono wa mtu,
wakimaanisha watu wanaotumiwa na wengine kutoka nje ya nchi, lakini bado
hainifanyi nishindwe kuwataja watu hao kama majuha na wasiokuwa na uzalendo
katika Taifa lao.
Watu hao ambao lengo lao kubwa ni kuiweka nchi katika
mtihani mzito, hasa katika kiu ya kuilinda amani yake, hawastahili kuchekewa
hata mara moja, maana wanavyoendelea kuchekewa, ndivyo sumu hiyo inavyozidi
kuenea na kuota mizizi hata kwa wale wasiokuwa na tabia hiyo.
Kila mtu wakiwamo viongozi wa serikali, chini ya Rais Jakaya
Mrisho Kikwete kwa upande wa Bara na Dk. Ali Mohamed Shein kwa upande wa
Visiwani kuendelea kuwa wakali kwa kundi lolote, mtu yoyote anayefanya uvunjifu
wa amani kwa makusudi kwa faida anayoijua mwenyewe.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi pamoja na vyombo vya ulinzi
na usalama vihakikishe kuwa vinakuwa mstari wa mbele, pamoja na kutoa elimu kwa
wananchi juu ya kulinda amani na mustakabali wa Tanzania.
Leo tunaona ni kawaida, lakini ikiendelea hivi, kila mmoja
ataona ana uhuru wa kufanya kila analotaka, hivyo kusababisha machafuko, mauaji
ya watu wasiokuwa na hatia, hasa tatizo hilo linapopitia kwa mlango wa dini au
vyama vya siasa, kama vile Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama
Cha Wananchi (CUF), Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vingine vya siasa
vilivyosajiliwa katika nchi yetu.
Huu ndio ukweli wa mambo. Tusipokuwa makini, kujua nini cha
kufanya kwa ajili ya nchi yetu, hakika hatutakuwa na kizazi chenye uzalendo,
kinachoithamini amani kwa ajili ya kulinda utu na heshima za watu.
Tuna wajibu wa kulijua hili, maana inapotokea machafuko
makubwa, wanaoathirika ni akina mama na watoto, hivyo ni wazi hawa wanaofanya
vitendo vya unyama kwa wenzao, wale wananaokesha kubuni namna ya kufanya vurugu
za kidini na kisiasa wafikie wakati waone imetosha kwa ajili ya kuendeleza
wimbo wetu wa Tanzania kisiwa cha amani.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment