https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Tuesday, April 02, 2013

Wizara ya Maliasili yashikilia msimamo wa serikali, sakata la Pori la Loliondo



Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki.
Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii, George Matiko.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SAKATA la mgogoro wa Hifadhi ya Loliondo, limezidi kuchukua sura mpya, baada ya Serikali kupitia kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kusema haitabadili uamuzi uliyotoa kuhusu Pori Tengefu la Loliondo, mkoani Arusha na kuwataka wanaharakati wanaochochea mgogoro huo kuacha mara moja kwa manufaa ya Taifa.

Tamko hilo la serikali, limekuja muda mfupi baada ya watu mbalimbali
kutoa maoni yao kwenye mitandao na vyombo vya habari kwamba uamuzi wa serikali kuhusu pori tengefu si sahihi.


Tamko la serikali lilitangazwa na Waziri wa Maliasili na Utalii,
Balozi Khamis Kagasheki hivi karibuni kwamba, wameacha  kilomita za
mraba 25,000 kwa ajili ya wananchi na serikali imechukua kilomita za
mraba 15,00 kwa ajili ya kutunza rasilimali za nchi, jambo ambalo lilitafsiliwa kama mwarobaini wa mgogoro huo, licha ya kushuhudia baadhi yao wakiendelea kuupinga.


Alifanya hivyo kwa kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya
Mwaka 2009, Sehemu ya 16 Vifungu Na. 4, 5 na 6 na kwamba muda mrefu
viongozi wa wizara wamekuwa wakikutana na wananchi na viongozi wa mkoa wa Arusha na Wilaya ya Ngorongoro kujua kero zilizopo ili zitatuliwe
na ndio imewezesha serikali kufanya uamuzi alioufanya.

"Ukweli ni kuwa Waziri Kagasheki alifuata sheria alipotoa tamko kuhusu
kupunguza eneo la pori tengefu la Loliondo kwa mujibu wa sheria
inayompatia waziri mwenye dhamana uwezo wa kupitia upya mapori tengefu na kufanya marekebisho mbalimbali muhimu kwa manufaa ya wananchi bila kuathiri uhifadhi,"alisema George Matiko, ambaye ni msemaji wa wizara.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari jana, Matiko alisema tamko
lilizingatia tafiti mbalimbali ikiwemo utafiti wa  Taasisi ya Utafiti
wa Wanyamapori (TAWIRI) na mapendekezo ya tume mbalimbali zilizoundwa kuchunguza mgogoro wa Loliondo ikiwemo ya Waziri Mkuu iliyoundwa mwaka
juzi.

Aliongeza kuwa eneo la kilomita za mraba 1,500 litaendelea kumilikiwa
na wizara kwa mujibu wa sheria na kwa kutambua kuwa ni sehemu ya
mazalia ya wanyamapori, mapito ya wanyamapori na vyanzo vikuu  vya
maji kwa hifadhi mbalimbali ikiwemo Serengeti.

Alisisitiza ardhi iliyobaki baada ya kuondoa eneo la pori tengefu la
Loliondo itasimamiwa na vijiji kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji
Namba 5 ya Mwaka 1999 na wananchi watawezeshwa ili waanzishe Eneo la
Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) katika ardhi hiyo kwa manufaa yao, hivyo wanaojaribu kupita na kuwarubuni wananchi ni kutowatendea haki.

"Tanzania inajali uhifadhi lakini pia inajali maslahi ya wananchi,
ndiyo maana asilimia 25 ya eneo la nchi hii limehifadhiwa bila kuwepo
migogoro. Hakuna migogoro kati ya wananchi na Serikali, kwa kuwa
wananchi wanatambua umuhimu wa uhifadhi kwao na kwa vizazi vijavyo.
Ndiyo maana wananchi wanachangia kwa kiwango kikubwa katika
kufanikisha uhifadhi,"alimaliza Matiko.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...