Waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kushoto na Abeid Amani Karume, wote kwa sasa ni marehemu.
Ni siku muhimu kwa Watanzania
wote. Baba, mama, mjomba na shangazi kuanzia siku ya kwanza ya Muungano huu
hadi leo, wanaikumbuka na kuitilia mkazo.
Sherehe za Muungano Kitaifa
zinafanyika katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, ambapo wananchi na
viongozi wanashiriki kwenye maadhimisho hayo.
Pamoja na sherehe hizo, kila
Mtanzania na asiyokuwa Mtanzania anapaswa kujua kuwa Mkataba wa Muungano
ulitiwa saini na Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume, Aprili 22, 1964,
Zanzibar.
Ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika
na Baraza la Mapinduzi Aprili 26, 1964, na Aprili 27, 1964 viongozi hao
walikutana katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Dalaam kubadilishana hati
za Muungano.
Sheria za Muungano ilitamka
kwamba, Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zililazimika, kuwa dola ya Jamhuri kwa jina la Jamhuri ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, jina ambalo lilibadilishwa Oktoba 28, 1964
na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia sheria ya Jamhuri ya Muungano,
sheria namba 61, ya mwaka 1964.
Msingi wa katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ni Hati
za Muungano za Mwaka 1964.
Hati za Muungano zilitiwa saini na
Nyerere na Karume, Aprili 22, 1964 na hapo Tanganyika na Zanzibar kuwa dola
moja kwa misngi inayotambulika kimataifa.
Baada ya kuungana, Mwalimu Nyerere
alikuwa rais wa kwanza na Karume alikuwa makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Aprili 26, 1964, bunge la
Tanganyika lilipitisha sheria za Muungano, ambazo baadayezilithibitishwa na
Baraza la Mapinduzi Zanzibar.
Mnamo Aprili 27, 1964 waasisi wa
Muungano walibadilishana Hati za Muungano na wajumbe saba wa Baraza la
Mapinduzi waliapishwa kuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Watanganyika
na Zanzibar ambao ni Amani Karume, Kassim Abdallah Hanga, Abdulrahman Babu,
Hassan Nassor Moyo, Aboud Jumbe, Hasnu Makame na Idris Abdul Wakil. Kati yao,
Aboud Jumbe na Hassan Nassor Moyo wangali hai.
Katiba ya muda ya mwaka 1965 ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianisha mambo 11 ambayo yalikubalika kuwa ni
ya Muungano ambayo ni;
Katiba na Serikali ya Muungano, Mambo ya nchi za nje,
Ulinzi, Polisi, Mamlaka juu ya mambo yanayohusika na hali ya hatari, Uraia,
Uhamiaji,
Mikopo na Biashara za nje, Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya
Muungano, Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa
forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa Tanzania unaosimamiwa na idara ya
forodha, Bandari, mambo yanayohusika na usafiri wa anga, posta na simu.
Katiba ya muda ya mwaka 1965
ilianisha utawala wa serikali ya mfumo wa chama kimoja, TANU kwa Bara na ASP
kwa Zanzibar. Katiba hii, ilizingatia misingi ya makubaliano ya Muungano ya
mwaka 1964 na sheria za Muungano wa Tangayika za Zanzibar.
Katiba hiyo ilianisha serikali
mbili, uwakilishi wa Zanzibar katika bunge la Muungano ikiwa na mamlaka juu ya
mambo yote ya Muungano na mambo yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanganyika. Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar ikiwa na mamlaka juu ya mambo yote yasiyo ya Muungano yahusuyo
Zanzibar.
Hata hivyo mambo ya Muungano
yaliongezwa kutoka 11 hadi 22 kutokana na mahitaji ya ndani ya nchi pamoja na
mabadiliko yaliyokuwa yanaendelea kutokea ulimwengini baada ya Muungano.
Mwaka 1985, jambo la 12 linalohusu
sarafu na fedha kwa ajili ya malipo na kurahisisha usimamizi wa fedha za kigeni
na benki katika Jamhuri ya Muunagno wa Tanzania, liliingizwa.
Kufuatia kuundwa kwa Jumuiya ya
Afrika Mashariki mwaka 1967, mambo matatu ya Muungano yaliyongezwa, ambayo ni
leseni za viwanda na takwimu; elimu ya juu; na usafirishaji wa anga.
Mwaka 1968, mambo ya maliasili ya
mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya magari na ama ya petroli na aina
nyingine za mafuta au bidhaa na gesi asilia yaliyongezwa kwenye orodha hiyo.
Aidha mambo ya Muungano
yaliendelea kuongezeka hadi kufikia 21 kufuatia kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mwaka 1992 kufuatia mabadiliko ya
mfumo wa siasa nchini suala la 22 la uandikishaji wa vyama vya siasa na mambo
mengine yanayohusiana navyo liliongezwa kwenye orodha hiyo.
MUHIMU LA KUZINGATIA
Katika miaka hivi karibuni
kumekuwa na mijadala mbalimbali kuhusiana na muundo wa Muungano, baadhi
wakitaka uwe wa zaidi ya serikali mbili, wengine serikali moja, wapo wanaotaka
Tanganyika iwe kivyake na Zanzibar kivyake.
Hata hivyo hekima inaonyesha
kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unabaki kuwa ni fahari ya Watanzania,
kwani mwelekeo wa dunia katika nyanja mbalimbali, mataifa kuungana kwa
ushirikiano wa aina mbalimbali ni muhimu kuliko taifa moja kupambana kivyake.
Urejeaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada
ya kuvunjika mwaka 1977, uwepo wa SADC, ECOWAS, COMESA, na jumuiya nyingine
nyingi duniani kote, ni vielelezo kwamba ushirikiano baina ya mataifa ni suala
lisilohitaji mjadala.
Ieleweke kwamba hakuna ushirikiano
usio kuwa na matatizo kama ilivyo kwa Muungano wa Tanzania, vivyo hivyo
muungano mwingine kama vile ya United Kingdom (UK), Uingereza na United States
of America (USA) kwa maana ya Marekani na United Arabs Emirate (UAE), nayo ina
matatizo, lakini hata mara moja mjadala juu ya matatizo hayo siyo kuvunja
ushirikiano bali kutatua na wale wanaotaka kuvunja hushughulikiwa ipasavyo.
Tunawatakia Watanzania wote Sikukuu njema ya Muungano.
No comments:
Post a Comment