Na Rahimu Kambi, Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) limesema kuwa ujumbe
wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) utawasili nchini Jumatatu ya Aprili 15 mwaka huu kwa ajili ya kushughulikia mchakato wa uchaguzi mkuu wa
TFF.
Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF akiwa na Rais wake, Leodgar Tenga
Kwa mujibu wa taarifa
kutoka FIFA, ujumbe huo utaongozwa na Mkuu wa Idara ya Uanachama ya FIFA, Primo
Covarro na utafanya kazi kwa siku tatu kuanzia siku ya ujio na kuondoka Aprili
18 mwaka huu.
Ukiwa nchini, ujumbe huo
utakutana na wagombea uongozi walioathiriwa na uamuzi wa Kamati ya Rufani ya
Uchaguzi ya TFF ambao waliomba mashauri yao yaangaliwe upya, wagombea ambao
walikata rufani FIFA, Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Kamati ya Rufani na
Sekretarieti ya TFF.
Wajumbe hao wangependa
kukutana na waziri anayehusika na michezo, hivyo TFF imeiandikia Wizara
ikipendekeza kuwa ujumbe huo ukutane na Waziri na wakuu wengine wa michezo
Aprili 16 mwaka huu 2013 kabla ya kuanza kazi zao.
Wagombea
watakaosikilizwa na ujumbe huo wa FIFA ni:
1. Farid Salim Mbaraka Nahdi: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa
Kamati ya Utendaji ambaye alienguliwa na Kamati ya Uchaguzi na baadaye rufani
yake kwa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF kutupwa na hali kadhalika ombi
lake la kutaka shauri lake liangaliwe upya, kukataliwa.
2. Elliud Peter Mvella: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati
ya Utendaji ambaye alikatwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF na kukata rufani
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF kabla ya maombi yake ya kutaka shauri lake
kuangaliwa upya, kukataliwa.
3. Mbasha Matutu: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya
Utendaji ambaye alikatwa na Kamati ya Uchaguzi na kukata rufani ambayo pia
ilitupwa kabla ya kuomba shauri lake liangaliwe upya, ombi ambalo lilikataliwa.
4. Hamad Yahya: Mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Bodi ya Ligi
ambaye alipitishwa na Kamati ya Uchaguzi, lakini mwekaji pingamizi akakata
rufani ambayo ilikubaliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF na kuondolewa.
Aliomba shauri lake liangaliwe upya, lakini Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF
ikatupa ombi lake.
5. Jamal Emily Malinzi: Mgombea wa nafasi ya urais wa TFF
ambaye alipitishwa na Kamati ya Uchaguzi, lakini mwekaji pingamizi akakata
rufani ambayo ilikubaliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF, hivyo
kuondolewa kwenye mchakato. Aliomba shauri lake liangaliwe upya, lakini
likakataliwa. Hata hivyo, alikuwa ameshakata rufani FIFA.
6. Michael Wambura: Mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF
ambaye alikatwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF na rufani yake kukataliwa na
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF. Hakuomba shauri lake liangaliwe upya,
lakini alikata rufani FIFA.
Shirikisho linawaomba
wote waliotajwa hapo juu kujiandaa kwa utetezi na maelezo ya kutosha na kwamba
barua za kuwaita zinafuata. (Orodha ya
waathiriwa na programu ya ujumbe wa FIFA imeambatanishwa)
No comments:
Post a Comment